TBL yataja ongezeko la faidaTBL yataja ongezeko la faida

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Tanzania Breweries PLC (TBL) imetangaza kuongezeka kwa mapato yake kwa asilimia 13 mwaka 2025 huku faida ya uendeshaji ikiongezeka kwa asilimia 35.

Kampuni ilieleza kuwa matokeo hayo yalitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa zake, usimamizi wa gharama na maboresho katika mfumo wa usambazaji wa bidhaa.

Aidha, wanahisa wa TBL wamepitisha ripoti ya wakurugenzi, ripoti ya wakaguzi wa hesabu pamoja na taarifa za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, baada ya kampuni kuripoti ongezeko la mapato na faida katika mwaka huo.

Maamuzi hayo yalifikiwa wakati wa Mkutano Mkuu wa 53 wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ambapo wanahisa pia walithibitisha mgao wa muda uliolipwa kwa mwaka 2025 na kuidhinisha kampuni ya PricewaterhouseCoopers kuwa wakaguzi wa hesabu wa nje kwa mwaka wa fedha 2026.

Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBL, Balozi Ami R. Mpungwe, alisema mkutano huo umeendelea kuimarisha misingi ya utawala bora na uwajibikaji kwa wanahisa, huku Bodi ikiendelea kusimamia maslahi ya kampuni na wanahisa wake.

Mbali na matokeo ya kifedha, kampuni ilieleza kuwa mwaka 2025 ulikuwa mwaka wa kwanza wa uendeshaji kamili wa Kiwanda cha Kimea cha Kilimanjaro chenye uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za kimea kwa mwaka, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya shayiri inayolimwa nchini.

Pia, TBL ilisema imeendelea kupanua matumizi ya mifumo ya kidijitali katika shughuli zake, kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara pamoja na kuwasaidia wakulima wadogo wa shayiri na mtama.

Mkutano huo pia ulitoa heshima kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo, marehemu Leonard C. Mususa, aliyefariki dunia Mei 30, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *