s

Chanzo cha picha, Habari leo

“Mimi nikisikia hayo matrilioni ya deni, sielewi kabisa. Nachojua sasa kodi zinaongezeka.”

Hivyo ndivyo anavyoeleza Mama Zai, muuza duka katika eneo la Kilimahewa jijini Dar es Salaam, kila mjadala wa deni la taifa unapochukua nafasi kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Lakini kwa Shaban Abdallah, mkulima wa mpunga kutoka Rudewa mkoani Morogoro, mjadala huo una sura tofauti. “Kama mkopo umejenga barabara hii ya Dumila – Kilosa na mpunga wangu unafika sokoni kwa urahisi, sina shida na mkopo huo wanaousema,” anasema.

Mitazamo hiyo miwili imeibuka tena baada ya deni la Taifa la Tanzania kufikia Shilingi trilioni 114.34 hadi Machi mwaka huu, likiongezeka kutoka Shilingi trilioni 104.93 katika kipindi kama hicho mwaka 2025. Kwa mujibu wa Serikali, deni la ndani ni Shilingi trilioni 38.44 huku deni la nje likiwa Shilingi trilioni 75.89.

Kwa wengi, namba hiyo ni kubwa kiasi cha kutisha. Lakini nyuma yake kuna swali ambalo kwa miongo mingi limekuwa likiulizwa: Kama Serikali inaweza kuchapisha fedha, kwa nini iendelee kukopa?

Kama kuchapisha fedha kunaonekana rahisi, kwa nini Serikali haifanyi hivyo?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mtazamo wa kawaida, suluhisho linaonekana rahisi. Kama Serikali ndiyo inayosimamia fedha kupitia Benki Kuu, kwa nini isichapishe noti za kutosha kujenga reli, barabara, hospitali na shule badala ya kuongeza deni?

Swali hilo si geni. Limewahi hata kuwa kichwa cha makala ya mchumi wa Taasisi ya Levy Economics nchini Marekani, L. Randall Wray, aliyeuliza: “If Government can print money, why does it borrow?” Kichwa kilichojenga msingi wa makala hii: Kama serikali inaweza kuchapisha fedha, kwa nini ikope?

Kwa mujibu wake, watu wengi hudhani serikali hukopa kwa sababu imeishiwa fedha, ilhali sababu ni pana zaidi kuliko hivyo. Sababu ya kwanza ni kwamba fedha si utajiri.

Fedha ni chombo cha kubadilishana bidhaa na huduma. Ukiongeza fedha bila kuongeza uzalishaji wa bidhaa, huduma na ajira, uchumi hauongezeki; kinachoongezeka ni kiasi cha fedha kinachozunguka mikononi mwa watu.

Mchumi na mwandishi wa kitabu Cracking Economics, Tejvan Pettinger, anaeleza jambo hilo kwa sentensi rahisi: “Kuchapisha fedha hakuzalishi bidhaa au huduma zaidi. Huongeza tu kiasi cha fedha kinachozunguka kwenye uchumi.”

Anachomaanisha, kuchapisha fedha hakuongezi mchele, saruji, dawa hospitalini wala umeme. Huongeza tu noti zinazogombea bidhaa hizo.

Fikiria Tanzania ina magunia milioni moja ya mpunga yanayouzwa kwa wastani wa Shilingi 100,000 kila moja. Serikali ikaongeza fedha mara mbili, lakini mavuno yakabaki yale yale. Wanunuzi watakuwa na fedha nyingi zaidi mfukoni, lakini mpunga utabaki magunia milioni moja.

Matokeo yake? Bei ya mpunga itapanda. Si kwa sababu umeongezeka, bali kwa sababu fedha zinazougombea zimeongezeka.

Ndiyo maana wachumi huonya kuwa kuchapisha fedha kupita kiasi kunaweza kusababisha mfumuko wa bei, kupunguza thamani ya fedha na kuongeza gharama za maisha. Pettinger anaonya pia kuwa hatua hiyo inaweza kushusha thamani ya sarafu ya nchi na kuwafanya wawekezaji wasiwe tayari kuikopesha serikali kwa masharti nafuu.

Lakini hiyo si sababu pekee. Kwa mujibu wa Randall Wray, serikali nyingi hukopa pia kwa sababu mfumo wa fedha umejengwa kwa namna inayosaidia kudhibiti viwango vya riba, kuimarisha masoko ya fedha na kuweka utulivu wa uchumi. Kwa maneno mengine, kukopa si lazima kuwe ishara kwamba Serikali imeishiwa fedha.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mfuatiliaji mwingine wa masuala ya fedha na uchumi, Vallary Mmbone, anayesema: “Kukopa kunaweka nidhamu katika matumizi ya Serikali. Kila mkopo huambatana na wajibu wa kulipa fedha pamoja na riba, hivyo hulazimisha Serikali kupanga matumizi yake kwa umakini na kuwajibika zaidi kwa fedha za umma.”

Kwa maneno mengine, mkopo una tarehe ya kulipa, una riba na una masharti. Hivyo hulazimisha Serikali kupanga matumizi yake kwa umakini zaidi kuliko kama ingeweza kuchapisha fedha bila kikomo.

Kama kuchapisha fedha si suluhisho, kukopa ni suluhu?

.

Chanzo cha picha, MW

Tanzania inadaiwa shllingi Trilioni 114, deni ambalo kwa Mujibu wa msemaji wa Serikali Gerson Msigwa ni ‘himilivu.

“Tathimini inaonyesha kuwa deni letu la taifa ni himilivu sana, ukomo wa deni la serikali kukopa kwa pato la taifa ni asilimia 55%, sisi mpaka sasa tuko asilimia 40.7%”, anasema Msigwa.

Si Tanzania tu inayokopa, karibu kila nchi duniani hukopa. Marekani, Japan, China, India, Uingereza na hata mataifa mengi ya Afrika yana madeni ya umma, tena yaliyo na kiwango cha juu ya ukomo wa uhimilivu. Tofauti si kama nchi inakopa au la, bali inakopa kwa sababu gani, inakopa kutoka wapi na fedha hizo zinafanya kazi gani.

Kwa mujibu wa Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, aliwahi kueleza kwamba deni ni chanzo halali cha mapato kwa serikali nyingi duniani kwa sababu mapato ya kodi mara nyingi hayatoshi kugharamia mahitaji yote ya wananchi.

Fikiria Serikali imekusanya shilingi trilioni 40 kupitia kodi, lakini inahitaji trilioni 45 kugharamia elimu, afya, maji, usalama na huduma nyingine muhimu. Tofauti hiyo ya shilingi trilioni tano ndiyo inayojulikana kama nakisi ya bajeti (budget deficit). Kushughulikia nakisi hiyo serikali inaweza kupunguza huduma, kuongeza kodi au kukopa. Mara nyingi huchagua kukopa ili huduma zisiathirike.

Lakini kuna sababu nyingine kubwa zaidi. Miradi mikubwa ya maendeleo haiwezi kusubiri mpaka kodi ikusanywe kwa miaka 10 au 20. Reli, mabwawa ya umeme, bandari, hospitali na barabara vinahitaji fedha nyingi kwa wakati mmoja. Serikali hukopa leo kwa matarajio kwamba uchumi utakua kesho na mapato yatakayozalishwa na uwekezaji huo yatasaidia kulipa deni.

Profesa Aurelia Kamuzora anasema: “Deni la taifa linavyozidi kukua, uchumi nao unaweza kukua ikiwa fedha zinazokopwa zinawekezwa vizuri.”

Anafafanua kuwa fedha za mikopo zinapoingia kwenye miradi yenye tija, huzunguka kwenye uchumi, huongeza ajira, uzalishaji na biashara. Hata hivyo, anasisitiza kuwa mikopo yenye masharti nafuu ndiyo yenye manufaa zaidi kwa uchumi kuliko mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa.

Vyanzo vikuu vitatu vya mikopo inayojenga deni la taifa

Chanzo cha kwanza ni ndani ya nchi. Serikali huuza hati fungani na dhamana za Serikali (Treasury Bonds na Treasury Bills), ambazo hununuliwa na benki, mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF, kampuni na hata wananchi. Mtu anaponunua hati fungani, kwa maana nyingine anaikopesha Serikali, ambayo huahidi kumrudishia fedha zake pamoja na riba baada ya muda uliokubaliwa.

Chanzo cha pili ni wawekezaji wa nje, wanaonunua hati fungani za Serikali ya Tanzania kupitia masoko ya fedha.

Chanzo cha tatu ni mikopo kutoka taasisi za kimataifa na washirika wa maendeleo, kama Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika na taasisi nyingine za kifedha.

Akizungumzia mwenendo wa deni la Tanzania, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa anasema sehemu kubwa ya deni hilo ni la nje.

“Kwa kiasi kikubwa tumekopa fedha kutoka nje, takribani trilioni 75.89 na deni la ndani ni trilioni 38.44. Tunakopa ili tukamilishe miradi mbalimbali ambayo wananchi wanaisubiri.”

Kwa mujibu wa Msigwa, fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, miradi ya maji, ujenzi wa barabara, upanuzi wa bandari na kuongeza uzalishaji wa umeme.

Anasema uwezo wa kuzalisha umeme umeongezeka kutoka megawati 1,902 hadi zaidi ya 4,000, huku bajeti ya kilimo na maji nayo ikiongezwa kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi.

Lakini wachumi wanaonya kuwa kukopa pekee hakumaanishi maendeleo.

Beatrice Kimaro anasisitiza: “Huwezi kukwepa kukopa kama unataka kufanya shughuli za maendeleo kwweli. Lakini kama unakopa na kufanya matumizi ya kawaida yasiyo na tija, ndipo mkopo unakuwa tatizo.”

Kauli hiyo inaendana na msimamo wa mchambuzi Damas Kanyabwoya, ambaye anasema mjadala wa deni haupaswi kuishia kwenye kutaja trilioni zilizokopwa. Badala yake, wananchi wanapaswa kuhoji kila shilingi ilikokwenda na matokeo yake.

Kwa maneno mengine, swali muhimu si Tanzania imekopa kiasi gani, bali fedha hizo zimezalisha nini.

Mwisho wa siku, deni la trilioni 114 Tanzania analilipa nani?

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Hili ndilo swali ambalo huibua hisia zaidi kuliko takwimu zote za uchumi. Je, deni la taifa hulipwa na Serikali au na wananchi?

Mwaka 1967, wakati wa Azimio la Arusha, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutoa tahadhari ambayo bado inanukuliwa hadi leo. “Hata tukitumia mikopo kujenga shule, hospitali au viwanda, lazima ilipwe. Mlipaji ni mkulima wa vijijini.”

Lakini Serikali inakuja na mtazamo muhimu kuhusu namna wananchi wanavyopaswa kulielewa deni hilo. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesisitiza kuwa: “Hakuna mtu atakayetozwa fedha za mfukoni kulipa deni la taifa.”

Kwa mtazamo wa wachumi, kauli hizo mbili hazipingani moja kwa moja. Hakuna mwananchi atakayeitwa ofisini na kupewa bili ya kulipa sehemu ya trilioni 114. Hata hivyo, Serikali hulipa madeni yake kupitia mapato inayokusanya kila mwaka, na sehemu kubwa ya mapato hayo hutokana na kodi, ushuru na tozo zinazolipwa na wananchi na wafanyabiashara.

Ndiyo maana aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliwahi kusema: “Mwisho wa siku, kila mwananchi hulipa deni hili kupitia kodi anazolipa kwenye bidhaa na huduma anazotumia.”

Kwa maneno mengine, deni la taifa halina jina la Mama Zai wala Shaban Abdallah, wala Yusuph Mazimu, lakini uchumi wanaoushiriki kila siku ndiyo unaobeba jukumu la kulihudumia.

Swali linalofuata ni ikiwa deni hilo bado linaweza kubebwa bila kuathiri uchumi. Kwa mujibu wa Serikali, jibu ni ndiyo. Akizungumza bungeni mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisema ongezeko la deni halimaanishi moja kwa moja kuwa nchi iko kwenye hatari.

“Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa baadhi ya mikopo tuliyopokea sasa ilisainiwa miaka ya nyuma. Pia, mabadiliko ya thamani ya fedha yamechangia kuonekana kuwa deni limeongezeka.”

Serikali inaeleza kuwa kipimo muhimu si ukubwa wa deni pekee, bali uwiano wa deni kwa Pato la Taifa (Debt-to-GDP Ratio). Kwa sasa uwiano huo ni takribani asilimia 40.7, chini ya ukomo wa asilimia 55 unaotumika kama moja ya viwango vya kupima uhimilivu wa deni kwa nchi zenye uchumi kama wa Tanzania.

Profesa Anna Tibaijuka aliwahi kusema mwaka jana kwamba pamoja na uwiano huo kuwa ndani ya viwango vinavyokubalika, kuna kipimo kingine muhimu zaidi cha kutazama, ni kiasi gani cha mapato ya Serikali kinatumika kulipa madeni badala ya kugharamia elimu, afya, maji na huduma nyingine za wananchi?

Kwa upande wake, mchambuzi Damas Kanyabwoya anashauri mjadala wa deni usiishie kwenye kutaja trilioni zilizokopwa. Anasema wananchi wanapaswa kujua kila shilingi ilikokwenda, ilifanya kazi gani na matokeo yake ni yapi.

Mtazamo unaoungwa mkono na utafiti wa Oxford Review ulionukuliwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP), David Kafulila, unaoonyesha kuwa katika mataifa 13 yenye uchumi mkubwa duniani, asilimia 62 ya utajiri wa nchi unatokana na rasilimali watu, asilimia 25 unatokana na taasisi imara, huku maliasili zikichangia karibu asilimia tano pekee.

Kwa maana hiyo, deni pekee haliwezi kuifanya nchi kuwa tajiri au maskini. Kinachoamua ni namna fedha hizo zinavyowekezwa, ubora wa taasisi zinazosimamia matumizi yake na uwezo wa uchumi kuzalisha mapato yatakayolipa deni hilo.

Ndiyo maana mjadala kuhusu trilioni 114 haupaswi kuishia kwenye ukubwa wa namba.Unapaswa kuendelea kuuliza je, kila shilingi inayokopwa leo inajenga uchumi ambao kesho utaweza kulilipa deni hilo bila kumbebesha mzigo mkubwa mwananchi wa kawaida kama Mama Zai na Shaban Abdallah?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *