Folarin Balogun

Chanzo cha picha, Getty Images

Ilikuwa moja ya mambo yasiyo na shaka katika mchezo huo: ukiondolewa uwanjani kwenye Kombe la Dunia, utakosa mechi inayofuata.

Hakuna cha ikiwa, lakini au kukata rufaa.

Uamuzi wa kubatilisha kadi nyekundu aliyotolewa dhidi ya mshambuliaji nyota wa Marekani, Folarin Balogun, umeibua maswali chungu nzima.

Balogun, alitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu wakati wa mechi ya hatua ya 32 dhidi ya Bosnia-Herzegovina, lakini sasa ataichezea Marekani katika mechi ya hatua ya 16 dhidi ya Ubelgiji leo Jumatatu. Balogun ndiye mfungaji bora wa Marekani kwenye michuano hiyo akiwa na mabao matatu.

Kumetolewa takribani kadi nyekundu 189 katika historia ya Kombe la Dunia, na ni wachezaji wawili tu ambao hawakutumikia adhabu.

Nyingine ilikuja mwaka wa 1962, wakati Garrincha wa Brazil alipotolewa kwa kadi nyekundu dhidi ya Chile katika nusu fainali, lakini alicheza katika mechi ya ushindi dhidi ya Czechoslovakia katika fainali.

Wakati huo, hata hivyo, hakukuwa na marufuku ya moja kwa moja. Iliamuliwa na kamati kwa ushahidi uliotolewa na viongozi.

Uamuzi wa kamati ya nidhamu ya Fifa mwaka 1962 uligubikwa na madai ya kuingiliwa kisiasa.

Kwa kuzingatia uhusiano wa karibu ulioimarishwa kati ya Ikulu ya White House na Fifa, maswali yataulizwa kwa sababu uamuzi ambao sio wa kawaida.

Mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani CBS News imethibitisha kuwa Balogun ameruhusiwa kucheza baada ya rais wa Marekani Donald Trump kumpigia simu rais wa Fifa Gianni Infantino siku ya Alhamisi na kuzungumza naye kuhusu kuhusu kuondolewa uwanjani kwa mchezaji huyo, vyanzo vinavyofahamu wito huo viliiambia CBS News.

Je, hii inaweka wapi historia ya soka?

Kwa nini Balogun amepewa ahueni, lakini wachezaji wengine 11 waliotolewa kwenye Kombe hili la Dunia wote wamefungiwa?

Je, itasababisha rufaa zaidi katika soka kwa nia ya kupunguza adhabu hata wakati kadi nyekundu zilihalalishwa kwa mujibu wa sheria?

Taarifa zinaposema mchezaji “kukosa mechi ijayo” ya Kombe la Dunia baada ya kupewa kadi nyekundu. Je, waandishi wa habari wana hakika gani kwamba uamuzi huo utazingatiwa?

Katika taarifa hii tunaangazia uamuzi huo na athari zinazoweza kutokana na hatua ya kubatilisha adhabu ya kadi nyekundu.

Fifa haikutoa sababu wala maelezo

Kuna swali moja kuu ambalo baadhi ya watu wanauliza. Ilikuaje?

Kanuni za nidhamu za Fifa zinasema kwamba Balogun anapaswa kupigwa marufuku ya “walau mechi mbili kwa kucheza visivyo”.

Sheria za Kombe la Dunia haziruhusu timu kukata rufaa dhidi ya kadi nyekundu.

Taarifa ya Fifa haikutoa sababu wala maelezo ya kubatilisha uamuzi wa kinidhamu uliyotolewa dhidi ya Balogun. Ilitaja tu “kifungu cha 27 cha kanuni za nidhamu za Fifa”.

Kifungu cha 27 kinaruhusu Fifa “kusimamisha kikamilifu au kwa sehemu utekelezaji wa hatua ya kinidhamu”.

Ni sheria pana ambayo inaruhusu Fifa kufanya uamuzi wowote inaotaka bila kukidhi vigezo vingine.

Kifungu cha 27 hakijawahi kutumika katika Kombe la Dunia.

BBC Sport imeuliza kwa nini hii ilitokea.

Lakini hatukupewa hoja yoyote. Tulielekezwa tu kwa marufuku iliyosimamishwa ya Cristiano Ronaldo kabla ya mashindano haya.

Chini ya kanuni za nidhamu za Fifa, Ronaldo alipaswa kupigwa marufuku ya mechi tatu kwa kumpiga kiwiko Dara O’Shea wakati Ureno ilipochapwa 2-0 na Jamhuri ya Ireland katika mechi ya kufuzu kwa michuano hiyo iliyokamilika kwa ushindi wa 2-0 mwezi Novemba.

Alitumikia mechi moja katika mechi ya mwisho ya kufuzu dhidi ya Armenia – lakini michezo miwili iliyosalia ya marufuku hiyo ilisitishwa.

Kadi nyekundu ya Ronaldo, hata hivyo, ilipokelewa katika mechi ya kufuzu. Haikuwa kadi nyekundu kwenye Kombe la Dunia.

Kumekuwa na visa vingi vya wachezaji kusamehewa kabla ya mashindano, sio Ronaldo pekee.

Kuna wachezaji kama vile Mfaransa Laurent Koscielny mwaka wa 2014, au Moises Caicedo wa Ecuador na Nicolas Otamendi wa Argentina kabla ya Kombe hili la Dunia.

Katika uamuzi wa Ronaldo, angalau tulipewa maelezo huku Fifa ikisema ilizingatia kwamba “hakuwa na kadi nyekundu katika mechi zake nyingine 225 za kimataifa”.

Na Balogun, hakufikia kiwango hicho hata kidogo.

Hali hii imeacha pengo la taarifa ambalo linaweza kkuibua uvumi.

Kwa nini hili lilikuwa tukio la kipekee? Ni mambo gani yalizingatiwa? Nani aliyefanya uamuzi huo?

BBC Sport imefahamishwa kuwa hakuna madai yoyote kwamba mwamuzi aliomba adhabu hiyo ya kusimamishwa iondolewe, au kwamba taratibu za matumizi ya video kusaidia mwamuzi (VAR) hazikuzingatiwa.

Nchini Uingereza, Chama cha Soka (FA) kingechapisha sababu kamili zilizoandikwa.

Marekani ina haki ya kuiomba FIFA ichapishe sababu hizo, lakini Ubelgiji haina haki hiyo.

Mchambuzi wa BBC Sport, Micah Richards, ambaye ni mchezaji wa zamani wa safu ya ulinzi ya Uingereza, alisema hali hiyo ni ya mzaha mtupu.

“Kusimamishwa kwa adhabu hiyo kwa mwaka mmoja kunafanya mashindano yote yaonekane kama mzaha,” alisema.

“Lengo ni kuwabakisha mastaa wakubwa kwenye mashindano. Hilo linawezekanaje? FIFA inapaswa kufanya vizuri zaidi.

“Jambo hili limewaacha wengi na hisia mseto.”

Bila shaka, Ubelgiji imekasirishwa sana. Ilitoa taarifa siku ya Jumapili ikisema kuwa ilishangazwa na uamuzi wa kumruhusu Balogun kucheza.

Chama cha Soka cha Ubelgiji kilirejelea kanuni kadhaa, mawasilisho ya semina na mikutano ya uratibu iliyofanyika kabla ya mashindano.

Wanasisitiza kuwa uamuzi huo unakinzana na kanuni za mashindano ambazo zinasema mchezaji “atasimamishwa moja kwa moja kucheza mechi inayofuata ya timu yake”.

Kwa hakika, wanasema FIFA ilitumia kanuni zake za nidhamu kupuuza kanuni za mashindano hayo.

Kocha mkuu wa Ubelgiji, Rudi Garcia, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, alizungumza zaidi. Alisema: “Sikujua kwamba katika Kombe la Dunia la FIFA, tarehe 5 Julai sasa ni tarehe 1 Aprili, siku ya kufanya mizaha (April Fool’s).

“Hatutetei timu ya taifa wala shirikisho, tunatetea soka.”

Je, wachezaji wengine walioonyeshwa kadi nyekundu katika mashindano haya wanawaza nini?

Mfano ni Assim Madibo wa Qatar, aliyehusika katika tukio la bahati mbaya lililosababisha kiungo wa Canada, Ismael Kone, kuvunjika mguu.

Kuna ushahidi wa wazi hapa kwamba Madibo hakufanya jaribio la kumzuia mpinzani (tackle), na kwamba jeraha hilo lilitokea kwa bahati mbaya na si kutokana na namna alivyocheza.

Hata hivyo, FIFA ilimpa Madibo adhabu ya kutocheza mechi tano—ikiwa ni pamoja na mechi tatu za ziada juu ya adhabu ya kawaida kwa kosa kubwa la uchezaji usio wa kiungwana.

Je, uamuzi wa balogun umeleta mfano wa kisheria

Balogun alionyeshwa kadi nyekundu kufuatia uamuzi wa VAR

Chanzo cha picha, Getty Images

Je, kadi nyekundu ya Balogun ilikuwa kali? Bila shaka.

Mshambuliaji huyo alikuwa akimkabili Tarik Muharemovic, na kwa bahati mbaya akampiga mguu wake kwenye kifundo cha mguu wa Mbosnia huyo.

Hasira haimaanishi kuwa ulikuwa uamuzi usio sahihi, au kwamba ulikuwa mbaya sana kiasi kwamba Fifa ilibidi iingilie kati.

Je, Fifa sasa ifute adhabu yoyote baada ya kadi nyekundu kutokana na kitendo cha bahati mbaya?

Makocha watakuwa wakitoa hoja – mfano umewekwa, sasa tuwe na msimamo thabiti.

Nia iliondolewa kwenye sheria miaka mingi iliyopita, na matokeo ya changamoto pekee ndiyo yanapaswa kuzingatiwa.

Kuchukua kadi nyekundu ya Xavi Simons dhidi ya Liverpool Desemba iliyopita. Mshambuliaji huyo wa Tottenham hakukusudia kusimama nyuma ya mguu wa Virgil van Dijk, lakini alifanya hivyo na ilihukumiwa kuhatarisha usalama wa mpinzani.

Kocha mkuu wa Tottenham wakati huo, Thomas Frank, alilalamika kuhusu kufungiwa mechi tatu moja kwa moja, lakini klabu hiyo iliamua kutokata rufaa, ikiamini hawakuwa na nafasi ya kufanikiwa.

Uamuzi wa Balogun unaongeza wasiwasi ndani ya ligi za ndani kutokana na maamuzi katika Kombe hili la Dunia.

Kuna hofu kwamba ukosefu wa kadi za njano, baadhi ya utekelezaji wa VAR, pamoja na tafsiri ya sheria mpya, haiwezi kuzingatiwa katika ngazi ya ligi.

Na mashabiki watatarajia iwe hivyo hivyo.

Kufuta marufuku dhidi ya Balogun kutafanya hali kuwa nguu zaidi kwao.

Kwa nini Chama cha Soka hakiwezi kuonyesha huruma kama Fifa ilivyofanya?

Hakika marufuku ya kupita kiasi kama yale yaliyotendwa na Simons yanapaswa kuzingatiwa?

Trump alihusikaje na uamuzi huo?

Mojawapo ya misingi ya mchakato wa nidhamu wa Fifa wa Kombe la Dunia ni kwamba huwezi kukata rufaa.

Kwa nini Fifa imeshughulikia kesi maalum kwa mchezaji nyota wa taifa mwenyeji?

Kadi nyekundu na kusimamishwa kulisababisha ghasia nchini Marekani.

Kumekuwa na madai nchini Marekani kwamba mshambuliaji huyo alipewa adhabu mara mbili kwa kukosa mechi moja na karibu theluthi moja ya nyingine – dakika 27 za mwisho dhidi ya Bosnia na mechi dhidi ya Ubelgiji. Hii haikuwa haki kabisa, wachambuzi walisema katika vyombo vya habari nchini Marekani.

Kulikuwa na shinikizo kutoka kwa vyombo vya habari na kutoka kwa utawala wa Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alisema Ijumaa kwamba Marekani “imevurugwa na kadi hiyo nyekundu” na kwamba “kuna haja ya kuwa na mchakato wa kukata rufaa”.

Hata hivyo, hakukuwa na matarajio kwamba Fifa ingeweza kutoa uamuzi maalum ambayo ingemruhusu mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal kucheza.

Kwa kweli, Balogun alipokea adhabu chungu nzima dhidi ya Bosnia na yuko huru kucheza tena.

Vyanzo vya vya habari ya CBS vilisema Trump alizungumza na Infantino moja kwa moja katika mazungumzo mafupi.

Infantino alimwambia rais kwamba kamati ya nidhamu ya Fifa itachunguza hilo, kulingana na moja ya vyanzo hivyo.

Andrew Giuliani, mkurugenzi mtendaji wa kikosi kazi cha Kombe la Dunia cha Ikulu ya White House, pia alizungumza na Infantino kuhusu hali hiyo, na Waziri wa Biashara Howard Lutnick pia alikuwa akiwasiliana na Fifa.

Wasemaji wa Ikulu ya White House, Lutnick na Giuliani hawakujibu ombi la CBS News la kutoa maoni.

Jumapili jioni, Trump aliishukuru Fifa kwa “kubatilisha dhuluma kubwa” katika chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

Kamati ya maadili ya Fifa ilikuwa tayari imeombwa kumchunguza Infantino, ikidai alivunja sheria za kutoegemea upande wowote kisiasa kuhusiana na kutoa Tuzo ya Amani ya Fifa ya Trump.

Sheria za baraza linaloongoza duniani zinapinga uingiliaji wa kisiasa katika soka.

Kwa kuwa utawala wa Marekani utahusika, kutakuwa na maswali zaidi ya kujibu.

Lakini kabla ya hapo, macho yote yatakuwa kwa Balogun na Marekani dhidi ya Ubelgiji Jumatatu.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *