
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Marekani zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya (MoU) kwa miaka mitano, yenye thamani ya Dola 3.14 bilioni za Marekani (Sh8.164 trilioni) huku maeneo matano ya vipaumbele yakiainishwa.
Maeneo yatakayokuwa msingi wa utekelezaji wake katika ushirikiano huo ni pamoja na kuwaingiza watumishi wa afya wanaofadhiliwa na nchi hiyo katika mfumo wa ajira wa Serikali.
Pia, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na uwezo wa kukabiliana na milipuko, kuimarisha mifumo ya maabara, kuongeza umiliki wa Tanzania katika ununuzi wa bidhaa za afya pamoja na kuendeleza mifumo jumuishi ya kidijitali ya taarifa za afya.
Maeneo hayo yametajwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Jeanne Clark jana Jumatano, Julai Mosi 2026 katika hotuba yake, mara baada ya kutiliana saini ya Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano huo.
Makubaliano hayo, yaliyosainiwa chini ya Mkakati wa Afya Duniani wa Utawala wa Trump wa America First Global Health Strategy, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa aliwakilisha ujumbe wa Tanzania.
Clark amesema makubaliano hayo yanaashiria mwanzo wa sura mpya ya ushirikiano unaojengwa katika misingi ya uwajibikaji wa pamoja, uwekezaji na manufaa badala ya utegemezi wa misaada.
Amesema Marekani imekusudia kuwekeza takribani Dola 1.34 bilioni (Sh3.48 trilioni) huku Tanzania ikichangia Dola 1. bilioni 8 (Sh4.68 trilioni) katika kipindi chote cha utekelezaji wa makubaliano hayo.
Clark amesema eneo la kwanza litahusu kuimarisha mfumo wa kitaifa wa kugundua, kuripoti na kukabiliana kwa haraka na milipuko ya magonjwa kabla haijawa janga la kitaifa au kikanda.
Eneo la pili litajikita katika kuimarisha maabara kwa kuboresha mitandao ya uchunguzi wa magonjwa, kuongeza uwezo wa vipimo na kuhakikisha maabara zinatoa huduma za kawaida na za dharura kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Clark amesema eneo la tatu ni mpito wa Tanzania kuchukua jukumu kubwa la kugharamia bidhaa za afya.
Amesema katika kipindi cha utekelezaji wa makubaliano hayo, Serikali itaanza kugharamia hatua kwa hatua asilimia 75 ya bidhaa za afya ambazo kwa sasa zinanunuliwa kwa ufadhili wa Marekani.
Kwa upande wa eneo la nne, Clark amesema wahudumu wa afya wa mstari wa mbele wanaolipwa kupitia fedha za Marekani wataingizwa katika mfumo wa ajira wa Serikali ili kuhifadhi utaalamu wao na kuimarisha nguvu kazi ya sekta ya afya nchini.
“Eneo la tano linahusu kujenga mfumo wa kisasa wa taarifa za afya unaounganisha huduma za tiba, ufuatiliaji wa magonjwa, mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, ugharamiaji wa huduma na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia za kidijitali,” amesema Clark.
Mbali na maeneo hayo matano, Clark amesema Marekani na Tanzania zimekubaliana kushirikiana kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ubora wa afya na uzalishaji wa dawa na bidhaa tiba katika ukanda ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, Waziri Mchengerwa amesema makubaliano hayo yanaashiria hatua mpya ya ushirikiano unaojengwa katika misingi ya usawa, uwajibikaji na kujitegemea, badala ya utegemezi wa muda mrefu.
“Tunaamini makubaliano haya yatakuwa mfano kwa bara letu na tunatamani nchi nyingine za Afrika zije kujifunza namna ambavyo Tanzania na Serikali ya Marekani zimejenga ushirikiano huu. Vilevile, makubaliano haya yanaendana na dira ya nchi ya kuingia katika uchumi wa viwanda kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani na kujenga uwezo wa kujitegemea katika sekta ya afya,” amesema Mchengerwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tommy Pigott amesema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha hospitali, maabara na wahudumu wa afya, pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya VVU, malaria, kifua kikuu, polio na kuboresha afya ya mama na mtoto.
Akitoa maoni yake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Alex Msoka amesema mabadiliko ya sera ya Marekani ya kuelekeza fedha za ushirikiano wa afya moja kwa moja kwa Serikali ya Tanzania ni hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa matumizi ya rasilimali.
Amesema baada ya ukaguzi wa miradi mbalimbali, ilibainika kuwa baadhi ya maeneo yalikuwa yakipokea fedha zinazofanana na bajeti zilizokuwa tayari zimetengwa na Serikali, hali iliyozua maswali kuhusu ufanisi wa matumizi ya fedha.
Dk Msoka amesema mfumo mpya utaiwezesha Serikali kupanga vipaumbele kulingana na mahitaji halisi ya wananchi.
Hata hivyo, amesema mabadiliko hayo yamewaathiri wataalamu wengi waliokuwa wakifanya kazi kupitia mashirika yaliyokuwa yakitekeleza miradi hiyo chini ya Serikali ya Marekani, huku kukiwa na sintofahamu kuhusu namna watakavyojumuishwa katika mfumo mpya.
Ameongeza kuwa, Serikali italazimika kubaini maeneo yenye upungufu mkubwa wa rasilimali watu na kuhakikisha fedha mpya zinaelekezwa kwenye mahitaji hayo kwa kuzingatia uwezo wa mfumo wa ajira wa umma.