Dar es Salaam. Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umewahalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwasilisha maombi ya kuonesha nia ya kuendeleza viwanja 38 vinavyomilikiwa na Serikali kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuharakisha maendeleo ya miradi ya kibiashara ya majengo nchini.

Kupitia tangazo la kuomba maombi ya kuonesha nia ya uwekezaji (Expression of Interest – EOI), TBA imesema fursa hizo zinahusisha maeneo yaliyopo katika mikoa 20 na zinajumuisha miradi ya makazi, biashara, matumizi mchanganyiko, vituo vya usafirishaji na ugavi (logistics), pamoja na huduma za malazi na utalii.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, wakala huo unatafuta wawekezaji wenye sifa, uwezo wa kifedha na kiufundi, pamoja na rekodi nzuri ya utekelezaji wa miradi, watakaoshirikiana na TBA kuendeleza maeneo hayo.

Hatua hiyo inafuatia kufanyika kwa marekebisho ya Amri ya Kuanzishwa kwa TBA yaliyofanyika Agosti mwaka 2023, yaliyopanua majukumu ya wakala huo na kuuruhusu kufanya shughuli za maendeleo ya miradi ya majengo kwa misingi ya kibiashara.

TBA ilieleza kuwa ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 ikiwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya majengo ya Serikali, kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu pamoja na kusimamia ujenzi na matengenezo ya majengo ya Serikali.

Miongoni mwa maeneo makubwa yaliyotangazwa ni ekari 630 zilizopo Nzuguni, jijini Dodoma, zinazotarajiwa kuendelezwa kwa matumizi ya biashara na makazi.

Maeneo mengine muhimu yapo Masaki, Oysterbay, Magomeni na Pugu jijini Dar es Salaam, pamoja na mikoa ya Arusha, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Kigoma, Geita, Tabora, Kagera, Songwe, Simiyu na mingine.

Miradi iliyopangwa kutekelezwa inajumuisha ujenzi wa makazi, nyumba za ghorofa, majengo ya biashara, vituo vya ugavi na usafirishaji, hoteli pamoja na majengo ya matumizi mchanganyiko.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *