Hispania imepata pigo baada ya mshambuliaji wake Yeremy Pino kuumia na sasa atakosa mechi zote zilizobakia za Kombe la Dunia mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti, hali ya Pino, mwenye umri wa miaka 23, sio nzuri baada ya kuumia dhidi ya Uruguay ambao Hispania ilishinda bao 1-0.
Kocha Mkuu wa Hispania, Luis De la Fuente, amesema kuwa nyota huyo wa Crystal Palace alipata jeraha kwenye mfupa wa bega baada ya kugongana angani na mchezaji wa Uruguay na kutua kwa nguvu kwenye bega lake la kushoto.
Mshambuliaji wa Hispania, Yeremy Pino. Picha na Mtandao
Hispania pia ipo na hofu ya kumkosa winga, Nico Williams anayesumbuliwa na maumivu wa nyonga.
Williams aliingia uwanjani akitokea benchi katika kipindi cha pili dhidi ya Uruguay, kama ilivyokuwa kwa Pino ingawa yeye aliweza kumaliza mchezo.
Hali hiyo inakuja baada ya Williams kuwa na msimu uliogubikwa na majeraha kabla ya kuitwa na De la Fuente kujiunga na kikosi cha Hispania kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Winga wa Hispania, Nico Williams wakati alipochezewa faulo kwenye mechi dhidi ya Uruguay. Picha na Mtandao
Hispania itavaana na Austria Julai 2, 2026 katika hatua ya 32 bora ya mashindano hayo makubwa dunini. Katika hatua ya makundi, vigogo hao wa Ulaya walimaliza katika nafasi ya kwanza ya kundi H baada ya kukusanya idadi ya pointi saba.
Licha ya kuanza kwa suluhu dhidi ya Cape Verde, Hispania ilirejea vizuri katika mechi ya pili baada ya kuichapa Saudi Arabia mabao 5-0, kisha ikaitupa nje Uruguay kwa kuifunga bao 1-0.