DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) wamezindua Nyumba Janja yenye mfumo wa kisasa wa utakaosaidia kuongeza uslaama wa nyumba kwa kupunguza hatari za majanga kama moto na ajali nyingine zinazosababishwa na hitilafu za umeme.

Akizungumza katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa ya Dar es salaam (sabasaba) Mkurugenzi wa Mawasiliano na huduma kwa wateja wa TANESCO, Irene Gowele teknolojia hiyo italenga kuongeza ufanisi wa maumizi ya umeme na kuboresha maisha ya watanzania na itawawezesha wananchi kuelewa kwa vitendo thamani ya matumizi ya umeme katika maisha ya kila siku.

Aidha, amesema teknolojia hiyo inamwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme kwa kutumia programu maalumu (application) kwenye simu ya mkononi. Kupitia mfumo huo, mteja anaweza kuwasha au kuzima vifaa vya umeme akiwa mahali popote duniani, sambamba na kufuatilia kiwango cha matumizi ya umeme wa kila kifaa ili kupunguza gharama za matumizi.

“Teknolojia hii inawasaidia wateja kudhibiti matumizi ya umeme kwa ufanisi zaidi. Pia ndani ya nyumba hiyo tumeweka vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi (energy efficient appliances), ambavyo vinatumia umeme kidogo lakini vinatoa huduma bora,” amesema Gowele.

Mbali na Nyumba Janja, TANESCO inaendelea kutekeleza mpango wa kuwawezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa njia ya mkopo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Gowele amesema wananchi wanaotembelea banda la TANESCO wanaweza kununua au kukopa majiko hayo kwa kuwasilisha namba ya mita ya umeme pamoja na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) kwa ajili ya kuthibitisha taarifa zao kama wateja wa TANESCO.

Ameeleza kuwa majiko hayo ni ya matumizi bora ya umeme na yana uwezo wa kupika vyakula mbalimbali vya Kitanzania kwa matumizi madogo ya nishati, hali inayowafanya wananchi kuokoa gharama za kupikia.

Katika maonesho hayo, TANESCO pia inatoa fursa kwa wananchi kujionea kwa njia ya teknolojia ya kidijitali baadhi ya miradi mikubwa ya uzalishaji umeme nchini, ikiwemo Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) pamoja na mradi wa kwanza mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jua uliopo Kishapu mkoani Shinyanga wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50.

Vilevile, shirika hilo linaendelea kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme. Katika banda hilo kuna magari, pikipiki na bajaji za umeme zinazowawezesha wananchi kujifunza kuhusu faida za teknolojia hiyo, ikiwemo kupunguza gharama za usafiri na kulinda mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *