
Taarifa iliyochapishwa leo Julai 1 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA inaeleza kwamba Timu ya Kibinadamu ya Nchi (HCT) katika Eneo la Palestina Linalokaliwa kimabavu na Israel, imesema vikosi vya Israel vimeendelea kutekeleza vizuizi vya kuingia katika maeneo hayo kwa kutumia nguvu za kuua, huku mashambulizi na mapigano pia yakiendelea kuripotiwa.
HCT ni chombo cha kimkakati kinachoongozwa na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Eneo la Palestina Linalokaliwa kimabavu na Israel, kikijumuisha mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kimataifa na ya Kipalestina yanayotoa huduma za kibinadamu.
Umoja wa Mataifa unasema kati ya Oktoba 10, 2025 na mwanzoni mwa Aprili 2026, ulithibitisha vifo vya Wapalestina 196, wakiwemo wanawake 18 na watoto 43, waliouawa katika mashambulizi ya Israel karibu na maeneo yaliyokuwa na vikosi vya Israel. Wengi wao waliripotiwa kuuawa walipokuwa wakipita katika maeneo ambayo mipaka yake haikuwa imewekwa wazi, huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Mashirika ya kibinadamu yamesema vikwazo vya usafiri vinaendelea kuchelewesha au kusimamisha shughuli za misaada ya dharura. Baadhi ya mashirika yamelazimika kupunguza au kusitisha kwa muda huduma muhimu, hasa baada ya wahudumu wa misaada kuuawa katika maeneo hayo, hali iliyoathiri maelfu ya familia.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa kuongezeka kwa maeneo yanayodhibitiwa kunapunguza nafasi salama kwa raia. Wapalestina wengi wa Gaza tayari wamekimbia makazi yao mara kadhaa na sasa wanaishi katika maeneo yenye msongamano mkubwa huku wakikabiliwa na ukosefu wa usalama. Wakati huo huo, upatikanaji wa huduma muhimu unaendelea kudorora kutokana na kiwango kidogo cha bidhaa za misaada kinachoruhusiwa kuingia Gaza.
Timu ya Kibinadamu ya Nchi, HCT imetoa wito wa:
- Kusitishwa mara moja kwa kulengwa kwa Wapalestina wanaokaribia maeneo yenye vikosi vya Israel.
- Kulindwa kwa raia wakati wote kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.
- Kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu kuingia na kusambazwa kwa usalama bila vikwazo katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza.