IRINGA: Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa imezidua jengo lake la kisasa lenye thamani ya Sh Bilioni 1.67, hatua inayotarajiwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Jengo hilo lililojengwa katika eneo la Gangilonga, Manispaa ya Iringa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha taasisi zake na kuondoa utegemezi wa ofisi za kupanga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, alisema ujenzi wa jengo hilo unaonyesha dhamira ya Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha taasisi zinazosimamia uwajibikaji na kulinda rasilimali za umma.

Alisema TAKUKURU haijengi majengo kwa ajili ya hadhi, bali kwa lengo la kuhakikisha taasisi hiyo inafanya kazi katika mazingira salama, yenye uhuru na yasiyoweza kuathiriwa na migongano ya kimaslahi inayoweza kujitokeza wakati wa kupanga majengo ya watu binafsi.

“Hatujengi majengo kwa ajili ya ufahari. Tunajenga mazingira yatakayowezesha taasisi kufanya kazi kwa uhuru, kwa usalama na bila migongano ya kimaslahi inayoweza kujitokeza pale inapolazimika kupanga ofisi,” alisema Chalamila.

Alisema kwa sasa TAKUKURU ina ofisi 145 nchini, zikiwemo za mikoa 28 na wilaya 111, lakini ni majengo 70 pekee yanayomilikiwa na taasisi hiyo, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mpango wa kuongeza idadi hiyo katika miaka ijayo.

Chalamila alisema historia ya jengo hilo ilianza mwaka 1999 wakati aliyekuwa Mkuu wa kwanza wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Ernest Barulo, alipotafuta na kuhifadhi eneo ambalo sasa limejengwa ofisi hiyo.

“Leo tunashuhudia matunda ya maono ya viongozi waliotangulia. Kama eneo hili lisingehifadhiwa miaka hiyo, usingekuwepo uwekezaji huu tunaouona leo,” alisema.

Aidha, alisema pamoja na kuimarisha miundombinu, TAKUKURU itaendelea kutumia elimu kwa umma, sanaa, muziki, maigizo na klabu za wapinga rushwa mashuleni ili kujenga jamii inayochukia rushwa.

Aliwahimiza wananchi wa Iringa kutumia jengo hilo kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa.

“Kila mwananchi ana wajibu wa kulinda fedha za maendeleo kwa kutoa taarifa pale anapoona viashiria vya rushwa au ubadhirifu,” alisema.

Pia alizitaka halmashauri kuhakikisha taarifa za miradi ya maendeleo zinawekwa wazi kwenye mbao za matangazo ili wananchi waweze kufuatilia matumizi ya fedha za umma na kushiriki katika usimamizi wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki wa TAKUKURU, Dk Mhandisi Emmanuel Kyabo, alisema mradi huo ulitekelezwa kwa utaratibu wa Design and Build kupitia Shirika la Magereza (Prisons Corporation Sole), huku usanifu na usimamizi wa ujenzi ukifanywa na wataalamu wa TAKUKURU kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza.

Kwa mujibu wa Dk Kyabo, mradi huo ulihusisha kubomoa majengo manne ya zamani na kujenga jengo jipya la ghorofa moja, nyumba ya walinzi, kituo cha kupokelea umeme wa TANESCO na jenereta, uzio wenye urefu wa mita 310 pamoja na mfumo wa maji wenye tanki la kuhifadhi lita 60,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *