
Dar es Salaam. Bingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu, atapatikana katika raundi ya mwisho, Jumanne, Juni 30, 2026 baada ya Yanga na Simba kila moja kupata ushindi katika mechi yake leo.
Matokeo hayo yameifanya Yanga iendelee kuongoza msimamo wa Ligi ikifikisha pointi 72 huku Simba ikifikisha pointi 70 na kuendelea kubaki katika nafasi ya pili.
Kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, wenyeji Yanga wameibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United, yote yakipachikwa na Allan Okello.
Mabao hayo yamemfanya Okello afikishe idadi ya mabao 14 moja pungufu dhidi ya Feisal Salum ambaye yuko kileleni mwa chati ya kuwania Ufungaji Bora wa msimu.
Pia Okello anakuwa mchezaji wa nne kufunga mabao matatu (hat-trick) katika mechi moja, wengine wakiwa ni Mossi Nduwumwe (Singida BS), Mathew Tegis (Pamba Jiji) na Fabrice Ngoy (Namungo FC).
Simba imetumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars.
Mabao ya Simba katika mchezo wa leo yamefungwa na Elie Mpanzu na Anicet Oura.
Katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amejitengenezea mazingira mazuri ya kuibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu huu baada ya kupachika bao katika ushindi wa mabao 2-0 ambao Azam FC iliupata dhidi ya wenyeji Coastal Union, ambapo bao lingine lilifungwa na Landry Zouzou.
Fei Toto anaendelea kuongoza orodha ya wafungaji bora wa ligi akifuatiwa na Okello na Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars wakiwa na mabao 14.
Matokeo ya mechi za leo
Yanga 3-0 TRA United
Simba 2-0 Singida BS
Coastal 0-2 Azam FC
Namungo 0-0 Fountain Gate
Dodoma Jiji 1-1 Mbeya City
Pamba Jiji 1-2 JKT Tanzania
Mashujaa FC 2-0 KMC
Tanzania Prisons 2-1 Mtibwa Sugar