Dunia haiwezi tena kupuuza fursa na hatari zinazoletwa na teknolojia hiyo inayokua kwa kasi, amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani.

Ni baada ya Jopo la Kisayansi la Umoja wa Mataifa kuhusu akili mnemba au (AI) lililoundwa mwezi Februari mwaka huu kutoa hii leo ripoti yake ya awali.

Bofya hapa kusoma yaliyomo kwenye ripoti

Picha ya UN/Mark Garten Katibu Mkuu António Guterres akiwaeleza waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Awali ya Jopo Huru la Kisayansi la Kimataifa kuhusu Akili Mnemba.

Guterres amesema baada ya ripoti hiyo sasa ni jukumu la serikali kuchukua za pamoja za usimamizi wa AI kwani, “tunachofanya sasa ni jukumu letu sote.”

Ripoti hiyo, iliyoandaliwa na wataalamu huru 40 wa jopo hilo, imesambazwa kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa na pia kuwekwa wazi kwa umma kabla ya kufanyika kwa Mdahalo wa Kwanza wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde, utakaoanza wiki ijayo mjini Geneva.

Ahadi kubwa, lakini pia hatari halisi

Katibu Mkuu amewashukuru wajumbe wa jopo hilo kwa kazi yao, akieleza kuwa tathmini hiyo inatoa picha ya kweli kuhusu uwezo mkubwa wa akili mnemba pamoja na changamoto zinazoambatana nayo.

“Ripoti inaonesha dhahiri kwamba ikiwa itasimamiwa kwa uwajibikaji, akili mnemba inaweza kuwa nguvu kubwa zaidi ya kuchochea maendeleo, kwa kuharakisha mafanikio katika sekta za afya, elimu, usalama wa chakula na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kuwa kadri akili mnemba inavyoendelea bila kuwepo kwa kanuni za pamoja, ndivyo serikali na wananchi watakavyokuwa na sauti ndogo katika kuamua matokeo yake. Ujumbe wake kwa serikali, ni kwamba, “msisubiri.”

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Katibu Mkuu ameungana na wenyeviti wenza wa jopo hilo lenye wajumbe 40, Yoshua Bengio akijiunga kwa video kutoka Canada na Maria Ressa akijiunga kutoka Amsterdam, Uholanzi.

Kauli ya Guterres yamgusa Mwenyekiti Mwenza Ressa

Kwa Bi. Ressa mwandishi wa habari mbobezi raia wa Marekani kwenye asili ya Ufilipino, nukuu ya Katibu Mkuu kutoka kwenye ripoti ya kwamba “Hatuwezi tena kusema hatukujua,” ndio iliyobeba mazungumzo yake na waandishi wa habari akitanabaisha kuwa “angalau ukweli unaanza kuwekwa bayana.”

“Hii ni ripoti ya awali. Inawakilisha ushahidi bora zaidi unaopatikana kwa sasa katika nyanja inayobadilika kwa kasi zaidi kuliko ambavyo yeyote kati yetu anaweza kuandika kuihusu.”

Ameeleza kuwa takwimu walizoripoti zinahusu kipindi kinachoishia mwezi Mei. “Na katika nyanja hii, hata muda huo tayari unaonekana kuwa ni wa zamani kiasi. Ripoti hii inaeleza kwa uaminifu yale tunayoyajua, na pia inaeleza kwa uaminifu yale tusiyoyajua.”

Bi. Ressa ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2021, amesema ripoti iliandaliwa kwa namna ambayo inaweza kutumika kwa viwango viwili kwa wakati mmoja: kwa serikali, ambao ndio walengwa wetu wakuu, na kwa ninyi, umma, ambao hamko mbali kamwe katika mawazo yetu.”

Pengo la uwezo wa AI unaoimarika na kasi ndogo ya usimamizi – Bengio

Fursa ikawadia kwa Bengio, Profesa na mtaalamu wa sayansi ya kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Montreal nchini Canada, yeye akaangalia mbele zaidi akisema, “pengo kati ya uwezo wa AI unaoendelea kuimarika kwa kasi na mbinu madhubuti za kudhibiti hatari linaweza kusababisha matokeo ya maafa.”

© Unsplash/Aidin Geranrekab Akili Mnemba sasa inabadilisha sekta nyingi sana ikiwemo ya simu ya rununu.

Mathalani kasi ndogo ya ufuatiliaji wa changamoto zinazohusiana na usalama wa mtandao, lakini kampuni pia zina wasiwasi kuhusu hatari za kibayolojia, na mashirika mengi ya kiraia yanaonesha kuwa AI inaweza kusababisha upotoshaji wa taarifa ambao unaweza kutishia demokrasia na haki za msingi za binadamu.

Ushirikiano wa kimataifa ndio jawabu mujarabu

Halikadhalika, pengo la walio na AI na wasio nao akisema, “ninataka kurudi kwenye suala hili la ukiritimba wa AI. Kadri uwezo wa AI unavyoendelea kukua, iwapo utaendelea kukua kwa kasi hii, pengo kati ya wale wenye uwezo na rasilimali na wale wasio nao lina uwezekano mkubwa wa kuongezeka. Nami sidhani kama bado tumelitathmini kikamilifu suala hilo.”

Ametamatisha akisema, ili kufanikisha manufaa yote ambayo AI inaweza kutoa huku tukipunguza hatari zake, tunahitaji kushughulikia masuala haya yote. “Na hilo lazima lifanyike katika ngazi ya kimataifa, kwa sababu AI, na hasa matumizi yake mabaya kama vile mashambulizi ya mtandaoni, hayazuiliwi na mipaka ya nchi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *