Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8
Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine amezungumzia uwezekano wa Syria kuwa na jukumu la kukabiliana na Hezbollah nchini Lebanon, na kutangaza kuwa amezungumza na Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa kuhusu hili na yuko mbioni kukabidhi faili la Hezbollah kwa Syria.
Bw. Trump alisema hayo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa G7 nchini Ufaransa kwamba alizungumza na Ahmed al- Sharaa kuhusu Hezbollah, siku moja baada ya kuwaambia waandishi wa habari kwamba Syria inaweza kufanya kazi “bora” kuliko Israel katika kukabiliana na kundi hilo la Lebanon.
Hii sio mara ya kwanza kwa Donald Trump kuibua uwezekano wa Syria kukabiliana na kundi la Hezbollah nchini Lebanon. Suala hilo ni nyeti sana nchini Lebanon, kwani uwepo wa jeshi la Syria nchini humo ulianza mnamo 1976, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vilimalizika kwa kuondoka kwa vikosi vya Syria nchini humo mnamo 2005.
Jambo muhimu katika matamshi ya hivi majuzi ya Bwana Trump ni kwamba, katika kujibu swali la mwandishi wa habari, alisisitiza kwamba kuzungumza na Ahmed al-Sharaa kuhusu Hezbullah, bila kufichua maelezo zaidi kuhusu muda wa mazungumzo au maudhui ya jibu la rais wa Syria.
Ahmed Sharaa amekataa uingiliaji wowote wa kijeshi katika mzozo huo, akisema, “Jambo muhimu zaidi ya yote, ni kusitisha vita.”
Serikali ya Lebanon haijatoa tamko lolote kujibu kauli ya Trump. BBC Idhaa ya Kiarabu iliwasiliana na ofisi ya habari ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon ili kupata maoni ya Waziri wa Mambo ya Nje Youssef Raghi kuhusu matamshi ya Bw. Trump, na jibu lilikuwa: “Hatuna maoni yoyote.”
Nchini Israel, Waziri wa Ulinzi Yisrael Katz, akijibu matamshi ya Bw. Trump, alisema nchi yake “haihitaji” msaada wa Rais wa Syria Ahmed Sharia nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa Channel 14 ya Israel, Bw. Katz, katika mahojiano na mtandao huo, alimtaja Bw. Sharaa kwa jina lake la zamani, “Jolani,” na kumtaja kuwa “gaidi aliyevalia suti.” Aliongeza kuwa Israel “inafanya kazi yenyewe,” akimaanisha operesheni zake za kijeshi dhidi ya Hezbollah.
Chanzo cha picha, Getty Images
Trump alisema nini hasa?
Rais wa Marekani Donald Trump amezungumza kwa kauli mbili tofauti kuhusu uwezekano wa Syria kujiunga na harakati za kukabiliana na Hezbollah nchini Lebanon.
Alitoa kauli ya kwanza kuhusiana na suala hilo mnamo Juni 16 mwaka huu, wakati wa mkutano wake na Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Amiri wa Qatar, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa G7 nchini Ufaransa.
Bw. Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba alipendekezaa Israel “waiachie Syria kundi la Hezbollah,” na kuongeza: “Kusema kweli, nadhani wanaweza kufanya vyema zaidi.”
Matamshi ya Bwana Trump yalitolewa akijibu swali kuhusu mashambulizi ya Israel nchini Lebanon na athari zake katika mchakato wa kidiplomasia wa kumaliza mzozo wa Iran.
Bw. Trump alimsifu Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa, akisema mtu “anayeiongoza Syria sasa,” akishirikiana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na wengine, wamefanya kazi “ya kushangaza” ya kuunganisha nchi hiyo. Aliongeza kuwa Ahmed al-Sharaa “si malaika,” lakini amefanya “kazi kubwa” nchini Syria, amefanya kazi nzuri kukabiliana na Hezbollah, na, kwa maneno ya Bw. Trump, “hakuwapenda.”
Kisha Bw Trump alikosoa jinsi Israel inavyoshughulikia Hezbollah nchini Lebanon, akisema kuwa Israel imekuwa ikipambana na kundi hilo kwa muda mrefu na kwamba “watu wengi wanauawa.” Aliongeza kuwa “sio lazima kuharibu jengo la makazi kila wakati” wanatafuta mtu, kwa sababu kuna watu wengi wanaoishi katika majengo hayo, “sio wote ni wanachama wa Hezbollah,” alisema.
Siku moja baadaye, shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa Donald Trump alikuwa amemthibitishia mwandishi kwamba kweli alikuwa amezungumza na Ahmed al- Sharaa kuhusu Hezbollah. Alipoulizwa ikiwa rais wa Syria yuko tayari kukabiliana na kundi hilo, Bw.Trump alisema atalizungumzia suala hilo baadaye.
Ni vyema kutambua kwamba Trump hakutaja jukumu lolote la maafisa wa Lebanon katika matamshi yake, wala hakutaja kuwafahamisha au kushauriana na maafisa wa Lebanon kuhusu uwezekano wowote wa Syria nchini Lebanon.
Rais wa Lebanon Joseph Aoun hapo awali, katika taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Kiarabu, alisema haoni sababu ya rais wa Syria kuingilia masuala ya la Lebanon, akisema kwamba Ahmed Sharaa ana “msimamo thabiti wa uwajibikaji na mwamko wa kisiasa” na kwamba hatakubali hatavutwa kwenye “mzozo wa Lebanon.”
Syria imesema nini
Mnamo Juni 13, watu kadhaa wanaosadikiwa kuwa watu mashuhuri kutoka viungani mwa jiji la Damascus walikutana katika Ikulu ya Syria lakini Rais Ahmed al-Sharaa alikanusha kile alichoelezea kama “uvumi” kuhusu uingiliaji wa Syria nchini Lebanon.
Bwana Sharaa alisema: “Kinachosemwa kuhusu Syria kuingia Lebanon si kweli. Tunachopendekeza kila mara ni kusitishwa kwa vita, kuimarisha taasisi za serikali, kuboresha uhusiano wa kiuchumi, na kutuliza hali ya Lebanon kadiri inavyowezekana.”
Kuhusu uhusiano wa Lebanon na Syria, Bw. Sharaa alisema kuwa mahusiano hayo yalijengwa katika “misingi ya uwongo” wakati wa utawala uliopita. Aliashiria kuwepo kwa “jeraha la Lebanon” lililotokana na kuingiliwa na Syria huko Lebanon na “jeraha la Syria” lililotokana na uingiliaji wa Hezbollah nchini Syria.
Maoni ya Bw. Sharia yalikuja siku chache baada ya Bw. Trump, katika mahojiano na NBC, kutaja uwezekano wa msaada wa Syria katika kukabiliana na Hezbollah nchini Lebanon.
Katika muktadha huu, shirika la redio na televisheni la Israel “Kan 11”, likinukuu chanzo cha Syria ambacho hakikutajwa jina, kiliripoti kwamba Damascus inaona uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi dhidi ya Hezbollah ni jambo lisilowezekana, kwani ulimwengu wa Kiarabu unaweza kufikiria hatua kama hiyo kutumikia masilahi ya Israeli.
Shirika hilo pia limeripoti, likinukuu chanzo hicho hicho, kwamba Uturuki imetuma ujumbe kwa maafisa wa Syria ikiwataka kujiepusha na makabiliano ya moja kwa moja na Hezbollah, kwa kuhofia kwamba makabiliano hayo yataimarisha nafasi ya kimkakati ya Israel katika eneo hilo.
Chanzo cha picha, Getty Images
Nusu karne baada ya kuingia kwa majeshi ya Syria nchini Lebanon
Uingiliaji wa kijeshi wa moja kwa moja wa Syria nchini Lebanon ulianza mwishoni mwa Mei 1976, mwaka mmoja baada ya kuanza kwa Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon, mapigano kati yaLebanese National Movement na Lebanese Front kuongezeka. Lebanese National Movement ilikuwa muungano wa vikosi vya mrengo wa kushoto, vya kitaifa, na vya Kiislamu vinavyoungwa mkono na makundi ya Kipalestina yenye silaha. Lebanese Front ilikuwa muungano wa vyama na vikosi vya Wakristo vya mrengo wa kulia, vikiwemo Chama cha Kata’ib na Chama cha Free Nationalist.
Chini ya Rais wa zamani Hafez al-Assad, Syria ilihalalisha uingiliaji kati wake kwa lengo la kusimamisha vita, kuzuia kuporomoka kwa Lebanon, na kudhibiti kuenea kwa mgogoro huo. Lakini pia ilifuata wito wa kuungwa mkono na vikosi vya Wakristo wa Lebanon, ambao wakati huo walikuwa chini ya shinikizo kubwa la kijeshi kutoka kwa wapinzani wao.
Hapo awali, uingiliaji kati wa Syria ulivishindanisha vilivyo vikosi vyake dhidi ya vikundi vya Wapalestina na vikosi vyenye mfungamano na Harakati ya Kitaifa ya Lebanon. Hii ilikuwa licha ya ukweli kwamba Damascus hapo awali iliunga mkono baadhi ya vyama vingine vya Palestina na Lebanon au kujaribu kushawishi mchakato wa makubaliano. Baada ya hapo, miungano ya Syria ndani ya Lebanon ilibadilika mara nyingi, kutegemea uwiano wa mamlaka na siasa za Damascus za kikanda na za ndani.
Mnamo Oktoba 1976, uwepo wa jeshi la Syria ulipata mfumo wa Waarabu kwa kuunda “Vikosi vya Kuzuia Waarabu” kwa uamuzi wa Jumuiya ya Waarabu, lakini vikosi hivi kwa vitendo vilikuwa vya Syria.
Uwepo wa kijeshi na usalama wa Syria nchini Lebanon uliendelea hadi 2005. Mwaka huo, Damascus iliondoa vikosi vyake kutoka nchini humo kufuatia mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri, chini ya shinikizo la maandamano yaliyoenea nchini Lebanon na Azimio 1559 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aprili 26, 2005, Syria iliiarifu Umoja wa Mataifa, huduma za kijasusi za Syria, na vifaa vyake vya upelelezi kutoka Lebanon.
Hezbollah nchini Lebanon
Baada ya maandamano dhidi ya serikali ya Bashar al-Assad nchini Syria kuanza mwaka 2011 na hatua kwa hatua kugeuka kuwa mgogoro wa silaha, Hezbollah iliingilia kijeshi kuunga mkono vikosi vya serikali ya Syria dhidi ya makundi ya upinzani yenye silaha na mashirika ya kijihadi.
Chama hicho kilipigana pamoja na wanajeshi wa Syria katika maeneo mengi, kutoka viunga vya Homs na Qusayr karibu na mpaka wa Lebanon hadi Aleppo, viunga vya Damascus na maeneo mengine. Hezbollah hatua kwa hatua ilitangaza uwepo wake nchini Syria hadharani, kwanza ikizungumza juu ya kulinda maeneo ya kidini ya Shiite na vijiji vya mpakani, kisha kuweka mpaka wa Lebanon, na hatimaye kutangaza ushiriki wake wa wazi katika mapigano ndani ya Syria. Chama kilipoteza idadi kubwa ya wanajeshi na makamanda wake wakati wa vita hivyo.
Baadaye, Hezbollah ilipambana na watu wenye silaha wa Syria kwenye mpaka wa Lebanon na Syria, hasa katika miinuko ya Arsal na Qalamoun.
Mnamo mwaka wa 2017, jeshi la Lebanon likiongozwa na Jenerali Joseph Aoun, lilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la Islamic State katika maeneo ya Ras Baalbek na Al-Qa’a. Wakati huo huo, Hezbollah na jeshi la Syria pia walikuwa wakiendesha operesheni katika upande wa mpaka wa Syria na katika maeneo mengine ya mpaka. Jeshi la Lebanon lilisisitiza wakati huo kwamba halikuwa likiratibu operesheni zake na Hizbullah au jeshi la Syria.
Kwa kuanguka kwa utawala wa Assad mnamo Desemba 2024, Hezbollah ilipoteza mshirika wake wa Syria na moja ya njia kuu za usambazaji kupitia Syria, na kupata pigo la kimkakati.
Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa vikosi vya Hezbollah na makamanda walikuwa wameondoka Syria kufikia Oktoba 2024 ili kuzingatia vita na Israel huko Lebanon. Wakati makundi ya upinzani yakisonga mbele kuelekea Damascus, chama kilituma maafisa kusimamia uondoaji wa vikosi vyake vilivyosalia huko.
Kwa nini hali kati ya Lebanon na Syria inaonekana kuwa ngumu zaidi?
Andrew J. Tabler, mtafiti katika Taasisi ya masomo ya Washington Near East, alionya kwamba kuhimiza Syria kuingilia kijeshi nchini Lebanon kunaweza kusababisha tishio kubwa kwa Damascus na Washington.
Bwana Tabler anaamini kwamba serikali ambayo bado inajaribu kuimarisha udhibiti wake ndani ya Syria haiko katika kujiingiza kwenye vita nje ya mipaka yake.
Mtafiti aliashiria baadhi ya mambo ambayo yangefanya uingiliaji kati wa Syria nchini Lebanon kuwa hatari kubwa. Kulingana na yeye, hatua kama hiyo inaweza, kwanza kabisa, kusababisha kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo na kuleta pamoja mitandao ya makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria, Iraqi na kwingineko.
Pili, uingiliaji wowote wa kijeshi wa Syria, Bw. Tabler alisema, unaweza kuchochea mivutano ya kidini nchini Lebanon na kanda. Aliandika kwamba Hezbollah itajaribu kuonyesha vikosi vya Syria kama “wanajihadi wa Kisunni,” wakiwemo wapiganaji wa Syria, Uzbek na Uyghur na kulenga jamii za Shiite. Hadithi kama hiyo inaweza kuimarisha mshikamano na Hezbollah katika msingi wake wa msingi.
Tatu, Bw. Tabler anaamini kwamba uwepo wowote mpya wa kijeshi wa Syria unaweza kudhoofisha uhalali wa serikali ya Lebanon. Alitabiri kwamba wengi nchini Lebanon, kwa kuzingatia miongo kadhaa ya uwepo wa jeshi na usalama wa Syria chini ya Assad, wangeona uwepo kama huo kama uungaji mkono wa uhuru wa Lebanon lakini kama aina fulani ya shinikizo la kigeni.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi