
Moshi/Dar. Mwaka 2019 ulikuwa mwanzo wa safari ngumu kwa Mwanaisha Bakari (26), mkazi wa Kilimani mjini Moshi. Badala ya kufurahia malezi ya mtoto wake Yasri Abdalla, alijikuta akipambana na maumivu ya kukataliwa na mume wake baada ya mtoto huyo kugundulika ana ulemavu.
Anasema maneno aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa mume wake yalimuumiza na hayajafutika akilini mwake.
“Akitoka kazini alikuwa ananiambia, ‘Niambie tu huyo mtoto ni wa nani? Huu ulemavu umetoka wapi?’ Si yeye peke yake, hata baadhi ya ndugu zake waliniambia nimezaa nuksi na walitaka niondoke kwenye familia yao,” anasimulia kwa sauti yenye utulivu, lakini inayobeba maumivu ya miaka mingi.
Swali hilo halikuulizwa mara moja, anasema lilikuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku baada ya mtoto wao, Yasri Abdalla, kugundulika kuwa na mtindio wa ubongo.
Kwa Mwanaisha, maumivu hayakuwa tu kumlea mtoto mwenye mahitaji maalumu. Maumivu makubwa zaidi yalikuwa kuona mwanaume ambaye walizaa naye mtoto akiamua kuugeuza ulemavu huo sababu ya kuvunja ndoa yao.
Shinikizo la maneno hayo lilimfanya aanze kuugua presha. Baada ya kutafakari, aliona kuendelea kubaki kwenye ndoa hiyo kungehatarisha maisha yake na ya mtoto wake.
“Nilimwambia kuliko nibaki nipate presha nife, bora niondoke. Nikachukua mwanangu na kuondoka.”
Alirejea kwa wazazi wake kwa muda mfupi. Baada ya miezi michache, alimweleza baba yake kuwa alikuwa amerudi mjini kuanza maisha mapya.
“Baba aliniuliza, ‘utaweza?’ Nikamjibu, nitaweza. Nitakachopata mimi na mwanangu tutakula.’ Nikarudi Moshi kupambana.”
Mwaka huohuo 2019, alianza kuhudhuria huduma za utengamao katika Kituo cha CCBRT Moshi baada ya kupewa ushauri kwamba mtoto wake hakupaswa kuendelea kukaa bila mazoezi maalumu.
Anavyopambana na maisha
Leo Mwanaisha anaishi Moshi akipambana na maisha kama mzazi pekee wa Yasri.
Amesomea ushonaji na anaweza kushona nguo mbalimbali, kusuka nywele na kutengeneza sabuni, lakini changamoto ya kumlea mtoto mwenye ulemavu bado imekuwa ikivuruga hata fursa za ajira.
“Unaweza ukaajiriwa leo, kesho unapigiwa simu mtoto anaumwa au amelazwa hospitalini. Ukirudi kazini unaambiwa nafasi yako imechukuliwa. Hivyo ndivyo maisha yalivyo.”
Anasema kuna nyakati alikosa hata uwezo wa kuendelea na mazoezi ya mtoto kutokana na ugumu wa maisha.
Licha ya yote, jambo moja limebadilika ndani yake.
“Mwanzoni nilikuwa sijiamini. Nilimwangalia mwanangu kwa huzuni. Lakini baada ya baba yake kuondoka ndipo nilipopata ujasiri wa kumpenda zaidi. Leo najivunia kuwa mama yake.”
Anasema Yasri amemfundisha kuvumilia, kupambana na kuamini kuwa ulemavu hauondoi utu wa mtoto.
“Nimejifunza kwamba watoto wenye ulemavu ni watu kama watu wengine. Wanahitaji kupendwa na kupewa nafasi.”
Lakini simulizi ya Mwanaisha si ya kipekee. Rosen Kiwelu, mwenye umri wa miaka 39, naye anakumbuka siku alipojifungua mtoto wake, Michael Leonardo, ambaye alichelewa kulia baada ya kuzaliwa.
Mwanzoni hakujua tatizo ni nini. Alianza kushangaa mtoto hakukaza shingo, hakukaa wala hakufikia hatua za ukuaji kama watoto wengine. Alipofika CCBRT akiwa na mtoto wa miezi saba ndipo alielezwa kuwa mtoto anahitaji mazoezi maalumu ya utengamao.
Hata hivyo, anasema safari haikuwa rahisi. Kutokana na hali ngumu ya uchumi, alilazimika kusitisha huduma kwa kipindi kirefu ili kutafuta riziki.
“Nilikuwa nafanya biashara ndogo ndogo. Ukifunga biashara ili umhudumie mtoto, familia nzima inaathirika. Ikabidi nisimame kwa muda.”
Mbali na changamoto za kiuchumi, naye anakiri ndoa yake ilitikiswa.
Anasema kulikuwa na vipindi ambavyo mume wake alikuwa karibu na familia, lakini wakati mwingine alijitenga kabisa kiasi cha kumlazimu kurudi kwa wazazi wake kwa miaka mitatu kabla ya kurejea tena kuendelea na maisha ya ndoa.
“Hizi changamoto zipo. Lakini nikajifunza kutokata tamaa.”
Leo anaamini mazoezi aliyopata mwanawe kupitia CCBRT yamebadili afya yake na kumpa matumaini mapya.
Kwa mujibu wa Mhudumu wa Afya ngazi ya jamii wa CCBRT Moshi, Eltruda Materu simulizi kama za Mwanaisha na Rosen zimekuwa zikijirudia kwa miaka mingi.
Anasema tangu aanze kutoa huduma za utengamao mwaka 1996, ameshuhudia watoto wengi wakibadilika na kuwa watu wazima wanaojitegemea baada ya kupata huduma mapema.
Lakini anasema changamoto kubwa haipo kwa watoto pekee.
“Mara nyingi tunakutana na kina mama waliotelekezwa na waume zao baada ya mtoto kuzaliwa na ulemavu,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, CCBRT imekuwa ikiwajumuisha baba na mama katika elimu kuhusu chanzo cha ulemavu, ili kuondoa dhana kwamba mtoto amelaaniwa au amerogwa.
Aidha, kituo hicho hutoa ushauri wa kisaikolojia kwa wazazi huku kikisaidia kuwaunganisha kwenye vikundi vya kuweka na kukopa ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Materu anasema bado kuna changamoto kubwa ya imani potofu katika jamii.
“Wapo wanaoamini mtoto amerogwa au familia imelaaniwa. Tunatumia muda mwingi kuelimisha jamii kwamba mara nyingi hali hizi zinahusiana na changamoto zinazoweza kutokea wakati wa ujauzito au kujifungua.”
Anasema pamoja na changamoto hizo, jambo linalompa nguvu ni kuona watoto aliowahi kuwahudumia zaidi ya miaka 20 iliyopita leo wakiwa watu wazima.
“Wengine wamekwenda shule, wamehitimu, wanafanya biashara, ufugaji, wengine wameajiriwa. Hiyo ndiyo furaha yetu.”
Kwa Mwanaisha, mafanikio hayo ndiyo anayoyaota kwa mwanaye Yasri. Anasema hana ndoto kubwa ya utajiri isipokuwa mwanawe kuimarika.
Anachohitaji ni mtaji mdogo utakaomwezesha kuendesha biashara yake bila kumwacha mwanawe nyuma.
“Nikipewa mtaji wa kufanya biashara nitahakikisha mwanangu hapungukiwi na mahitaji yake.”
Anapotafakari miaka aliyopitia, hasikiki kama mwanamke aliyeshindwa na maisha.
Badala yake, anatoa ushauri kwa wazazi wanaojikuta katika hali kama aliyopitia.
“Hakuna anayependa kupata mtoto mwenye ulemavu. Lakini akishazaliwa, ukubaliane na hali. Mtoto hakuchagua kuzaliwa hivyo. Mungu ametupa jukumu la kuwapenda na kuwapigania.”
Anasema hata kama siku moja akipata mtoto mwingine, upendo wake kwa Yasri hautabadilika.
“Yasri amenifanya kuwa jasiri. Amenifundisha kupambana. Amenifanya nijue kwamba mama anaweza kuwa baba pia,” ni maneno ya Mwanaisha yanayobeba uzito, lawama na mapambano, lakini pia ushuhuda.