RAIS wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Julai 2 hadi 4, 2026. Rais Chapo alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Mahmoud Thabit Kombo, akishirikiana na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Akiwa nchini, Rais Chapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, yatakayofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Mbali na mazungumzo hayo, Rais Chapo anatarajiwa kufungua rasmi Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF). Pia atamtembelea Mama Maria Nyerere kwa ajili ya kumsalimia, kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ubalozi wa Msumbiji jijini Dar es Salaam.
SOMA: Rais wa Msumbiji kuwasili leo Dar
Hii ni mara ya tatu tangu Rais Chapo alipoingia madarakani mwaka 2025, ikiwa ni ishara ya dhamira ya viongozi wa Tanzania na Msumbiji ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kirafiki, undugu na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili. Ziara hii itafungua fursa mpya za ushirikiano katika nyanja mbalimbali, kwa kuzingatia historia ya muda mrefu ya ujirani mwema na mshikamano kati ya nchi hizo.
