Akizungumza kwenye Kongamano la Dunia dhidi ya Hukumu ya Kifo, Türk amesema Umoja wa Mataifa unapinga adhabu hiyo kwa mazingira yote bila kujali aina ya kosa.

“Hukumu ya kifo haiendani na utu wa binadamu na haki za msingi, hususan haki ya kuishi.”

Türk amesema kuua mtu kwa makusudi kupitia mfumo wa sheria si haki, bali ni adhabu ya kikatili, isiyo ya kibinadamu na inayodhalilisha utu.

“Kumuua mtu kwa makusudi ni kitendo cha kikatili, kisicho cha kibinadamu na kinachodhalilisha.”

Amesema katika nchi nyingi ambako hukumu hiyo bado ipo, mara nyingi hutumika kwa ubaguzi, huku maskini na watu wa jamii zilizotengwa wakibeba mzigo mkubwa zaidi.

Kwa mujibu wa Türk, hukumu ya kifo pia haijawahi kuthibitishwa kupunguza uhalifu, ikiwemo makosa yanayohusiana na dawa za kulevya. “Hukumu ya kifo imeshindwa katika kila ngazi.” Amesema.

Wengi waiondoa

Pamoja na kuhimiza huko kuondolewa kwa adhabu ya kifo, amesema kuna maendeleo makubwa duniani kwani karibu asilimia 90 ya nchi zimeondoa hukumu hiyo kisheria au zimeacha kuitumia kwa vitendo.

Hata hivyo, ameonya kuhusu baadhi ya mataifa yanayorudisha au kupanua matumizi ya adhabu hiyo, akizitaja nchi za Israel, Burkina Faso, Iran na China.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Türk ametoa wito kwa serikali, mashirika na wadau wote duniani kushirikiana kuhakikisha hukumu ya kifo inakuwa historia.

“Tunahitaji juhudi za pamoja kuhakikisha mfumo huu wa kikatili unabaki historia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *