
Akilihutubia Baraza hilo linalokutana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa asubuhi hii ya Alhamis Julai 2 kwa saa za New York, Marekani, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ujenzi wa Amani na Msaada wa Amani, Elizabeth Spehar, ameonya kuwa kuongezeka kwa mapigano hayo kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa eneo hilo, amani na usalama wa kimataifa pamoja na uchumi wa dunia. Ameeleza kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yanayoandaliwa na Qatar mjini Doha yanaendelea, lakini akasisitiza kuwa hali bado ni tete.
Spehar ameeleza pia matukio ya hivi karibuni, yakiwemo mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara karibu na Mlango wa Hormuz, mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya Iran na mashambulizi ya Iran yaliyolenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait. Ametoa wito kwa pande zote kujizuia, kulinda raia na miundombinu ya kiraia, na kuunga mkono juhudi za kidiplomasia.
Mwakilishi wa Bahrain
Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Abdullatif bin Rashid Al Zayani, ameliambia Baraza kuwa nchi yake imekumbwa na mashambulizi zaidi ya 800 tangu mwishoni mwa Februari, yakiwemo makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani. Amesema mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya raia watatu, kujeruhi mamia ya wengine na kuharibu miundombinu ya kiraia, huku akikanusha madai ya Iran kwamba yalilenga maeneo ya kijeshi pekee.
Kikao cha Baraza la Usalama kinaendelea huku nchi nyingine wanachama zikitarajiwa kutoa kauli zao kuhusu hali ya usalama katika eneo la Ghuba.
Tutaendelea kukuarifu kadri mazungumzo yatakavyoendelea katika kikao hiki cha dharura.