
Bao la dakika ya 76 lililofungwa na beki Daniel Munos limetosha kuamua mchezo huo ambao Colombia iliutawala na kutengeneza nafasi nyingi.
Kwenye mchezo huo Colombia ilikaribia kupata ushindi mzuri, lakini mabao matatu yamekataliwa, mawili yakifungwa na Munos na moja lilikuwa la Luis Dias lakini yalinaswa kwenye mtego wa kuotea, na lingine kucheza madhambi dhidi ya mchezaji wa DR Congo kabla ya kufungwa.
Kipa wa DR Congo, Lionel Mpasi, amefanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi makali ya Colombia akizima manane ya wazi.
DR Congo imepata mashuti mawili yaliyolenga lango kwenye dakika ya 90 kupitia mshambuliaji Nathanael Mbuku na pia kichwa alichopiga beki na nahodha wa timu hiyo, Chancel Mbemba, dakika ya 90+2.
Ushindi huo unaifanya Colombia kuongoza kundi K ikifikisha pointi sita ikishinda mechi mbili, Ureno ikiwa ya pili na pointi nne huku DR Congo ikiwa nafasi ya tatu na pointi moja wakati Uzbekistan iko mkiani bila alama yoyote.
DR Congo bado ina nafasi ya kufuzu endapo itashinda mchezo wa mwisho dhidi ya Uzbekistan ambayo haijapata pointi yoyote, lakini italazimika kufunga mabao zaidi ya sita na kuiombea Ureno kupoteza mchezo wa mwisho dhidi ya Colombia na pia bila kufunga bao.