NI mshikemshike, hayawi hayawi au mtoto hatumwi dukani.’ Unaweza kuchagua neno lolote upendalo kuonyesha ushindani uliopo katika kuepuka upangaji matokeo mechi tatu za mwisho wa Ligi Kuu Bara na zitakazochezwa kwa muda mmoja katika viwanja tofauti.

Katika mbio za ubingwa, wakongwe Yanga (pointi 66) na Simba (64) zinakabana koo kwa tofauti ya pointi mbili na lolote linaweza kutokea. Hiyo tisa, kumi kule chini ya msimamo kuna vita kubwa na timu nane hazipo salama zikiwania kukwepa kuungana na KMC kucheza Ligi ya Championship msimu ujao.

Umuhimu wa mechi hizo umewafanya Bodi ya Ligi Kuu Bara kuchukua uamuzi mgumu tofauti na misi-mu iliyopita, msimu huu raundi tatu za ligi zilisosalia kila moja itachezwa siku moja na muda mmoja, kila timu ikitumia uwanja wake kumalizia mechi hizo tatu.

Vumbi hilo litaanza kutimka kesho Jumatano kuanzia saa 10:00 jioni na hakuna uwanja utakaotumika kwa mechi mbili kila timu itatumia uwanja wake hatua ambayo imezitawanya Simba na Yanga zikianza hesabu mpya.

Yanga iliyokuwa jijini Mwanza, Uwanja wa CCM Kirumba ikicheza mechi ya Nusu Fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho la CRDB, ilitaka kutumia uwanja huo kucheza dhidi ya matajiri hao wa Chamazi kwenye mechi ya ligi. Hata hivyo, mpango huo ukagoma baada ya Pamba Jiji awali kuwasilisha maombi ya kuutumia uwanja huo kwenye mechi yake ya Juni 24,2026 itakapokuwa mwenyeji wa Mbeya City.

Yanga pia isingeweza kucheza mechi yake dhidi ya Azam Uwanja wa KMC na siku husika wamiliki wa uwanja huo nao watakuwa na mechi ya nyumbani dhidi ya Namungo, wakati Simba wenyewe wa-takuwa Morogoro kuwavaa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri.

MTEGO UPO HAPA

Mzunguko wa 28 ndiyo utakuwa na kitendawili kigumu na Simba ikimalizana na Mtibwa Sugar, itarudi nyumbani kucheza dhidi ya Singida Black Stars wakati Yanga nayo itatakiwa kucheza nyumbani dhidi ya TRA United.

Yanga na Simba zote zinatumia uwanja wa KMC kama uwanja wao wa nyumbani na vinara hao wa ligi wameshamaliza matumizi yao ya kikanuni ya kuhamisha mechi mbili za nyumbani kwenda viwanja vin-gine na ilizipeleka Simba na Azam pale Amaan, Zanzibar.

Yanga hana namna lazima atumie uwanja wa KMC kucheza mechi yake dhidi ya TRA United wakati Simba ambayo imebakiza mechi moja kuhamisha inaweza kuchagua uwanja mwingine kucheza dhidi ya Singida BS.

Simba kama itahama kuna viwanja viwili itaweza kuvitumia hapa jijini Dar es Salaam, Meja Jenerali  Isamuhyo au ikimbilie Azam Complex, Chamazi ambako wekundu hao hawapataki wakiona kama ha-wana bahati na uwanja huo.

Wenyeji wa Uwanja wa Meja Isamuhyo JKT Tanzania Juni 27 itakuwa ugenini ikiwafuata Pamba jiji, pia Azam FC itawafuata Coastal Union pale CCM Mkwakwani, Tanga na kuacha viwanja vyao vikiwa wazi.

Mzunguko wa mwisho hautakuwa na shida kwani Yanga itawafuata JKT Tanzania pale Meja Isamuhyo wakati Simba ikisalia KMC Complex, itakapokuwa mwenyeji wa wamiliki wa uwanja huo KMC itaka-yokuwa inacheza mechi yao ya mwisho ya ligi kabla ya kushuka Championship.

KULE CHINI YA MSIMAMO

Ukiacha mbio hizo za ushindani wa kuusaka ubingwa, kuna kazi nyingine ipo chini ya msimamo na timu nane ambazo moja kati ya hizo inaweza kuungana na KMC kushuka daraja.

KMC tayari ina tiketi yake ya kucheza Championship msimu ujao, lakini kuanzia pale ilipo Mbeya City nafasi ya 15 hadi ilipo Dodoma Jiji katika nafasi ya nane zote zinaweza kushuka daraja endapo zita-poteza mechi zote tatu na wenzake kushinda mechi hizo.

Hali ni tofauti kuanzia timu ya saba Pamba Jiji wenyewe wapo salama bila ya kujalisha matokea ya wengine walio chini yake huku vita yao ikiwa ni kusaka kumaliza katika tano bora.

HAWA HAPA TPLB

Kaimu Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB) Tanzania, Issa Abushehe amekiri uwepo wa uamuzi huo ni kutaka kuona ushindani sawa kwa kila timu wakati msimu ukielekea mwisho na kuondoa wasiwasi wa kupanga matokeo.

“Ni kweli huo uamuzi umefanyika, tumesalia na mizunguko mitatu kumaliza msimu na ushindani umekuwa mkubwa, tunazipongeza timu zote namna zinavyoendelea kushindana lakini tunataka kuweka usawa katika ushindani huu,” alisema Abushehe.

“Kila mchezo utachezwa muda mmoja na kila timu itatumia uwanja wake, tunataka kila timu icheze mechi zake kwa hesabu zake na sio kuangalia moja imepata matokeo yapi na yenyewe ifanye nini ili tumalize msimu kwa haki ya kila klabu.

Abushehe akizungumzia hatua ya mzunguko wa 29 na Simba na Yanga zitagongana kwa mechi ya nyumbani, Abushehe alisema hilo litapangiwa na bodi kwa kutangulia kuzungumza na klabu husika ili moja ikatumie uwanja tofauti.

“Ni kweli Yanga itakuwa nyumbani na Simba itakuwa nyumbani mzunguko wa 29, sasa kwa hatua hiyo bodi itawasiliana na hizo klabu mbili na kuangalia ipi itatakiwa kutumia uwanja mwingine ili kila mechi ichezwe siku hiyo hiyo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *