
Mamlaka za Venezuela zimeripoti kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na matetemeko ya ardhi ya tarehe 24 Juni imefikia 1,719. Idadi ya waliojeruhiwa imeongezeka hadi 5,000.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu kutokea Caracas, Venezuela, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Gianluca Rampolla, amesema watu 7 waliokolewa wakiwa hai siku ya Jumapili, huku shughuli za kuwatafuta manusura zikiendelea chini ya vifusi.
Rampolla ambaye pia ni Mratibu wa UN wa Masuala ya Dharura Venezuela amesema;
- Takriban watu 12,000 wamekosa makazi kutokana na janga hilo.
- Zaidi ya waokoaji 2,000 kutoka nchi 27, pamoja na timu zaidi ya 40 za utafutaji na mbwa wa uokoaji, wanaendelea na operesheni katika maeneo yaliyoathirika.
- Umoja wa Mataifa na Serikali ya Venezuela wanatoa huduma za dharura ikiwemo afya, chakula, maji, makazi ya muda na ulinzi kwa waathirika, huku wakijiandaa kwa mahitaji makubwa zaidi ya kibinadamu.
- Maeneo yaliyoathirika bado yako kwenye hatari kutokana na mitetemo midogo zaidi ya 500 iliyofuata, pamoja na tishio la mvua kubwa.
- Umoja wa Mataifa umeanza maandalizi ya vituo vya msaada kwa familia zilizopoteza makazi na unasema hatua ya ujenzi na urejeshaji wa maisha itahitaji muda na ushirikiano wa karibu na mamlaka za Venezuela.
- Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono Venezuela wakati wa juhudi za uokoaji na ujenzi upya.