
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk imetoa taarifa na kuonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko kubwa la vifo vya wahamiaji vinavyotokea katika vituo vya kuwazuilia wahamiaji nchini Marekani wakati wa muhula wa pili wa utawala wa Donald Trump, na ametaka kufanyika uchunguzi huru kuhusu suala hilo.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa yake kuwa ana wasiwasi kuhusu ukosefu wa uwazi kuhusiana na vifo vya wahamiaji vinavyotokea katika vituo vya kuwazuilia wahamiaji nchini Marekani.
Volker Turk ameongeza kusema kuwa,”Wale wote wanaohusika na ukiukaji wa sheria wanapaswa kuwajibishwa. Aidha, haki za familia za waathiriwa za kujua ukweli, kupata haki, kufidiwa madhara, na kuhakikishiwa kwamba matukio kama haya hayatatokea tena, zinapaswa kuheshimiwa.”
Mtandao wa Al Jazeera umeeleza kuwa vifo vya wahamiaji katika vituo vya kuwazuilia wahamiaji nchini Marekani vimeongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha muhula wa pili wa utawala wa Donald Trump. Kwa mujibu wa makundi ya kutetea haki za binadamu na mawakili wa masuala ya uhamiaji, hali hiyo inatokana na uzembe wa kimfumo, mazingira yasiyo ya kibinadamu katika vituo vya kuwazuilia wahamiaji, pamoja na vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wahamiaji.
Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilisema katika ripoti yake iliyochapishwa mwanzoni mwa mwezi huu:
Kiwango cha vifo katika vituo vya kuzuilia wahamiaji vinavyosimamiwa na Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) kimefikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita, na tangu kuanza muhula wa pili wa utawala wa Donald Trump, idadi hiyo imeongezeka zaidi ya mara mbili.