
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya, (WHO) Dkt. Tedros Ghebreyesus, ametangaza kumalizika kwa mlipuko wa hivi karibuni wa virusi vya Hanta huku akionya kuwa milipuko ya Ebola na virusi vya Marburg bado unaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma.
Amesema hayo Alhamisi huko Geneva, Uswisi alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa masuala ya magonjwa duniani huku pia akizungumza umuhimu wa kulinda vijana dhidi ya madhara ya matumizi holela ya mitando ya kijamii.
Virusi vya Hanta
Mlipuko huo uliotangazwa rasmi kutokomezwa unahusishwa na meli ya kitalii MV Hondius, baada ya mtu wa mwisho aliyekuwa amekutana na mgonjwa kukamilisha kipindi cha ufuatiliaji na kupimwa kuwa hana maambukizi. Hakujakuweko na mgonjwa mpya tangu Mei 25.
Jumla ya watu 13 walithibitishwa kuambukizwa, wakiwemo watatu waliofariki dunia. Zaidi ya watu 650 waliokuwa wamekutana na wagonjwa walifuatiliwa katika nchi na maeneo 33.
Dkt. Tedros amesema WHO itaendelea na utafiti unaohusisha nchi 21 ili kuboresha vipimo vya utambuzi, matibabu na maendeleo ya chanjo dhidi ya hantavirus kwa milipuko ya baadaye.
Mlipuko wa Ebola washamiri DRC- Wagonjwa wapya 38 kila siku
Akizungumzia Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) Dkt. Tedros amesema ugonjwa unaendelea kuongezeka, huku wastani wa wagonjwa wapya 38 wakithibitishwa kila siku katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Hadi sasa, nchi hiyo imethibitisha wagonjwa 1,406 wa Ebola na vifo 438. WHO imeongeza uwezo wa maabara za kupima ugonjwa huo, vituo vya matibabu na ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa. Pia, majaribio ya kitabibu ya dawa mbili zinazotarajiwa kutibu Ebola yameanza.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa WHO ameonesha wasiwasi kuhusu mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya baada ya kituo cha matibabu ya Ebola katika jimbo la Ituri kushambuliwa na kuchomwa moto, hali iliyovuruga juhudi za kudhibiti mlipuko huo.
Uganda yathibitisha mgonjwa wa virusi vya Marburg
Wakati Uganda haijaripoti mgonjwa mpya wa Ebola tangu Juni 21, WHO imethibitisha kuwepo kwa mgonjwa mmoja wa virusi vya Marburg katika Wilaya ya Kyegegwa, magharibi mwa nchi hiyo.
Dkt. Tedros amesema mgonjwa huyo aligunduliwa kupitia mfumo ulioimarishwa wa ufuatiliaji wa Ebola.
“Mamlaka za afya zinaendelea kuwafuatilia watu wote waliokutana na mgonjwa huyo, huku hadi sasa hakuna maambukizi mapya yaliyoripotiwa. WHO inaendelea kusaidia uchunguzi wa chanzo cha maambukizi na shughuli za uhamasishaji wa jamii,” amesema Dkt. Tedros.
WHO yataka mitandao ya kijamii iwe salama kwa vijana
Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amezungumzia pia tahariri ya pamoja waliyochapisha na Rais wa Ufaransa, Emmanuel kuhusu madhara ya mitandao ya kijamii kwa vijana.
Katika tahariri hiyo wameonya kuhusu kuongezeka kwa madhara ya mitandao ya kijamii na mazingira ya kidijitali kwa afya ya watoto na vijana.
“Uenezaji wa maudhui yanayolenga kuongeza muda wa matumizi badala ya usahihi wa taarifa vinachangia kusambaa kwa taarifa potofu. Aidha, huduma kama kusogeza maudhui bila ukomo, uchezaji wa video kiotomatiki na maudhui yanayopendekezwa kulingana na mtumiaji vinaweza kuchochea uraibu wa matumizi ya mitandao ya kijamii,” amesema.
Watoto si wa kufanyiwa majaribio
Halikadhalika, watoto wanaokumbana mara kwa mara na maudhui yenye vurugu, ubaguzi au yanayowajengea taswira zisizo halisi wanaweza kuathirika kisaikolojia na kupoteza kujiamini.
Dkt. Tedros ametaka kuwepo kwa sheria madhubuti zaidi, mifumo salama ya kidijitali inayozingatia umri wa watoto, pamoja na uwajibikaji mkubwa kutoka kwa kampuni za teknolojia.
“Watoto si watu wa kufanyiwa majaribio, si soko lililofungwa wala bidhaa ya kibiashara, bali ni mustakabali unaopaswa kulindwa.”