KWA matokeo ya mechi za jana Jumamosi katika raundi ya 29 ya Ligi Kuu Bara, kuna baadhi ya timu hesabu zao hazijakaa sawa, hivyo wanasubiri Juni 30, 2026 siku ya kuhitimisha ligi hiyo msimu huu 2025-2026 kuamua hatma yao.
Katika hilo, kila upande unasema: “Tutajuana hukohuko siku ya mwisho.”
Hii si tu kwa wanaowania ubingwa, wala kupambana kuepuka kushuka daraja, bali hata kwa wachezaji katika mbio za ufungaji bora, lakini pia ishu ya asisti. Kwa upande wa clean sheet, Djigui Diarra wa Yanga amefunga mjadala baada ya kufikisha 17, kwa mechi zilizobaki, hakuna kipa mwingine atakayemzidi. Anafuatiwa na Mahamadou Kassali wa Simba mwenye 15.
Yanga na Simba mbio zao za ubingwa zinakwenda kuamuliwa siku ya mwisho kwani baada ya jana zote kushinda, zimeendelea kutofautiana pointi mbili, Yanga ikiwa na 72, Simba inazo 70.
OKELLO AKOLEZA PATI LA UBINGWA YANGA
Pati la ubingwa wa tano mfululizo wa Yanga katika Ligi Kuu Bara linazidi kunoga baada ya nyota wa timu hiyo, Allan Okello kufunga mabao matatu (Hat-Trick) katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Okello alianza kuipa Yanga furaha baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 27, likiwa ni bao lake la 12 katika Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Vipers SC ya kwao Uganda.
Okello alifunga bao hilo baada ya kutumia vyema pasi ya mshambuliaji Prince Dube na kuuzamisha mpi-ra wavuni uliomshinda kipa wa TRA United, Jean-Noel Amonome, huku mabeki wa kikosi hicho waki-dhani mfungaji huyo tayari alikuwa katika eneo la kuotea.
Katika mechi hiyo ilishuhudiwa Yanga ikitengeneza mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la TRA United, tofauti na wapinzani wao ambao muda mwingi walionekana kucheza kwa tahadhari kubwa ya kujilinda huku wakishambulia kwa kushtukiza zaidi.
Kipindi cha pili kikaendelea kwa Yanga kulishambulia lango la wapinzani wao ambapo dakika ya 51, Okello alifunga bao la pili na la 13 kwake kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa TRA United, Christo-pher Tebandeke kuunawa mpira katika eneo la hatari na mwamuzi, Saad Mrope kutoka Dodoma kuipa Yanga faida hiyo.
Wakati TRA United ikijipanga kwa ajili ya kusawazisha mabao hayo, Okello akazidi kupeleka kilio kwa timu hiyo baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 60, ikiwa ni hat-trick yake ya kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Hat-trick hiyo ya Okello inakuwa ya kwanza kwa Yanga msimu huu lakini ni ya nne kufungwa katika Ligi Kuu Bara, baada ya Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars, Mathew Momanyi wa Pamba Jiji na Fab-rice Ngoy wa Namungo kutangulia kufunga pia.
Mabao hayo matatu yanamfanya Okello kufikisha 14 ndani ya Ligi Kuu Bara na kukoleza vita mpya ya ufungaji bora akiwa sawa wa Mrundi wa Singida Black Stars, Mossi Ndumumwe, wakizidiwa na kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga 15 akiwa kileleni.
Huu unakuwa ni ushindi wa kwanza kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya TRA United, baada ya mechi ya kwanza kati ya miamba hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Machi 18, 2026, kutoka suluhu ya (0-0).
Ushindi huo ni muhimu zaidi kwa Yanga inayosaka taji la tano mfululizo la Ligi Kuu Bara, kutokana na upinzani mkali unaoendelea kati yao na watani zao wa jadi Simba ambayo ndio mshindani aliyebakia kwa kikosi hicho cha mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, mechi za mwisho wa msimu wa 2025-2026, zitakazopigwa Jumanne ya Juni 30, 2026, ndizo pia zitakazoamua bingwa wa Ligi Kuu Bara, japo ushindi huu kwa Yanga kwa sasa unaiweka katika maz-ingira mazuri zaidi tofauti na wapinzani wao.
Yanga itahitimisha msimu ugenini dhidi ya maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar, ambapo kwao hata sare tu itatwaa ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara, kuto-kana na tofauti ya mabao endapo pia Simba nayo itaifunga KMC kwani zote zitakuwa na pointi 73.
Lakini ushindi utanogesha zaidi ubingwa wa Yanga.
SIMBA HAIJAISHA MPAKA IISHE
Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Simba imeendelea kupambana katika harakati zake za kuutafuta ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa Singida Black Stars mabao 2-0.
Mabao mawili ya Simba yalifungwa na Elie Mpanzu dakika ya 28 akimalizia pasi ya Anicet Oura na lile la pili likiwekwa kambani na Oura kwa pasi ya Mpanzu.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 70 baada ya kucheza mechi 29, ikiendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa imefunga mabao 53 na kuruhusu 11 pekee, rekodi inayoifanya kuwa moja ya timu zenye safu bora ya ulinzi msimu huu.
Wekundu hao wa Msimbazi waliingia kwenye mechi hiyo wakisaka pointi tatu pekee ili kuendelea ku-wania ubingwa na kuweka presha kwa vinara wa ligi ambao ni watani zao, Yanga.
Licha ya ubora wa timu zote mbili kwenye dakika 90, Simba ilionyesha ubora mkubwa hasa kwenye sa-fu yao ya ulinzi ikiongozwa na beki Rushine De Reuck ambaye alikuwa na kazi ya kuondoa hatari lango-ni.
Kipigo ilichokipata Singida, imekuwa muendelezo wa kushindwa kufurukuta mbele ya Simba iliyoon-ekana kuwa na ubora mkubwa kila walipokutana katika misimu ya hivi karibuni.
Takwimu zinaonyesha Simba imekuwa na rekodi nzuri kila inapokutana na Singida. Kwenye mechi 10 za hivi karibuni, Simba imeshinda saba, Singida Black Stars ikishinda moja, huku mechi mbili zikimalizika kwa sare.
Mbali na ushindi huo, Simba imeendelea kuonyesha uimara wa safu yake ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao 11 katika mechi 29 za ligi, huku ikifunga mabao 53 msimu huu.
Licha ya kukusanya pointi tatu, Simba bado inalazimika kusubiri matokeo ya mechi ya mzunguko wa mwisho huku ikitumaini vinara wa ligi, Yanga wapoteze dhidi ya JKT Tanzania itakayopigwa Juni 30, 2026 kwenye Uwanja wa Isamuhyo ili kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa.
TANO ZABAKI NA PRESHA
Kule chini kwenye vita ya kupambana kuepuka kushuka daraja, baada ya KMC kuaga mapema ikiwa na pointi tisa ikicheza mechi 29, hivi sasa kuna timu tano zimebaki na presha.
Presha hiyo imebaki kwa Mtibwa Sugar iliyopo eneo la kushuka moja kwa moja kufuatia kukusanya pointi 27, huku Tanzania Prisons na Mbeya City zenye pointi 29 kila moja, zipo eneo la play off ya kupambana kubaki, wakati Fountain Gate (pointi 30) na Namungo (pointi 31), zitalazimika kushinda mechi za mwisho ili kutofikiwa na walio chini yao.
Mashujaa (pointi 33) sawa na Coastal Union, Dodoma Jiji (pointi 35) na Pamba Jiji (pointi 36), zote zipo salama kama ilivyo kwa JKT Tanzania (pointi 42), wakati Singida Black Stars (pointi 50) na Azam (pointi 61) zikiwa na tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Mtihani zaidi inao Mtibwa kwani inakwenda kucheza dhidi ya Namungo inayohitaji ushindi ili kubaki salama.
Mtibwa Sugar imezidi kuwa na presha kwani imepoteza ugenini dakika za mwisho kwa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mabao ya Seleman Boban dakika ya 70 na Kelvin Sengati dakika ya 90, yameipa pointi tatu Tanzania Prisons kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Matokeo hayo yanaifanya Mtibwa Sugar kushuka nafasi ya 15 kwa pointi 27 huku Prisons ikipanda nafasi ya 14 kwa pointi 29 ikijiandaa kumaliza msimu ugenini dhidi ya Mashujaa.
Mabadiliko ya Prisons kumtoa Haruna Chanongo na kuingia Boban ndio yaliipa matumaini ya kuendelea kuamini kukwepa kushuka daraja.
Hata hivyo haikuwa mechi nyepesi kwa timu zote kufuatia kila upande kuhitaji ushindi ili kujiweka paz-uri lakini wenyeji waliweza kutakata kwa pointi tatu.
Mtibwa Sugar ambayo imerejea msimu huu Ligi Kuu baada ya kudumu msimu mmoja Championship, imeendeleza gundu katika mechi za ugenini.
Prisons ndio ilitangulia kupata bao kupitia kwa Boban, ambapo Mtibwa Sugar ilisawazisha dakika ya 85 kupitia Juma Liuzio, kabla ya Sengati kuiongezea la pili na kurejesha furaha kwa Wajelajela hao.
Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema matokeo hayo si mazuri sana kwao na badala yake wanasubiri tu muujiza wa Mungu kwa mechi ya mwisho na Namungo.
“Mchezo ulikuwa mzuri na tulitawala kipindi cha kwanza, tunaenda kupambana mechi ya mwisho ja-pokuwa matokeo haya si mazuri kwetu, Ligi imekuwa ngumu na kilichobaki ni kudra za Mungu kujua tubaenda wapi,” alisema Kifaru.
Kocha Mkuu wa Prisons, Shedrack Nsajigwa, alisema licha ya ushindi huo kurejesha nafuu kikosini, lakini wanahitaji pointi tatu kwenye mechi dhidi ya Mashujaa ili kukwepa mchujo ‘Play Off’.
“Mchezo haukuwa rahisi kwa kuwa kila timu ilitaka ushindi japokuwa sisi ndio tulikuwa wahitaji zaidi, niwapongeze wachezaji na sasa tujipange na mechi ijayo,” alisema Nsajigwa.
MATOKEO MENGINE
Coastal Union ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, imefungwa 2-0 na Azam, wa-fungaji wakiwa Landry Zouzou dakika ya 2 na Feisal Salum dakika ya 32. Azam imefikisha pointi 61 ikiendelea kusalia nafasi ya tatu, Coastal ikiwa ya tisa na pointi 33.
Bao la Dodoma Jiji dakika ya 28 lililofungwa na Idd Kipagwile, lilikuwa la kusawazisha baada ya Mbeya City kutangulia dakika ya 13 kupitia Adili Buha kwa penalti kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Kule CCM Kirumba, Mwanza, wenyeji Pamba Jiji wamefungwa 2-1 na JKT Tanzania, huku Namungo na Fountain Gate zikitoka 0-0, Mashujaa ikiikandamiza KMC mabao 2-0, wafungaji wakiwa Balama Mapin-duzi dakika ya 32 na Isamil Mgunda dakika ya 34 kwa penalti.
DIARRA AMALIZA KAZI
Wakati Yanga ikikaribia kusherehekea pati la ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara, kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra amejihakikishia kumaliza kinara wa clean sheet msimu huu wa 2025-2026, baada ya nyota huyo kufikisha 17 ambazo haziwezi kufikiwa na makipa wengine kwa mechi moja iliyobaki.
Clean Sheets hizo 17 za Diarra ni sawa na alizokuwa nazo pia msimu uliopita wa 2024-2025, japo alizidi-wa mbili na kipa wa Simba, Moussa Camara aliyeibuka kidedea baada ya kufikisha 19, ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Horoya AC ya kwao Guinea.
Kipa aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kushindana na Diarra ni Mahamadou Tanja Kassali wa Simba, am-baye hata hivyo, kikosi hicho kisiporuhusu bao lolote ataishia na 16 ambazo haziwezi kumfia Diarra anayehitaji Clean Sheets moja ili kuivunja rekodi yake aliyoweka kwa msimu uliopita wa 2024-2025