TANGA: SIASA za Mkoa wa Tanga zimechukua sura mpya baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe Hamza, kutangaza rasmi kuondoka upinzani na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tukio hilo limefanyika leo, Julai 6, 2026, katika Ofisi za CCM Mkoa wa Tanga, ambapo kiongozi huyo alipokelewa rasmi na viongozi wa chama hicho tawala.
Akizungumza mbele ya wanachama na umma wakati wa hafla hiyo, Rashid Jumbe alieleza kuwa uamuzi wake wa kuhamia CCM umetokana na kuridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
“Nimeona hakuna sababu ya kuendelea kubaki upande wa upinzani wakati miradi mingi ambayo nilikuwa nikiipigania kwa miaka mingi sasa imetekelezwa,” alisema Jumbe.
Alisisitiza kuwa uamuzi huo ameufanya kwa hiari yake binafsi, bila kushawishiwa na mtu yeyote wala kupewa malipo ya kifedha, bali ni kutokana na imani yake katika dira ya maendeleo ya chama hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahman akimkaribisha kiongozi huyo mpya, amesema kujiunga kwa Jumbe ni nyongeza kubwa na muhimu kwa chama chao.
Abdallah alibainisha kuwa uzoefu na ushawishi aliokuwa nao Jumbe katika siasa za upinzani utakuwa chachu ya kuimarisha zaidi mtandao na ushawishi wa CCM mkoani humo.
Tukio hili linatazamwa na wachambuzi wa siasa kama mwendelezo wa mabadiliko ya kisiasa mkoani Tanga, huku CCM ikizidi kuonyesha nia ya kujikita zaidi kupitia sera zake za maendeleo.
