
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu, OCHA, watu wasiopungua 18 wamefariki dunia katika mji mkuu huo, ambako maeneo yenye wakazi wengi yameharibika sana na wakazi wengi yameharibika kwa kiwango kikubwa na wakazi kwenye baadhi ya mitaa ya mji huo wamehamishwa.
“Usiku wa kuamkia leo, wakazi wengi kati ya takribani milioni tatu wa mji wa Kyiv, pamoja na maelfu ya wengine katika maeneo ya jirani, walitumia hadi saa 11 katika makazi ya kujikinga dhidi ya mabomu au wakijificha majumbani mwao huku wakisikiliza sauti za kutisha za vita.” Mwakilishiw a Umoja wa Mataifa nchini Ukraine ambaye pia ni Mkuu wa OCHA nchini humo, Matthias Schmale amesema kupitia taarifa yake ya kulaani mashambulizi hayo.
Ameongeza kwamba, “operesheni za utafutaji na uokoaji zinaendelea ili kuwaokoa watu waliokwama chini ya vifusi vya majengo ya makazi yaliyoporomoka, wakiwemo msichana mwenye umri wa miaka 15 pamoja na familia yake.”
Mbali na waliouawa mjini Kyiv, karibu watu 90 wamejeruhiwa, wakiwemo watoto kadhaa, katika kile ambacho meya wa jiji hilo amekieleza kuwa “shambulio kubwa zaidi kuwahi kutokea”, huku vyombo vya habari vya kitaifa vikieleza kuwa majengo ya makazi na hoteli yaliteketezwa kwa moto.
Wahudumu wa afya waathirika
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni wahudumu wa afya na madereva wa gari za wagonjwa baada ya kituo cha gari hizo kushambuliwa na magari kadhaa kuharibika.
Bwana Schmale amesema karibu kila sehemu ya mji mkuu imeathirika, huku nyumba nyingi, hoteli, soko na miundombinu mingine ya kiraia ikiharibiwa au kuathiriwa.
Kwa mujibu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Binadamu nchini Ukraine, kati ya Desemba 2025 na Mei 2026, idadi ya raia waliouawa au kujeruhiwa iliongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka mmoja uliopita.
Mlolongo wa mashambulizi unaoendelea
“Raia wa Kyiv na kote nchini hawapaswi kuishi kwa hofu wakisubiri shambulio lingine; wanalindwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu,” amesisitiza Bwana Schmale.
Ameeleza kuwa mashambulizi ya karibuni dhidi ya maeneo yenye wakazi wengi nchini Ukraine ni sehemu ya “mlolongo unaoendelea wa mashambulizi ya mauti.” Wakati huo huo, nchini Urusi na katika eneo la Crimea la Ukraine linalokaliwa na Urusi, ongezeko la mashambulizi ya makundi ya ndege zisizo na rubani, ambayo vyombo vya habari vinayahusisha na vikosi vya Ukraine, yamesababisha usumbufu mkubwa katika miundombinu ya mafuta na kufungwa kwa viwanja vya ndege vya Moscow.
Kote nchini Ukraine, mashirika ya misaada yanatoa msaada wa dharura kwa karibu watu milioni moja walioathiriwa na mashambulizi ya Urusi tangu uvamizi wake kamili ulipoanza tarehe 24 Februari 2022.
Misaada hiyo muhimu inajumuisha huduma ya kwanza, malazi ya dharura, ulinzi, msaada wa fedha taslimu na huduma za afya ya akili, athari kubwa lakini ambazo mara nyingi hazionekani za vita hivyo.
“Maumivu ya kupoteza wapendwa na hofu inayosababishwa na shambulio hili pamoja na mengine yote huongeza athari za kisaikolojia ambazo watu wengi wanalazimika kuishi nazo,” amesema Bwana Schmale. “Kadri vita vinavyoendelea, ndivyo makovu haya yasiyoonekana yanavyozidi kuwa makubwa.”