
Vyombo vya habari vinaripoti kuwa zaidi ya watu 1,450 wamepoteza maisha na hivyo mshikamano huo katika uokozi unakuja wakati wananchi wenyewe hivi sasa wanasema hata kama ndugu zao wamefukiwa chini na vifusi basi angalau wawaone kwa mara ya mwisho.
Video ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA inaanzia kwenye jimbo la La Guaira lililoko kaskazini mwa mji mkuu wa Venezuela, Caracas. Taswira ni vifusi vya majengo yaliyoporomoshwa na matetemeko ya ardhi ya jioni ya jumatano ya Juni 24 mwaka huu wa 2026.
Hata kama wamekufa basi tuone miili yao tuagane nao
Manusura wa tetemeko la ardhi wanaonekana hawaamini macho yao na mfanyakazi wa huduma za kibinadamu anaonekana akimkumbatia mmoja wa manusura hao Mireya Quesada sojo. Bi. Sojo kwa huzuni anasema, “kwanza kabisa kwa kutumia mikono yetu tulianza kuchimba kwenye vifusi kujaribu kuona iwapo tutawaona jamaa zetu. Tunajua hawako tena hai, lakini angalau tuweze kuwaona tena, hataka kama ni majonzi. Kwa hiyo, tunaomba msaada ili tuweze kuwafukua. Watu wamekuja kujaribu kusaidia, na kwa hilo tunashukuru mno.”
Manusura mwingine ni Nury Camacho, yeye akaulizwa na msaidizi wa kibinadamu ni wanafamilia wangapi ambao amepoteza? Na huku akielekeza akasema, hapa watano. Kule wengi sana wamekufa.
Waokoaji wakionekana juu ya kifusi cha moja ya jengo lililoporomoka wanaendelea na kazi huku upande mwingine waokoaji wengine wakiwa na vizibao vya rangi ya chungwa wanatembea mstari mmoja wakiwa kila mmoja amebeba mfuko bila shaka wenye vifaa vya uokoaji.
Tunahamasisha uchangiaji wa rasimali – UNDAC
Stefania Trassari ni Naibu Kiongozi wa timu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu na Tathmini ya Majanga, UNDAC anasema, “kwenye mitaa tunaona watu waliofurushwa makwao, familia zilizopoteza kila kitu zikihitaji msaada wa kibinadamu. Kwa hiyo tuko hapa kuhamasisha uchangiaji wa rasilimali, na kama unavyoona tuko kwenye eneo hapa ambako timu ya Kutafuta na Kuokoa imekutana na wanatoka maeneo mbali mbali duniani. Leng oni kutoa aina hii ya msaada, kunasua watu kwenye vifusi.”
Na eneo hili walilokusanyika waokoaji hawa ni kwenye uwanja wa mpira ambao sasa umegeuzwa pia makazi. Bendera za nchi zao wanakotoka waokozi hawa zinapepea na mojawapo ni Ujerumani.
Je ni nini kipaumbele cha Umoja wa Mataifa kwenye janga hili lililokumba Venezuela? Gianluca Rampolla ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa MAtaifa kwenye taifa hili la Amerika ya Kusini anafafanua kwamba, jambo la kwanza ni kuwaokoa watu ambao bado wako hai chini ya vifusi. Ndiyo maana kipaumbele ni kusaidia na kuratibu timu zinazowasili kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ukweli ni kwamba, katika wakati ambao mara nyingi tunaangazia mambo yanayoenda vibaya duniani, hapa tunaona ishara ya mshikamano kutoka dunia nzima katika kuwaunga mkono watu wa Venezuela. Kwa hiyo, tuunge mkono juhudi za utafutaji na uokoaji wa wale waliobaki chini ya vifusi, na wakati huohuo tuwasaidie manusura.”
Video nyingine ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF inatupeleka manispaa ya Libertador iliyoko mji mkuu Caracas ambako watoto na familia zao wako kwenye eneo la wazi baada ya nyumba zao zikiendelea kufanyiwa tathmini iwapo ni salama kwa kuishi.
Familia zinasubiria tathmini za makazi yao
Na kwenye kitongoji cha Catia hapa hapa Caracas nyakati ni usiku na akina mama na watoto wao wanaonekana wanapata mlo, mama mmoja angalau amepata fursa ya kumnyonyesha mtoto wake mchanga, ingawa machoni anaonekana na fikra lukuki kuhusu masaibu yaliyowafika.
Kwingineko, watoto na wazazi wao wanaelekea kwenye makazi ya muda baada ya kupokea mgao wa vifaa vya misaada vikiwemo vyakula, maji na mablanketi kwenye hospitali ya Catia.
Hofu ni usalama lakini Bwana Rampolla, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa anasema, “tunashirikana na serikali, mamlaka za mikoa na serikali za mitaa, pamoja na jeshi na taasisi za ulinzi wa raia.”
Wakati waokoaji wakitumia vifaa mahsusi kuchimba katikati ya vifusi iwapo wanaweza kubahatika walioko hai, au hata kama wamefariki dunia basi wapumzishwe kiutu, narejea kwa Stefania Trassafri, afisa wa UNDAC wanaotathmini na kuratibu majanga akielezea vipaumbele.
“Vipaumbele vya msingi kwa sasa ni msaada wa chakula; katika sekta ya afya, huduma za matibabu; makazi kwa wale waliopoteza nyumba zao na wanaoishi barabarani; pamoja na vifaa muhimu vitakavyowawezesha kuishi kiutu katika siku chache zijazo.”