STAA wa zamani wa Simba, Meddie Kagere, amesema klabu hiyo imeanza kurejea katika mstari wa kunyakua mataji, lakini inabidi isajili wachezaji wengine wa kuongeza nguvu msimu ujao wa 2026-2027.
Kagere aliyeichezea Simba kuanzia 2018 hadi 2022 akitokea Gor Mahia ya Kenya, alisema mabadiliko ya kiushindani katika klabu hiyo aliyaona baada ya kuongeza wachezaji kipindi cha usajili wa dirisha dogo ambao wameonyesha kiwango cha juu na kuisaidia timu hiyo kuchukua mataji mawili ambayo ni Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho la CRDB.
“Kipindi nasajiliwa Simba ilikuwa na wachezaji wenye viwango vya juu, katika nafasi yangu alikuwepo Emmanuel Okwi, nilikuwa najua wazi ni mchezaji hatari, ili nipate nafasi nikamfuatilia yeye anapenda kuzunguka zaidi uwanja na kutoa asisti, mimi nikachagua kusimama katika eneo la kufunga ili nifunge mabao mengi na plani yangu ilifanikiwa,” alisema Kagere na kuongeza;
“Ukiachana na Okwi, kulikuwa na John Bocco, Cris Mugalu, Luis Miquissone, Clatous Chama, Pascal Wawa, Shomari Kapombe na wengine wengi.
“Hivi sasa Simba imesajili wachezaji wazuri dirisha dogo, hivyo katika usajili wa dirisha kubwa waongeze wengine wenye uwezo wa juu ambao wataleta ushindani kwa hao waliopo ili kikosi cha kwanza mchezaji anayeanza na anayekaa benchi viwango viwe sawa, siyo mchezaji akikosekana katika mechi timu iwe inayumba.”
Mastaa wapya ambao walisajiliwa Simba dirisha dogo la Januari 2026 ni Inno Jospin Loemba (bao moja), Anicet Oura (mabao sita, asisti nne), Mahamadou Djibrilla Kassali (cleansheets 16), Nickson Kibabage, Libasse Gueye (mabao saba) pia kurejea kwa Clatous Chama kutoka Singida BS aliyemaliza msimu akiwa na mabao manane na asisti saba, kitu ambacho Kagere anaona kimeleta mabadiliko kwa Wanamsimbazi.
Msimu wa 2017-2018, alianza Okwi kunyakua kiatu cha ufungaji bora, akafuatia Kagere aliyechukua mara mbili mfululizo 2018-2019 akifunga mabao 23 na 2019-2020 akafunga mabao 22, uliofuata wa 2020-2021 alikuwa Bocco aliyemaliza na mabao 16, jambo alilosisitiza mafanikio hayo yalitokana na wachezaji wa viwango vya juu.
“Tulikuwa tunachukua viatu vya ufungaji bora kwa mfululizo kwa sababu wachezaji tulikuwa na ushindani kuanzia kwenye timu hadi kwa wapinzani, hicho ndicho kilichoipa mafanikio Yanga kipindi inachukua ubingwa kwa mfululizo,” alisema.