Chanzo cha picha, Wizara ya Afya Tanzania
Tanzania na Marekani zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya afya yenye thamani ya dola bilioni 3.1 za Marekani.
Makubaliano hayo ni sehemu ya mpango wa Marekani unaojulikana kama America First Global Health Strategy, unaolenga kuimarisha ushirikiano wa afya duniani kupitia uwekezaji katika mifumo ya afya na uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Mipango kama hiyo imekuwa ikikumbwa na upinzani katika baadhi ya nchi za Afrika, kutokana na hofu kuhusu matumizi ya taarifa binafsi za kiafya na uwezekano wa kuhusishwa na maslahi mengine, ikiwemo sekta ya madini.
Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Tanzania amesema makubaliano hayo hayatahusisha kupelekwa kwa sampuli za maabara nchini Marekani kwa ajili ya uchunguzi.
Katika mpango huo, Nigeria inaongoza kwa thamani ya makubaliano ya dola bilioni 5.1, ikifuatiwa na Tanzania kwa dola bilioni 3.1.
Kati ya fedha hizo, Marekani inatarajiwa kuchangia dola bilioni 1.3, iwapo fedha hizo zitapitishwa na Bunge la Marekani, huku Tanzania ikichangia dola bilioni 1.8 katika kipindi cha miaka mitano.
Makubaliano hayo pia yanalenga kuendeleza na kudumisha mtandao wa maabara uliounganishwa na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja katika ngazi mbalimbali za mfumo wa afya, ili kuimarisha uwezo wa kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa kuzingatia viwango vya mfumo wa 7-1-7.
Kwa mujibu wa mfumo huo, mlipuko unaoshukiwa unapaswa kugunduliwa ndani ya siku saba, kuripotiwa kwa mamlaka za afya ya umma ndani ya siku moja, na hatua madhubuti za kukabiliana nao kuchukuliwa ndani ya siku saba.
Chanzo cha picha, Wizara ya Afya Tanzania
Marekani inasema lengo ni kusaidia nchi kama Tanzania kujenga mifumo ya afya inayojitegemea kwa kuongeza uwekezaji wa ndani.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa afya ya umma na sheria za kimataifa wanasema baadhi ya makubaliano ya aina hii katika nchi nyingine za Afrika yameibua mjadala kuhusu ulinzi wa taarifa za afya, usimamizi wa sampuli za maabara na mamlaka ya nchi katika kusimamia rasilimali zake za kisayansi.
Kwa sasa, utekelezaji wa makubaliano haya ndio utakaobainisha mafanikio yake.
Swali litakuwa si tu kama yataongeza fedha za sekta ya afya, bali pia kama yataimarisha uwezo wa Tanzania kujitegemea, kulinda taarifa za afya za wananchi na kuhakikisha ushirikiano huu unawanufaisha Watanzania kwa muda mrefu.
Sio Tanzania pekee imetia saini na Marekani, pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Marekani zimekubaliana kuhusu ushirikiano wa kimkakati wa afya wenye thamani ya dola bilioni 1.2, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na serikali hizo mbili.
Ushirikiano huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka sita, kuanzia 2026 hadi 2031, Reuters imeripoti
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makubaliano hayo yanajumuisha:
Dola milioni 900 za msaada wa moja kwa moja kutoka serikali ya Marekani kwa ajili ya sekta ya afya; na
Dola milioni 300 ambazo serikali ya DRC itaongeza hatua kwa hatua katika bajeti yake ya matumizi ya afya ndani ya kipindi hicho.
Lengo la ushirikiano huo ni kuimarisha huduma za afya nchini DRC kupitia ufadhili wa pamoja kati ya serikali ya Marekani na serikali ya DRC katika kipindi cha miaka sita ijayo.
Takribani nchi 24 za Afrika zimesaini makubaliano yenye utata ya ushirikiano wa afya na Marekani chini ya mkakati mpya wa misaada wa Rais Donald Trump, huku baadhi ya nchi zikiyakataa.
Wanaounga mkono makubaliano hayo wanasema yanazipa serikali za Afrika mamlaka makubwa zaidi ya kusimamia mifumo yao ya afya na kutumia misaada kwa uwazi zaidi.
Hata hivyo, wakosoaji wanaibua maswali kuhusu uwajibikaji, ulinzi wa taarifa binafsi za afya (data), na iwapo Marekani itaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika sekta ya afya za nchi hizo kupitia makubaliano hayo.
Chanzo cha picha, GETTY
1. Kenya
Mwezi Desemba, Mahakama Kuu Kenya ilisimamisha kwa muda utekelezaji wa makubaliano kama hayo ya ufadhili wa afya yaliyokuwa yamesainiwa kati ya serikali ya Kenya na Marekani, baada ya Consumers Federation of Kenya kufungua kesi ikieleza wasiwasi kuhusu usalama wa taarifa za afya za Wakenya.
Mfumo wa ushirikiano wa afya kati ya Kenya na Marekani ulitiwa saini tarehe 4 Desemba 2025.
Jaji Chacha Mwita wa Mahakama Kuu ya Milimani alitoa amri za muda akizuia utekelezaji wa makubaliano hayo kwa ujumla wake hadi kesi iliyowasilishwa kupinga uhalali wake itakaposikilizwa na kuamuliwa. The Citizen la nchini humo liliripoti.
Uamuzi huo ulitolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Kaunti ya Busia Okiya Omtatah, ambaye alidai kuwa mfumo huo wa ushirikiano ulisainiwa bila ushirikishwaji wa umma wala kupata idhini ya Bunge.
Pia alieleza wasiwasi kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi , uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma, na athari zinazoweza kujitokeza kwa haki ya Wakenya ya kupata huduma za afya kwa usawa.
“Amri zilizotolewa katika kesi hii zinahusu masuala mbalimbali yanayogusa mamlaka na uhuru wa Jamhuri, kanuni za usimamizi wa fedha za umma, nafasi ya serikali za kaunti, ukuu wa Katiba, pamoja na uhamishaji wa taarifa (data),” alisema Okiya Omtatah.
“Hoja yetu ni kwamba taarifa binafsi ni mali ya mtu binafsi, si ya Serikali. Haziwezi kukusanywa, kuunganishwa wala kubadilishwa bila idhini ya wazi kutoka kwa mhusika anayehusika na taarifa hizo.”
Mahakama Kuu pia ilikuwa imetoa awali amri za muda kwa upande mmoja (ex parte) za kusitisha utekelezaji wa makubaliano hayo baada ya Consumers Federation of Kenya (COFEK) kudai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria katika uhamishaji, ushirikishaji au usambazaji wa taarifa za kitabibu, taarifa za magonjwa ya mlipuko (epidemiolojia), pamoja na taarifa nyingine nyeti za afya za watu binafsi, Citizen iliripoti.
2. Zimbabwe
Zimbabwe imekataa makubaliano ya afya na Marekani ambayo yangetoa ufadhili wa dola za Marekani milioni 367 kwa kipindi cha miaka mitano, kutokana na sharti la Washington la kutaka kupata taarifa nyeti za kiafya.
Uamuzi huo umebainika baada ya waraka wa serikali wa mwezi Desemba kuvuja, ukionesha kuwa Rais Emmerson Mnangagwa aliona makubaliano hayo kuwa hayakuwa ya haki kwa pande zote.
Msemaji wa serikali baadaye alieleza kuwa Marekani ilikuwa ikitaka kupata sampuli za kibaiolojia kwa ajili ya utafiti na manufaa ya kibiashara, lakini haikuwa tayari kushirikisha Zimbabwe faida zitakazotokana na chanjo au tiba zitakazotengenezwa baadaye.
“Sasa tutalazimika kuanza mchakato mgumu na wa kusikitisha wa kusitisha msaada wetu wa sekta ya afya nchini Zimbabwe,” alisema Pamela Tremont katika taarifa yake.
Ubalozi wa Marekani ulisema kuwa Marekani imetoa zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.9 kwa ufadhili wa sekta ya afya nchini Zimbabwe katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Chama cha madaktari nchini Zimbabwe kimeitaka serikali na Marekani kuendelea na mazungumzo ili kufikia makubaliano yatakayokubalika kwa pande zote mbili, ili programu ya nchi hiyo ya kupambana na Virusi vya Ukimwi iendelee bila kuvurugika.
Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu kurejea madarakani mwaka jana, Rais wa Marekani Donald Trump amepunguza kwa kiasi kikubwa misaada ya kigeni na kulifunga United States Agency for International Development.
Shirika hilo lilikuwa likisimamia utoaji wa misaada kwa niaba ya serikali ya Marekani. Hata hivyo, Trump alidai kuwa matumizi yake yalikuwa ya ubadhirifu, na kwamba utawala wake ulikuwa ukihamasisha makubaliano ya moja kwa moja kati ya serikali na serikali ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa Ubalozi wa Marekani nchini Zimbabwe, hadi sasa nchi 16 za Afrika zimesaini mikataba ya ushirikiano wa afya yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 18.3 za ufadhili mpya.
Ubalozi huo ulisema fedha zilizokusudiwa Zimbabwe zingeelekezwa katika:
- Matibabu na kinga dhidi ya Maambukizi ya HIV
- Kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu
- Kudhibiti Malaria;
- Kuboresha afya ya mama na mtoto; na
- Kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
“Tunaamini ushirikiano huu ungeleta manufaa makubwa kwa jamii za Zimbabwe, hasa kwa wanaume, wanawake na watoto milioni 1.2 ambao kwa sasa wanapata matibabu ya HIV kupitia programu zinazoungwa mkono na Marekani,” alisema Pamela Tremont.
Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Zimbabwe, Nick Mangwana, alisema mpango huo haukuwa wa usawa kati ya pande mbili.
“Zimbabwe iliombwa kushiriki rasilimali zake za kibaiolojia na taarifa zake kwa kipindi kirefu, bila kuwa na dhamana yoyote ya kupata ubunifu wowote wa kitabibukama vile chanjo, vifaa vya uchunguzi au tiba, ambavyo vinaweza kutengenezwa kutokana na taarifa hizo zilizotolewa,” ilisema taarifa yake.
“Kwa maana halisi, taifa letu lingekuwa linatoa malighafi za ugunduzi wa kisayansi bila uhakika wowote kwamba bidhaa za mwisho zingepatikana kwa wananchi wetu iwapo kutatokea janga jingine la kiafya siku zijazo.”
3. Zambia
Chanzo cha picha, Getty Images
Zambia imepinga sehemu ya makubaliano ya msaada wa afya wa zaidi ya dola bilioni 1 kutoka Marekani, ikisema kuwa baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo haviendani na maslahi ya taifa, serikali ilisema mwezi Februari mwaka huu, Reuters liliripoti.
Wakati huohuo, watetezi wa masuala ya afya wameonya kuwa makubaliano hayo yanaweza kuhusisha utoaji wa fedha hizo na upatikanaji wa rasilimali za madini, pamoja na kuwa na hatari zinazohusiana na ushirikishaji wa taarifa binafsi.
Makubaliano hayo yanahusu zaidi ya dola bilioni 1 za ufadhili kutoka Marekani kwa kipindi cha miaka mitano, zikiwa zinalenga kupambana na magonjwa kama HIV na Malaria, kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa, pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto.
Aidha, rasimu ya makubaliano iliyopitiwa na Reuters inaonesha kuwa serikali ya Zambia ingetakiwa kuchangia takribani dola milioni 340 katika kipindi hicho hicho cha miaka mitano kama sehemu ya ufadhili wa pamoja.
Makubaliano hayo yalitarajiwa kutiwa saini mwezi Novemba, lakini yalicheleweshwa baada ya rasimu zilizofanyiwa marekebisho kujumuisha kipengele kilichoonekana kuwa na utata na kisichokubalika, kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Afya nchini humo ambaye aliliambia shirika la Reuters.
“Kipengele hicho hakikuwa kinaendana na msimamo na maslahi ya Serikali ya Zambia… Kwa hiyo, tumeomba kifanyiwe marekebisho zaidi kuhusu maudhui yanayohusika,” alisema msemaji huyo.
Hata hivyo, alikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu maudhui ya kipengele hicho au kueleza hasa kilihusu nini.
Imehaririwa na Mariam Mjahid