Watanzania wametakiwa kutokuwa sehemu ya kundi la wanaotumiwa kisiasa kupotosha mafanikio na Maendeleo yanayopatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali
Wito huo umetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Iringa katika ziara yake ya kuimarisha chama na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kihongosi amesema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia majukwaa ya kisiasa kubeza na kupunguza thamani ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, licha ya ushahidi wa miradi inayotekelezwa kuonekana wazi katika sekta mbalimbali.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu, hatua iliyosaidia kuboresha huduma za kijamii na kuongeza fursa za maendeleo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Kihongosi, ni muhimu wananchi kutathmini maendeleo kwa kuangalia matokeo yanayoonekana badala ya kuamini kauli za kisiasa zinazolenga kupotosha ukweli kuhusu kazi zinazofanywa na Serikali.
Amesisitiza kuwa CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani yake pamoja na kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Ziara ya Kihongosi katika Mkoa wa Iringa ni sehemu ya kampeni ya chama hicho ya kuhamasisha wananchi kutambua na kuthamini mafanikio ya Serikali sambamba na kuimarisha shughuli za chama ngazi za msingi.
(Feed generated with FetchRSS)