
Dar es Salaam. Wafugaji wa ng’ombe nchini sasa wataweza kulinda mifugo yao dhidi ya hasara zinazotokana na vifo, huku wakipata fursa ya kuitumia kama dhamana ya mikopo kupitia huduma mpya ya bima ya kidijitali, Smart Mifugo.
Huduma hiyo iliyozinduliwa leo Juni 29, 2026 inatumia teknolojia ya akili mnemba kutambua alama ya pua ya mnyama
Hafla hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, kupitia ushirikiano wa CRDB Insurance Company na Agriculture and Climate Risk Enterprise (ACRE Africa) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya mifugo kwa kutumia teknolojia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meena amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika zenye idadi kubwa ya mifugo sekta ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi kwa kutoa ajira, kuongeza usalama wa chakula na kipato cha kaya.
Hata hivyo, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za magonjwa ya mifugo, ukame, mafuriko na majanga mengine yanayosababisha wafugaji kupata hasara kubwa.
“Nafurahi kuona ushirikiano wa CRDB Insurance Company na ACRE Africa umeleta teknolojia ya kisasa kulinda mali za wafugaji wetu. Kupitia Smart Mifugo, wafugaji sasa wanaweza kupata bima kwa njia ya kidijitali kwa urahisi, usalama na uwazi zaidi,” amesema.
Amesema matumizi ya akili mnemba kutambua alama ya pua ya ng’ombe ni hatua kubwa katika kuboresha sekta hiyo kwa kuwa yataongeza uaminifu, kupunguza udanganyifu na kuboresha utoaji wa huduma za bima.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuleta ubunifu unaoongeza tija katika uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela amesema ubunifu huo umetokana na kutambua umuhimu wa sekta ya mifugo katika uchumi wa taifa na changamoto zinazowakabili wafugaji kupata bima na mikopo kutokana na kukosekana kwa mfumo wa uhakika wa kutambua umiliki wa mifugo.
Amesema kupitia teknolojia ya utambuzi wa alama ya pua ya ng’ombe (cow muzzle biometrics), kila mnyama atakuwa na utambulisho wa kipekee unaorahisisha uthibitishaji wa umiliki wake.
“Ubunifu huu unaondoa utata wa umiliki wa mifugo, unaongeza uaminifu katika utoaji wa huduma za bima na kuwezesha mifugo kutambulika rasmi kama mali yenye thamani inayoweza kutumika kama dhamana ya kupata mikopo,” amesema.
Dk Nsekela amesema baada ya uzinduzi nchini Tanzania, huduma hiyo itapanuliwa pia Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako Benki ya CRDB inatoa huduma na kuna idadi kubwa ya mifugo.
Amesema mbali na kuwalinda wafugaji dhidi ya hasara, Smart Mifugo itachochea ukuaji wa sekta ya mifugo, kuongeza uwekezaji, kupanua ujumuishaji wa kifedha vijijini na kuimarisha usalama wa chakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava amesema huduma hiyo ni sehemu ya dhamira ya taasisi hiyo kuendeleza ubunifu wa kifedha unaojenga uchumi jumuishi na endelevu.
“Leo tunaanza na ng’ombe, lakini tuna matarajio makubwa ya kupanua huduma hii kwa aina nyingine za mifugo kadri tunavyoendelea,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ACRE Africa, Ewan Wheeler amesema Tanzania ina takriban ng’ombe milioni 40 wenye thamani inayokadiriwa kufikia Dola 4.5 bilioni za Marekani lakini sehemu kubwa ya utajiri huo bado uko katika sekta isiyo rasmi.
“Matumizi ya akili mnemba katika utambuzi wa mifugo yataongeza imani kwa taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wafugaji, hatua itakayochochea uwekezaji na kuongeza tija katika sekta ya mifugo nchini,” amesema.