Katika taarifa yake Jumatatu usiku, msemaji wa Hamas, Hazem Qassem, alisema kwamba mtoto wa Kipalestina asiye na hatia aliyeuawa jana na jeshi la Israel ndiye mwathirika wa hivi karibuni zaidi miongoni mwa makumi ya maelfu ya watoto wa Kipalestina waliouawa katika mashambulizi ya mabomu ya Wazayuni, njaa, kunyimwa huduma za matibabu, ugaidi na kutokana na huzuni ya kufiwa na wazazi wao.
Ni baada ya msichana mdogo wa Kipalestina kuuawa shahidi jioni ya jana Jumatatu wakati ndege za kivita za Israel ziliposhambulia kwa mabomu mahema yaliyochakaa yaliyokuwa yakihifadhi familia zilizokimbia makazi yao huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
“Uhalifu wa Israel unaendelea kufanyika huku dunia ikitazama na kusikia kila kitu lakini haifanyi chochote,” amesema Qassem akikosoa kimya cha jamii ya kimataifa ambacho amekitaja kuwa ni ushiriki wa moja kwa moja katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amezikosoa vikali nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiarabu, (Arab League) vyama vya siasa, mabunge, wasomi na wanazuoni wa Kiarabu kwa kutochukua hatua na kutojali kwao mbele ya ukatili huo.
Hazem Qassem pia ameilaani vikali Mamlaka ya Palestina, akiikosoa kwa kuendelea kuwa mtazamaji asiyejali mauaji yanayofanyika huko Gaza, kana kwamba uhalifu huo unafanyika katika sayari nyingine.
Msemaji wa Hamas ametangaza kwamba wale wote ambao wananyamazia kimya uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza watawajibika mbele ya Mungu kwa damu ya mtoto huyo na mashahidi wote wa Ukanda wa Gaza katika vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni. Ameongeza kwamba, ukimya wao umewezesha kuendelea uhalifu huu wa kutisha dhidi ya binadamu.

Vyanzo vya kimatibabu huko Gaza vimethibitisha kwamba kwa uchache Wapalestina wanane, wakiwemo watoto wawili, waliuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel katika ukanda huo jana Jumatatu, huku wengine zaidi ya 40 wakijeruhiwa.
Katika taarifa ya awali, Hazem Qassem alieleza hali ya Gaza kuwa ni “damu inayoendelea kumwagwa,” huku huzuni na hofu vikizidi kutanda katika neo hilo zima la Palestina.
“Gaza inabaki kuwa jeraha linalovuja damu, huku huzuni na hofu vikiwa vimekita mizizi. Hasara hii isiyo na mwisho na mauaji yasiyositiishwa yanaendelea huku wale wanaotuzunguka wakitazama tu na kuona mauaji yetu kana kwamba tunatoka sayari nyingine,” amesema msemaji wa Hamas.
Vita vya mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza, vilivyosita chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano Oktoba 10, 2025, vimeua shahidi Wapalestina 73,000 na wengine zaidi ya 173,000 walijeruhiwa. Majeshi ya Israel pia yamesababisha uharibifu mkubwa ulioathiri takriban 90% ya miundombinu ya raia, jambo ambalo limetatiza operesheni za kuopoa maelfu ya maiti zilizonaswa chini ya vifusi.