Mashine inaanza kunguruma majira ya saa tatu asubuhi.

Ndani ya banda la bati sokoni pembezoni mwa Barabara ya Dodoma–Morogoro, gunia la mahindi linapasuliwa kwa kisu na kumwagwa taratibu ndani ya kinu. Dakika chache baadaye, upande mmoja unatoka unga mweupe unaopeperusha vumbi jembamba, huku upande mwingine ukitiririka mkondo wa pumba za rangi ya dhahabu.

Hakuna anayezifagia. Hakuna anayezitupa.

Vijana wawili wanazikusanya kwa kutumia sepetu na kuzimwaga juu ya maturubai yaliyotandazwa ardhini. Pembeni, magunia yaliyokwisha kujazwa yamepangwa mstari mmoja yakisubiri kupakiwa kwenye pikipiki na malori madogo yanayoondoka kuelekea maeneo mbalimbali ya nchi.

Mita chache kutoka hapo, wanawake kadhaa wameketi wakiwa wamejifunga na kijifunika nguo kichwani huku nyuso zao kikiwa zimesakafiwa kwa vumbi wakipepeta pumba za mpunga. Kwa kila ungo wanaoutikisa, chembe ndogo za mchele hujitenga na pumba. Hazitupwi. Hukusanywa kwenye ndoo ndogo na kupelekwa majumbani kupika vitumbua, uji na vyakula vingine. Kilichobaki huingia kwenye magunia mengine, safari hii kikielekea kwa wafugaji.

Ni taswira ambayo miaka michache iliyopita isingeaminika.

Kulikuwa na wakati ambapo nyuma ya mashine nyingi za kusaga nafaka hasa vijijini kulijaa milima ya pumba. Wakati mwingine watoto waliitumia kuchezea au kuikanyaga wakipita. Haikuwa bidhaa; ilikuwa mabaki yasiyo na thamani yoyote.

Leo, mlima huo haupo. Kila kilo ina mnunuzi. Kila gunia lina bei.

“Bei hubadilika kulingana na msimu, lakini siku hizi pumba hazikai. Wafugaji wanazifuata wenyewe,” anasema Meshaki Juma, mfanyabiashara wa pumba za mahindi, mpunga na mashudu ya alizeti jijini Dodoma. Anasema wakati wa mavuno gunia la ujazo wa debe sita linaweza kuuzwa kwa takribani Sh45,000, huku mahitaji yakiongezeka kadiri shughuli za ufugaji zinavyopanuka.

Kauli yake inaeleza mabadiliko makubwa yanayotokea kimya kimya katika uchumi wa Tanzania.

Akiwa katikati ya miungurumo ya mashine za kusaga na vumbi jembamba la pumba linalotanda hewani, Meshaki anaketi kimya kwenye benchi la mbao nje ya ghala lake. Amevalia sweta la kahawia lililotapakaa vumbi la mahindi na suruali ya jeans nyeusi, huku nyuma yake magunia yaliyojaa pumba za mahindi, mpunga na mashudu ya alizeti yakipangwa kutoka sakafuni hadi ukutani, yakisubiri kupakiwa kwenye malori.

Anatazama vijana wawili wakifunga gunia jingine kwa kamba kabla ya kulipakia. Kisha anatabasamu kidogo na kusema: “Zamani tulikuwa tunafagia pumba na kuzitupa nyuma ya mashine. Leo tunazifungia kwenye magunia, kwa sababu kila kilo ina mnunuzi.”

Kwa muda mrefu mafanikio ya kilimo yalipimwa kwa idadi ya magunia yaliyovunwa. Leo, kipimo hicho kinabadilika. Gunia la mahindi halizalishi unga pekee; linazalisha pumba, biashara ya usafirishaji, ajira kwa vijana wanaobeba na kufungasha magunia, na malighafi inayotumika kutengeneza chakula cha mifugo.

Kwa maneno mengine, thamani ya zao haimaliziki linapoondoka shambani. Hapo ndipo safari yake mpya inaanza.

Takwimu zinaonesha kwa nini mabadiliko hayo yanaonekana kwa kasi. Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, Tanzania ilizalisha zaidi ya tani milioni 23.78 za mazao ya chakula mwaka 2024/25, kiwango kilichowezesha nchi kufikia zaidi ya asilimia 130 ya kujitosheleza kwa chakula. Serikali pia iliongeza uwezo wa Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), ambayo sasa ina uwezo wa kuhifadhi takribani tani 776,000 za nafaka ili kuimarisha usalama wa chakula na uthabiti wa soko.

Lakini takwimu hizo zinaeleza nusu tu ya kilichopo. Hadithi nyingine inaanzia pale gunia linapoingia kwenye mashine ya kusaga.

Katika Bajeti ya mwaka 2026/27, Serikali imeweka mkazo kwenye kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao kwa kuwekeza katika masoko ya kisasa, maghala, uchakataji na kuongeza thamani ya mazao, badala ya kuishia kuongeza uzalishaji pekee.

Kwa mchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Esther Kokunywanisa Ishengoma, mafanikio ya sekta ya kilimo hayawezi tena kupimwa kwa mavuno pekee.

“Uchumi wa mkulima unaongezeka pale ambapo zao linaendelea kuzalisha thamani baada ya mavuno kupitia usindikaji, masoko na biashara zinazolizunguka,” anasema.

Anachokieleza Profesa Ishengoma ndicho kinachoonekana kwenye eneo hili la kusaga nafaka.

Mashine hazizalishi unga pekee. Zinazalisha uchumi. Prof Esther anadai: “Gunia la mahindi halipaswi kuishia sokoni. Linapaswa kuendelea kuzalisha uchumi.”

Na ushahidi unaonekana hata kwenye sekta ya viwanda. Kwa mujibu wa Ripoti mpya ya Daftari la Takwimu za Biashara Tanzania 2023/24 lililochapishwa Septemba 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kati ya viwanda 17,463 vya uzalishaji vilivyosajiliwa nchini, asilimia 38.4 ni viwanda vya usindikaji wa bidhaa za chakula—idadi kubwa kuliko sekta nyingine yoyote ya uzalishaji. Hii inamaana kati ya viwanda vyote vya Tanzania, karibu viwanda vinne kati ya kilaviwanda  kumi vinahusika na usindikaji wa chakula. Sekta hiyo pia ndiyo mwajiri mkubwa zaidi, ikitoa zaidi ya asilimia 32 ya ajira zote katika viwanda.

Kwa lugha rahisi, kila gunia linaloingia kwenye mashine kama hii linaweza kuwa mwanzo wa mlolongo mrefu wa shughuli za kiuchumi unaounganisha mkulima, msagaji, mfanyabiashara wa pumba, mfugaji, kiwanda na mlaji.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka lengo la kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha minyororo ya thamani ya ndani kuwa miongoni mwa nguzo za kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani. Vivyo hivyo, Ripoti ya Uwekezaji ya Tanzania 2025 inaonesha kuwa sekta ya uzalishaji imeendelea kuwa miongoni mwa sekta zinazoongoza kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, ishara kwamba thamani ya mazao ya kilimo haitatafutwa shambani pekee, bali pia viwandani.

Lakini kwa Meshaki, uchumi huo mkubwa unaanza kwa picha rahisi sana.

Gunia moja la pumba likiondoka ghalani. Gunia hilo halisafiri kwa bahati.

Baada ya kuondoka kwenye ghala la Meshaki, baadhi ya pumba husafirishwa kwenda kwa wafugaji wa kuku na ng’ombe katika mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Manyara na Arusha. Mengine hupelekwa kwenye viwanda vidogo vya kutengeneza chakula cha mifugo, ambako huchanganywa na mashudu ya alizeti, pamba, madini lishe na malighafi nyingine kabla ya kurudi tena mashambani, safari hii kama chakula kinachoongeza uzalishaji wa nyama, maziwa na mayai.

Ni mzunguko ambao hauonekani kwa macho ya wengi, lakini ndiyo unaoifanya thamani ya zao kuendelea kukua hata baada ya kuvunwa.

Kwa miaka mingi, kilimo na mifugo vilionekana kama sekta mbili tofauti. Leo, gunia la pumba linaonesha jinsi sekta hizo zinavyotegemeana. Bila mahindi hakuna pumba; bila pumba, gharama za uzalishaji wa chakula cha mifugo hupanda; na bila chakula bora cha mifugo, uzalishaji wa nyama, maziwa na mayai hupungua.

Katika Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2026/27, kipaumbele kimewekwa katika kuongeza uzalishaji wa mifugo, kuboresha upatikanaji wa malisho na chakula cha mifugo, kuimarisha usindikaji wa bidhaa za mifugo na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa uzalishaji. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dk. Bashiru Kakurwa anasema zaidi ya robo tatu ya bajeti ya wizara imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, ishara kwamba sekta hiyo sasa inaonekana kama sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Kwa Profesa Esther Ishengoma, huu ndiyo mwelekeo unaoweza kuongeza kipato cha mkulima bila kuongeza ukubwa wa shamba.

“Kilimo hakiwezi tena kuangaliwa kama shughuli ya kuzalisha mazao pekee. Thamani halisi inapatikana pale ambapo zao linaendelea kuzalisha biashara, ajira na uwekezaji katika kila hatua ya mnyororo wa thamani,” anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mwenendo wa uchumi wa Tanzania. Lakini thamani ya pumba haionekani kwenye maghala ya Dodoma pekee. Inaonekana pia kwenye masoko yanayoendelea kujengwa ili kuunganisha wakulima na wanunuzi.

Mei mwaka huu, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba alizindua Soko la Mazao la Kibakwe wilayani Mpwapwa, Dodoma, akisema maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kutenganishwa na uwekezaji katika masoko, miundombinu na biashara ya mazao.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mhandisi Athuman Kilundumya, alisema soko hilo ni sehemu ya miradi inayotekelezwa kupitia Programu ya Tanzania Food Systems Resilience Program (TFSRP), inayolenga kuboresha masoko, uhifadhi na usafirishaji wa mazao. Soko hilo, lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 603, linatarajiwa kuhudumia wakulima na wafanyabiashara kati ya 300 na 350 kwa wakati mmoja, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake pamoja na kupanua fursa za biashara za mazao.

Kwa Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, hatua hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya sekta ya kilimo isibaki kwenye uzalishaji pekee bali iwe chanzo cha biashara, viwanda na ajira kupitia kuongeza thamani ya mazao.

Mabadiliko hayo yanaonekana hata kwenye maeneo ambayo watu wengi hawayaangalii.

Kando ya mashine za kusaga, wanawake wanaendelea kupepeta pumba za mpunga kutafuta chembe za mchele ambazo huzipeleka nyumbani kupika vitumbua na uji. Kilichobaki hakiendi dampo; hujazwa kwenye magunia na kuuzwa kwa wafugaji wa kuku, ng’ombe na nguruwe. Kwao, hakuna kinachopotea.

Kwa upande mwingine, wafugaji wanaendelea kutafuta pumba hizo kila msimu. Kadiri gharama za uzalishaji wa chakula cha mifugo zinavyoongezeka, ndivyo thamani ya pumba inavyozidi kupanda. Gunia lililokuwa likionekana kuwa mabaki sasa limekuwa bidhaa inayounganisha mkulima, msagaji, mfanyabiashara, mfugaji na msindikaji wa chakula cha mifugo.

Hata Meshaki anasema ameona mabadiliko hayo kwa macho yake.

“Miaka ya nyuma pumba zilikuwa zinabaki hapa. Leo, wakati mwingine zinauzwa hata kabla hatujamaliza kuzifungasha. Wafugaji wanapiga simu kuuliza mzigo umefika au bado,” anasema.

Jioni inaanza kuingia.

Miungurumo ya mashine inapungua taratibu. Magunia yaliyokuwa yametapakaa juu ya maturubai sasa yamefungwa na kupangwa mlangoni. Lori dogo linaingia, vijana wawili waliinua gunia la mwisho na kulipakia.

Meshaki analifuatilia kwa macho hadi linapoondoka.

“Kesho tutaanza tena,” anasema kwa utulivu. Ndani ya gunia hilo hakuna pumba pekee. Kuna ajira za vijana waliolibeba. Kuna kipato cha mwanamke aliyepepeta mchele. Kuna chakula kitakachowafikia wafugaji. Kuna malighafi ya kiwanda.

Na kuna ushahidi kwamba leo mafanikio ya kilimo nchini Tanzania hayapimwi tena kwa mavuno pekee, bali kwa thamani ambayo mazao yanaendelea kuzalisha muda mrefu baada ya kuondoka shambani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *