
Dar es Salaam. Kuna wakati mafanikio ya taifa hayapimwi tu kwa maneno, bali kwa ushahidi wa kazi inayogusa maisha ya wananchi kila siku, hii ndiyo maana ushindi wa Tanzania katika sekta ya miundombinu sasa umeendelea kuvuta hisia ndani na nje ya nchi, baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kutunukiwa tuzo ya juu kabisa ya Afrika Mashariki kama taasisi bora ya huduma za umma katika sekta ya barabara.
Akizungumza leo Julai 2, 2026 katika makao makuu ya Tanroads, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Mohamed Besta amesema tuzo hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa za Serikali ambayo imeendelea kuwekeza kwa kasi katika ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara nchini.
“Mafanikio haya si ya Tanroads pekee bali ni ya Watanzania wote, kwani yanatokana na kazi ya pamoja ya serikali, wataalam na wadau mbalimbali wanaohakikisha barabara zinajengwa na kuboreshwa ili kuimarisha uchumi na usafirishaji wa bidhaa na huduma,”amesema Besta.
Tuzo hiyo ilitolewa katika Tuzo za Huduma za Umma Afrika Mashariki 2026 zilizofanyika Juni 30 katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, zikihusisha taasisi za umma kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda. Hafla hiyo ilileta pamoja viongozi wa serikali, mabalozi na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza Juni 30, 2026 katika hafla hiyo, Mwenyekiti na mwenyeji wa tuzo hizo, Steven Mkomwa, alisema tuzo hizo zimekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uwajibikaji, ubunifu na ubora katika utoaji wa huduma za umma.
“Tuzo hizi zilianza Tanzania kama mpango wa kitaifa wa kutambua taasisi bora za umma, kabla ya kupanuka na kufikia Afrika Mashariki kwa lengo la kusherehekea ubora wa kikanda katika huduma za umma. Kufuatia mafanikio na athari inayoongezeka ya jukwaa hilo, EAPSA sasa inaweka mkakati wa kujitanua kimataifa, ikiwa na mpango wa kutambua na kuunganisha taasisi bora za huduma za umma duniani kote,”alisema Mkomwa.
Hata hivyo, Besta amesema katia tuzo hizo Tanroads imetambuliwa kuwa mshindi wa jumla Afrika Mashariki kutokana na mchango wake katika kuendeleza miundombinu ya barabara, kuunganisha maeneo ya ndani na mipaka ya kimkakati, kuboresha usafirishaji na kuchochea ukuaji wa biashara ndani na nje ya nchi.
Amesema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya utawala bora ndani ya taasisi za umma, uwajibikaji pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya Tanroads sekta binafsi kupitia mfumo wa ubia (PPP), ambao umeongeza kasi ya upatikanaji wa mitaji ya miradi ya barabara.
“Tanzania inaendelea kupanua mtandao wake wa barabara kupitia miradi mbalimbali inayoendelea nchini kote, huku serikali ikiendelea kutenga rasilimali kwa ajili ya matengenezo makubwa ya miundombinu ili kuhakikisha ubora unadumu licha ya changamoto za mvua na matumizi makubwa ya barabara,”amesema.
Aidha, amesema uzoefu wa nchi zinazoendelea kama Singapore, Malaysia, Indonesia na Philippines unaonesha mafanikio ya kutumia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP), mfumo ambao Tanzania nao inaendelea kuutumia kwa kasi.
Amesema Tanroads itaendelea kuboresha huduma zake na kuhakikisha Watanzania wanapata miundombinu bora zaidi, akisisitiza kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza bidii, uwajibikaji na ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya barabara nchini.