Harare. Hatimaye Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesaini kuwa sheria muswada unaoongeza muda wa urais kwa miaka miwili, hatua inayomruhusu kuendelea kuhudumu madarakani hadi mwaka 2030.

Msemaji wa Serikali ya Zimbabwe, Nick Mangwana, alithibitisha hatua hiyo, jana Jumanne Julai 7, 2026 kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, akisema: “Imesainiwa, imethibitishwa na sasa ni sheria,” huku akiambatanisha nakala ya sheria hiyo.

Mwezi uliopita, mabunge yote mawili ya Zimbabwe yaliidhinisha muswada huo baada ya mjadala mkali ulioibua maoni yanayokinzana.

Wanaounga mkono hatua hiyo wanasema marekebisho hayo yatasaidia kupunguza gharama za kuandaa uchaguzi, huku wanaoupinga wakidai yanadhoofisha misingi ya demokrasia kwa kuwanyima wananchi haki ya kumchagua rais wao kupitia kura ya moja kwa moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Idhaa ya Kiswahili BBC, sheria hiyo pia ina kipengele kinachoruhusu rais kuchaguliwa na Bunge badala ya wananchi kumpigia kura moja kwa moja.

Dalili za Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, kutaka kuendelea kubaki madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili mwaka 2028 zilianza kujitokeza takribani miaka miwili iliyopita.

Wafuasi wake walikuwa wakichombeza kwa kuimba kaulimbiu katika mikutano ya chama tawala cha ZANU–PF wakimtaka apewe muda zaidi ili akamilishe ajenda yake ya maendeleo.

Mwaka jana Chama cha ZANU–PF kilipitisha azimio la kufanya marekebisho ya katiba kwa lengo la kuongeza muda wa mihula ya urais.

Baadaye, Februari mwaka huu, pendekezo hilo lilipata uungwaji mkono na idhini ya baraza la mawaziri na hatimaye kupitishwa na mabunge yote mawili kabla ya kutiwa saini na rais na kuwa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *