Meya wa Manispaa ya Mjini Zanzibar, Mheshimiwa Mohamed Ibrahim Razalee, amewataka vijana, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati, kutumia fursa ya mafunzo ya ujasiriamali na uandaaji wa maandiko ya biashara ili kuongeza uwezo wao wa kupata mitaji na kukuza biashara zao.

Meya Razalee amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya kuwawezesha vijana kuendesha biashara zenye tija, huku yakiwajengea uwezo wa kuandaa maandiko ya biashara yanayokubalika na taasisi za kifedha pamoja na wadau wa maendeleo.

Ametoa kauli hiyo alipokutana na kupokea ujumbe kutoka kampuni ya CoProsperity Fund ofisini kwake, uliofika kumweleza kuhusu mpango wa kuendesha Mfululizo wa Semina za Biashara Ndogo Tanzania, unaolenga kuwajengea uwezo wajasiriamali wanaochipukia pamoja na wamiliki wa biashara ndogo na za kati nchini.

Kwa mujibu wa ujumbe uliowasilishwa kwa Meya huyo, mfululizo wa semina hizo utaanza jijini Dar es Salaam Julai 25 mwaka huu na baadaye kuendelea katika mikoa ya Zanzibar, Morogoro, Dodoma, Arusha na Mwanza.

Mafunzo hayo yatahusisha mada mbalimbali ikiwemo mbinu za kuongeza mauzo, usimamizi wa fedha na upatikanaji wa mitaji, sheria za biashara pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii katika kukuza biashara.

Aidha, washiriki watapata fursa ya kukutana na wataalamu wa biashara, taasisi za kifedha na wadau mbalimbali watakaowasaidia kupata maarifa na kujenga mitandao ya kibiashara.

Meya Razalee amepongeza hatua ya kuanzishwa kwa programu hiyo akieleza kuwa itaongeza uwezo wa vijana kujiajiri, kuanzisha biashara endelevu na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, ujumbe wa CoProsperity Fund umeeleza kuwa lengo la programu hiyo ni kuwajengea uwezo wajasiriamali kupitia mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha kuboresha biashara zao, kuongeza ushindani na kuzalisha ajira zaidi kwa jamii.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *