Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema leo kote nchini Algeria kwa ajili ya uchaguzi wa pili wa Bunge tangu baada ya maandamano makubwa mwaka 2019 yaliyopelekea kujiuzulu Rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika.

Televisheni ya taifa ya Algeria imetangaza kuwa vituo vya kupigia kura vilikuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi kwa saa za huko katika mikoa yote 69 ya nchi hiyo huku upigaji kura ukitarajiwa kuendelea hadi saa moja jioni hii leo.

Picha za televisheni zimeonyesha wananchi wa Algeria wakishiriki katika zoezi la upigaji kura katika majimbo ya kusini-magharibi ya Tindouf na Bechar, pamoja na jimbo la mpakani la Tebessa mashariki mwa nchi hiyo.

Zaidi ya wapiga kura milioni 24 wanashiriki katika uchaguzi wa leo ili kuwachagua wawakilishi wa Bunge la Taifa la Wananchi lenye viti 407 katika uchaguzi wa pili wa Bunge kufanyika Algeria tangu kujiri  maandamano makubwa mwaka 2019.

Uchaguzi wa Bunge la Taifa la Algeria unajumuisha vita 12 vilivyotengwa kwa ajili ya Waalgeria wanaoishi nje ya nchi.

Maandamano ya miezi kadhaa ya mwaka 2019, yaliyojulikana kama harakati za Hirak, yalihitimisha utawala wa miaka 20 wa Rais Bouteflika

Itakumbukwa kuwa kabla ya kujiuzulu Rais Abdelaziz Bouteflika mwaka 2019, jeshi la Algeria lilikuwa limemtaka kiongozi huyo atangaze kwamba hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi. Bouteflika wakati huo alikuwa na umri wa miaka 82 akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *