
NI vita nyingine mpya. Ndivyo unavyoweza kusema kuelezea mtifuano wa kukwepa kushuka daraja kati ya ndugu, Tanzania Prisons na Mbeya City.
Hii ni baada ya matokeo ya jumla ya Ligi Kuu kumalizika kwa msimu wa 2025/26, huku timu hizo za jijini Mbeya zikiangukia hatua ya mchujo wa kuwania kubaki au kushuka daraja.
Katika mechi za kuhitimisha msimu, Mbeya City ikiwa nyumbani Uwanja wa Sokoine ililazimishwa sare ya bila kufungana na TRA United, huku Tanzania Prisons ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa. Wakati huohuo, Mtibwa Sugar ilishuka daraja baada ya kufungwa mabao 2-1 na Namungo, na hivyo kuungana na KMC waliokuwa tayari wameshuka kwenda Championship.
Katika mchezo huo, Mbeya City ilionesha dhamira na uhitaji mkubwa wa kupata pointi tatu, jambo lililodhihirishwa na mashambulizi ya mara kwa mara, lakini wapinzani wao walikuwa imara katika kudhibiti hatari zote.
TRA United ilicheza kwa utulivu, ikitegemea mashambulizi ya kushtukiza, mbinu ambayo haikuwapa mafanikio ya kupata bao.
Hata hivyo, Mbeya City itajilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi nne muhimu, zikiwamo mbili za mipira ya faulo na nyingine za mashuti ya mbali katika dakika za 37, 56 na 67, ambapo baadhi ya mipira iligonga mwamba wa lango na mingine kupita nje kidogo ya lango.
Wenyeji hao, waliorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kudumu misimu miwili Championship, walihitaji pointi tatu ili kukwepa kushuka daraja na kucheza hatua ya mchujo (play-off), lakini matokeo hayo sasa yanawafanya kusubiri hatima yao kulingana na matokeo ya wapinzani wao waliokuwa juu na chini yao kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Katika mchezo huo, mwamuzi Omary Mdoe kutoka Tanga aliwaonyesha kadi za njano wachezaji watatu wa TRA United ambao ni Jean Noel kwa kupoteza muda, Mzamiru Yassin na Joe Makoye.