Dar es Salaam. Nyuma ya mafanikio makubwa ya mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Fally Ipupa, kuna simulizi ya mapenzi iliyobeba uvumilivu, imani na kusimama pamoja katika nyakati za shida.
Hadithi ya Fally na mpenzi wake wa muda mrefu, Nana Ketchup, ilianza mwishoni mwa miaka ya 1990. Wakati msanii huyo akiwa bado hajajijengea jina katika tasnia ya muziki.
Wakati huo, Fally alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa za kufanikiwa lakini maisha yake hayakuwa mepesi. Hakuwa na umaarufu wala uwezo mkubwa wa kifedha, hali iliyowafanya baadhi ya watu kutokuwa na imani naye.
Kutokana na mwonekano wake mwembamba na hali yake ya maisha. Baadhi ya watu wa karibu wa Nana walimpa jina la utani la “Puku”, likiwa na maana ya kumdharau na kuonyesha kwamba hawakumuona kama mwanaume ambaye angeweza kufanikiwa maishani.
Shinikizo kwa Nana lilikuwa kubwa. Baadhi ya ndugu na marafiki walimtaka aachane na Fally na kutafuta mwanaume mwingine mwenye uwezo zaidi wa kifedha.
Hata hivyo, Nana alichagua kubaki upande wake, akiamini kuwa siku moja ndoto zake zingetimia. Katika mahojiano mbalimbali aliyowahi kufanywa Fally ameeleza kuwa, kulikuwa na vipindi vigumu ambapo hata chakula kilikuwa changamoto.
Katika nyakati hizo, Nana ndiye aliyekuwa akimtia moyo, kumuuliza kama amekula na kumsaidia kwa uwezo wake wote huku akiendelea kumuamini.
Kadri miaka ilivyosonga mbele, ndoto za Fally zilianza kutimia. Kutoka kuwa kijana aliyedharauliwa na wengi. Na kuwa mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika, akijaza maelfu ya mashabiki katika maonyesho yake na kujenga jina kubwa katika muziki wa kimataifa.
Matunda ya safari yao ya pamoja yanaonekana pia katika familia yao. Wawili hao wamejaliwa watoto watano wanaofahamika kwa majina ya Marcosins, Vincenzo, Jaden, Malka Monikel na Fanalya.
Ingawa kwa miaka mingi kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu ndoa yao, tarehe rasmi ya kufunga ndoa haijawahi kuthibitishwa hadharani.
Simulizi ya Fally na Nana ni simulizi ya mwanamke aliyesimama na mwanaume wake wakati hakuwa na chochote. Fally ni miongoni mwa majina makubwa katika muziki wa bara hili, safari ya Fally Ipupa imeendelea kuwa ushahidi kwamba wakati mwingine mtu mmoja anayekuamini anaweza kubadili mwelekeo wa maisha yako.