BEKI wa Timu ya Taifa ya Wanawake,  Twiga Stars, Julietha Singano, yupo mbioni kujiunga na Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia kutokana na kiwango chake alichokionyesha akiwa Mexico.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza kuwa Al Ittihad ndiyo iko siriazi katika mazungumzo ya kumsajili beki huyo, huku Al Nassr na Al Hilal nazo zikiwa zimeonyesha nia ya kupata saini yake.

Chanzo cha karibu na mchezaji huyo kimesema mazungumzo yanaendelea vizuri na huenda yakakamilika ndani ya muda mfupi.

“Ni kweli kuna mazungumzo yanaendelea kati ya upande wa mchezaji na klabu za Saudi Arabia. Kwa sasa Al Ittihad ndiyo ipo karibu zaidi kukamilisha dili,” kilisema chanzo hicho.

Singano alijiunga na FC Juarez ya Mexico katika msimu wa 2022-2023 akitokea Simba Queens na tangu wakati huo amekuwa mmoja wa mabeki tegemeo.

Licha ya kushindwa kutwaa ubingwa wa ligi, beki huyo ameendelea kupata sifa kutokana na uimara wake katika safu ya ulinzi, jambo lililovutia vigogo wa soka la Saudi Arabia kutaka huduma yake.

Kama dili hilo litakamilika anaweza kuungana na mshambuliaji wa Tanzania, Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr ya Saudia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *