
UNICEF, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, limesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa Jumamosi mji mkuu wa Venezuela, Caracas.
Matetemeko mawili ya ardhi yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Ritcher, yalirekodiwa kwa tofauti ya dakika moja tu tarehe 24 Juni, ikiwa ni tukio kubwa zaidi la mtetemeko wa ardhi kuikumba Venezuela katika kipindi cha zaidi ya karne moja.
UNICEF inasema uchambuzi wa awali wa picha za satelaiti umeonesha kuwa karibu theluthi moja ya majengo katika moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi yaliyotathminiwa hadi sasa, Catia La Mar, katika jimbo la La Guaira kaskazini mwa Caracas, yameharibika.
Mahitaji yaanza kudhihirika
“Baada ya siku tatu za mwitikio wa dharura, ukubwa wa mahitaji unaanza kuwa wazi zaidi,” amesema Manuel Rodríguez Pumarol, Mwakilishi wa UNICEF nchini Venezuela.
Amesema, “hospitali zinafanya kazi zaidi ya uwezo wake, maelfu ya watoto hawana upatikanaji wa uhakika wa maji safi, na shule nyingi zimeharibika. UNICEF inashirikiana na Serikali ya Venezuela pamoja na washirika wake kuongeza msaada kwa watoto na familia zao, na ufadhili endelevu utakuwa muhimu ili kuendeleza mwitikio huu katika wiki zijazo.”
Hospitali zimeharibiwa
Hospitali kwenye mji mkuu Caracas na majimbo ya La Guaira, Carabobo, Aragua na Falcón zimepata uharibifu mkubwa, hali iliyozifanya baadhi ya taasisi hizo kufikia kiwango cha dharura na kuathiri vibaya utoaji wa huduma kwa watoto na wanawake wajawazito.
Katika wilaya ya mji mkuu pekee, taarifa za awali zinaonesha kuwa shule 432—zaidi ya theluthi moja ya shule zote za wilaya hiyo—zimeharibika, jambo linalowafanya watoto kushindwa kuendelea na masomo yao.
Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka baada ya tathmini katika majimbo mengine kukamilika. Mamlaka zinaandaa shule ambazo hazikuathirika kutumika kama makazi ya muda kwa familia zilizohamishwa.
Mwitikio mpana zaidi wa dharura
Kwa kushirikiana na Serikali ya Venezuela, mfumo wa Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa kibinadamu, UNICEF imeanzisha mwitikio uliopanuliwa wa dharura kwa kupeleka wafanyakazi wa ziada na kusambaza vifaa vya msaada ili kuwafikia takriban watu 650,000, wakiwemo watoto 234,000, kwa huduma za afya, lishe, maji na usafi wa mazingira, ulinzi wa watoto na elimu.
Ndege ya kwanza ya UNICEF iliyobeba tani 20 za vifaa vya matibabu pamoja na vifaa vya maji na usafi wa mazingira iliwasili Valencia nchini Hispania, tarehe 27 Juni ikitokea katika ghala la kikanda la UNICEF nchini Panama.
Shehena ya pili kutoka kituo cha kimataifa cha usambazaji cha UNICEF kilichopo Copenhagen, Denmark, imepangwa kuwasili katika siku zijazo. Kwa pamoja, shehena hizo mbili zitahudumia zaidi ya watu 100,000.
Fedha zinazohitaijka na UNICEF ni dola milioni 52
UNICEF inakadiria kuwa dola za Marekani milioni 52 zinahitajika kukabiliana na dharura hii ya matetemeko ya ardhi, ikiwa ni sehemu ya ombi lake pana la Ombi la Dharura la Usaidizi kwa watoto la mwaka 2026 kwa Venezuela lenye thamani ya jumla ya dola za Marekani milioni 137.6.
UNICEF tayari imehamasisha takriban dola za Marekani milioni 3.5 kutoka katika mfuko wake wa ndani wa dharura ili kuwezesha kupelekwa kwa awali kwa wafanyakazi na vifaa vya msaada, na sasa inatoa wito kwa wafadhili kuongeza ufadhili wa ziada na unaobadilika kulingana na mahitaji ili kudumisha na kupanua mwitikio huu.