
Ripoti hiyo, Tathmini ya Haraka ya Hali ya Kijamii na Kiuchumi Kuhusu Mlipuko wa Ebola katika DRC, inaonya kuwa mlipuko wa sasa wa virusi vya Bundibugyo Ebola ni mshtuko mkali wa kurudisha nyuma maendeleo na kuongeza umaskini katika DRC na nchi jirani, zikiwemo Uganda, Rwanda na Sudan Kusini. Ingawa tishio la haraka la kiafya ni kubwa na linahitaji hatua za kudhibiti kama karantini, baadhi ya vizuizi vya jumla vya usafiri na biashara kwa bahati mbaya vinaharibu uchumi wa maeneo na maisha ya watu wanaofanya biashara zisizo rasmi.
“Ebola haizuiliwi kwenye lango la hospitali,” anasema Ahunna Eziakonwa, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa UNDP wa Kanda ya Afrika na anaongeza akisema, “inaathiri maisha, elimu, uhakika wa chakula, biashara, fedha za umma na imani. Ikiwa tutachukulia mlipuko huu wa Ebola kama changamoto ya afya pekee, tunaweza kukosa kuona dharura kubwa zaidi ya maendeleo inayoendelea kujitokeza.”
Uchambuzi unaonesha kuwa uharibifu wa kiuchumi unaenea zaidi ya wale walioambukizwa, ukizigharimu zaidi jamii zilizo hatarini ambazo hazina akiba ya kukabiliana na mshtuko huo. Hata katika hali ya msingi ambapo virusi vinadhibitiwa kwa mafanikio katika DRC na Uganda, athari za kiuchumi bado ni kubwa, ambapo DRC inakadiriwa kupoteza zaidi ya dola bilioni 1 za pato halisi la taifa (GDP) na kupoteza ajira 55,000.
Usumbufu wa biashara, vizuizi vya mipakani, ucheleweshaji wa usafiri, kushuka kwa imani ya watumiaji na kuvurugika kwa masoko yasiyo rasmi kunaweza kupunguza GDP ya bara kwa dola bilioni 2.37, hata kama maambukizi yatabaki kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa. Asilimia 20 ya kaya maskini zaidi zinatarajiwa kukumbwa na kushuka kwa matumizi ya kila siku kwa asilimia 1.76, hasara ambayo inafuta mafanikio dhaifu ya maendeleo na kutishia kuanzisha mgogoro wa umasikini wa muda mrefu.
Athari kijinsia
Mtikisiko huu wa umaskini pia una athari kubwa za kijinsia. Tathmini inaeleza jinsi wanawake wanavyokabiliwa na mgogoro wa ziada kutokana na majukumu yao ya kijamii na nafasi zao za kiuchumi. Kwa kuwa wanawake wanatawala sekta ya biashara isiyo rasmi ya mipakani, vizuizi vinaathiri zaidi uwezo wao wa kupata kipato. Wanawake pia wanaunda idadi kubwa ya wahudumu wa afya wa mstari wa mbele na mara nyingi huwa walezi wakuu nyumbani, hali inayowaweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi moja kwa moja.
Ripoti inakadiria kuwa kuvurugika kwa huduma za afya kunaweza kusababisha hadi vifo vya ziada vya watoto wachanga 2,520 katika DRC kutokana na sababu zisizo za Ebola.
Ushauri
Ili kupunguza athari hizi kubwa za kijamii na kiuchumi, tathmini ya UNDP inapendekeza mfumo wa sera wenye ngazi nyingi na unaozingatia usawa wa kijinsia:
• Kutoa msaada lengwa: Utekelezaji wa uhamishaji fedha taslimu na ruzuku za matumizi kwa makundi yaliyo hatarini zaidi, hasa kaya zinazoongozwa na wanawake.
• Kubadilisha utaratibu wa ufungaji mipaka na kujielekeza katika mifumo inayoruhusu biashara kuendelea.
• Kulinda matumizi ya kijamii: Kuanzisha mifumo ya dharura ya kifedha kuhakikisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto zinaendelea kufanya kazi kikamilifu sambamba na ajibu ya Ebola.