DAR ES SALAAM: MASHINDANO ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF 2026) awamu ya nane yanatarajiwa kuanza Julai 6, mwaka huu. Mechi ya ufunguzi iitachezwa uwanja wa Azam complex,Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Michuano hiyo, Brigedia Jenerali Saidi Hamisi Saidi ameeleza hayo kwenye viwanja vya Gofu vya Lugalo Dar es Salaam.

Amesema kauli mbiu ya mashindano hayo ni “Amani, Umoja na Mshikamano kwa Ujenzi wa Taifa Letu”, ambayo inaakisi dhamira ya JWTZ kutumia michezo kama nyenzo ya kujenga mahusiano, uzalendo na ushirikiano miongoni mwa wanajeshi na wananchi.

Ameeleza dhumuni la mashindano hayo ni kuimarisha utimamu wa mwili na afya ya akili kwa maafisa na wapiganaji, kujenga ujasiri, ukakamavu na kujiamini, pamoja na kubaini na kukuza vipaji vya wanamichezo ndani ya jeshi.

Amesema kuwa mashindano hayo yatahusisha timu kutoka katika makamandi mbalimbali ya JWTZ ikiwemo Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Anga, Jeshi la Wanamaji, Makao Makuu ya Jeshi, Jeshi la Akiba na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Brigedia Jenerali Hamis amesema jumla ya michezo 13 itashindaniwa katika mashindano hayo ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, riadha, kulenga shabaha, kuogelea, kupita kwenye vikwazo, darts, soka la ufukweni na michezo mingine, huku mchezo mpya wa pool table ukiwa umeongezwa mwaka huu.

Amesema kuwa mchezo wa ngumi utakuwa na upekee katika CDF Cup ya mwaka huu ambapo mabondia kutoka makamandi mbalimbali watashindania mikanda maalum ya CDF Cup kwa uzito tofauti kwa wanaume na wanawake, ikiwa ni sehemu ya kutambua vipaji vya wanajeshi katika mchezo huo.

Aidha amesema wananchi watapata fursa ya kushuhudia mashindano hayo bila kiingilio katika viwanja mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Azam Complex Chamazi ambako kutafanyika ufunguzi na ufungaji wa mashindano hayo, pamoja na viwanja vya kambi mbalimbali za jeshi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *