
Akizungumza katika Mkutano wa Nne wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa wa Wakuu wa Taasisi za Kupambana na Ugaidi, jijini New York, Marekani, Shamsiya Ibrahim Barde ameelezea uzoefu wake wa kukulia kaskazini mashariki mwa Nigeria, eneo lililoathiriwa vibaya na migogoro, na ambako vijana wengi wamekabiliwa na ukosefu wa usalama, kuhama makazi yao kwa lazima na athari za misimamo mikali yenye kutumia vurugu.
Shamsiya, ambaye ni mnufaika wa Mpango wa Uwezeshaji na Ushirikishwaji wa Vijana wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi (UNOCT), amesema mpango huo ulimpatia ujuzi wa mawasiliano ya kimkakati uliomwezesha;
- Kupambana na propaganda za makundi yenye misimamo mikali,
- Kushirikiana na jamii na
- Kuchangia juhudi za ujenzi wa amani.
“Mpango huo umeonesha kuwa vijana wanapoaminiwa, kuungwa mkono na kupewa fursa zenye maana, huwa mawakala wa kuzuia migogoro, wabunifu wa suluhisho na chachu ya mabadiliko chanya badala ya kuwa walengwa wa misimamo mikali,” amesema.
Amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuondokana na ushirikishwaji wa vijana wa kiwango cha ishara pekee na badala yake kuwahusisha kikamilifu katika kubuni, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini sera na programu zinazowahusu.
Shamsiya amekumbusha kuwa, “vijana si wanufaika tu wa juhudi za amani na usalama. Sisi ni washirika. Sisi ni wabunifu. Sisi ni wahamasishaji wa jamii. Sisi ni wajenzi wa amani.”
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, akihutubia ameonya kwamba kuongezeka kwa misukosuko ya kimataifa, mabadiliko ya tabianchi, ugumu wa hali ya kiuchumi na matumizi mabaya ya teknolojia zinazoibuka ikiwemo akili mnemba au AI, kunazalisha mazingira yanayowezesha ugaidi kustawi.
Amesema hali hizo ni “mazingira muafaka kwa ugaidi kustawi,” huku akisisitiza kuwa “maendeleo endelevu na ulinzi wa haki za binadamu ni nguzo muhimu katika kuzuia misimamo mikali yenye kutumia vurugu.”
- Nini Kifanyike?
- Kupanua fursa za kiuchumi.
- Kuhakikisha ushirikishwaji wa jamii za wachache.
- Kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika maamuzi na maendeleo.
- Kuunga mkono juhudi za ujenzi wa amani katika ngazi za jamii.
- Kulinda nafasi ya kiraia na uhuru wa kiraia.
- Ushuhuda wa manusura wa ugaidi unaweza kusaidia kupinga propaganda za makundi yenye misimamo mikali.
- Teknolojia inaweza pia kutumika kutambua vitisho mapema, kukomesha ufadhili haramu na kubaini njia zinazopelekea watu kuingia katika misimamo mikali.