
LICHA ya kushindwa kutwaa Tuzo ya Ufungaji Bora katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026, straika wa Namungo, Fabrice Ngoy amesema kwake ni mafanikio kuvuka rekodi ya mabao ya msimu uliopita na kuibakiza salama timu kwenye ligi hiyo.
Hata hivyo, nyota huyo raia wa DR Congo hakusita kukubali ugumu na ushindani wa Ligi Kuu akieleza kuwa kwa misimu minne sasa aliyodumu Tanzania yapo mengi ya kujifunza kwa wachezaji wazawa na wa kigeni akiwamo straika wa Yanga, Prince Dube kutoka Zimbabwe.
Ngoy aliyetambulishwa Tanzania na Kitayosce iliyobadilishwa kuwa Tabora United na sasa inaitwa TRA United, kwa mara ya kwanza alifunga mabao 15 wakati akiipandisha timu hiyo Ligi Kuu ambapo Namungo ilimuona na kumvuta kikosini.
Msimu uliopita straika huyo hakuwa na makali baada ya kuumia na kujikuta nje ya uwanja muda mrefu akifanikiwa kufunga mabao mawili pekee, ambapo msimu ulioisha ameonekana kuwaka akifunga mabao 11 ikiwamo ‘hat trick’ moja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkongomani huyo ambaye alishatajwa kufanya mazungumzo na Simba, alisema licha ya hesabu zake kutamani kiatu cha mfungaji bora msimu huu, lakini hata kuvuka rekodi ya msimu uliopita na kuiacha salama timu Ligi Kuu ni mafanikio makubwa kwake.
Alisema kwa muda aliodumu Tanzania, ameona ugumu wa ligi na ushindani wa wachezaji kuanzia vita ya namba hadi mafanikio, akimtaja Dube kuwa mshambuliaji anayemfundisha vitu ndani ya uwanja.
“Kwa ujumla ligi ilikuwa ngumu kuanzia ubingwa, nafasi nne na hadi kujua timu mbili za kushuka daraja, kwakuwa yote yamepatikana mechi za mwisho, kwangu najiona nimefanikiwa kwanza kufunga mabao 11 na kuibakiza timu Ligi Kuu.
“Ushindani ulikuwa mkubwa, nilikutana na mabeki wengi walionipa ugumu kuwapita lakini washambuliaji nao wameonesha ukomavu, binafsi najifunza kwa Dube namna anavyocheza,” alisema straika huyo.
Kuhusu hatma yake ya kubaki au kuondoka Namungo, nyota huyo alisema kwa sasa anasubiri simu ziite kwa kuwa mkataba wake na timu hiyo umeisha, akieleza kuwa kazi yake ni mpira na yuko tayari kukipiga popote.