
Joto huwaathiri watu wote, lakini mawimbi ya joto yanaweza kuwa hatari kubwa kiafya kwa watu wanaohudhuria mikusanyiko mikubwa na matukio ya michezo, amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia video iliyochapishwa leo Juni 29 katika ukurasa wake wa mtandao wa X.
Kama sehemu ya Kombe la Dunia la FIFA, WHO imekuwa ikishirikiana na FIFA pamoja na nchi mwenyeji ili kuwalinda wachezaji, maafisa na mashabiki dhidi ya athari za joto kali kupitia mpango uliopewa jina, Beat the Heat au saw ana kusema ‘Lishinde Joto’.
Mpango huo unasaidia kuandaa mipango ya kukabiliana na joto kali, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, kuboresha upatikanaji wa maji salama ya kunywa, kuhamasisha umma kuhusu hatari za joto kali na kutekeleza mikakati ya kupunguza joto pamoja na upangaji bora wa matukio.
“Joto huwaathiri watu wote, lakini mawimbi ya joto yanaweza pia kuwa hatari kubwa ya kiafya kwa watu wanaohudhuria mikusanyiko mikubwa na matukio ya michezo,” Dkt. Tedros amesema.
Joto kali duniani
Juhudi hizo zinakuja wakati nchi nyingi duniani zikikumbwa na mawimbi ya joto yanayozidi kuongezeka kwa ukali na mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya tabianchi, huku wataalamu wa afya wakionya kuwa joto kali linaendelea kuwa moja ya vitisho vikubwa zaidi vya kimazingira kwa afya ya binadamu.
Kwa mujibu wa WHO, joto kali linaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini, uchovu unaotokana na joto na kiharusi cha joto, pamoja na kuzidisha magonjwa ya moyo, mfumo wa upumuaji na figo. Wazee, watoto, watu wenye magonjwa sugu na wafanyakazi wanaofanya kazi nje wako katika hatari zaidi.
Mpango wa Beat the Heat, uliobuniwa kwa ushirikiano kati ya WHO, FIFA na nchi mwenyeji, unalenga kuhakikisha kuwa matukio ya michezo na mikusanyiko mikubwa xc yanaandaliwa vyema kukabiliana na joto kali kupitia mipango madhubuti, hatua za afya ya umma na mifumo ya uratibu wa dharura.
WHO inasema kuwa tahadhari za mapema, upatikanaji wa maji ya kutosha, maeneo ya kivuli na mikakati ya kupunguza joto vinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa na vifo vinavyohusishwa na joto kali.
Kadiri mabadiliko ya tabianchi yanavyochochea ongezeko la joto duniani, WHO inazitaka serikali, waandaaji wa matukio na jamii kuweka ulinzi dhidi ya joto kali kuwa sehemu muhimu ya mipango ya afya ya umma.