
Rais Masoud Pezeshkian na Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al-Zaidi, wamehudhuria hafla rasmi ya mapokezi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Najaf, kwa ajili ya kupokea mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kabla ya kuanza kwa taratibu za mazishi nchini Iraq.
Ndege iliyobeba jeneza la Kiongozi huyo Shahidi pamoja na wanafamilia wake ilitua Najaf usiku wa Jumanne.
Majeneza hayo yatapelekwa katika misafara ya kuwaaga mashahidi iliyopangwa kufanyika siku ya Jumatano katika mji wa Najaf na mji mtakatifu wa Karbala.
Mamilioni ya Wairaqi wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo, ikizingatiwa kuwa Shahidi Ayatullah Khamenei alikuwa mwanachuoni anayeheshimika sana nchini Iraq na chanzo cha kuigwa (Marjaa) kwa mamilioni ya Waislamu wa Kishia katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Waziri Mkuu Al-Zaidi ametangaza siku ya Jumatano kuwa mapumziko ya kitaifa nchini Iraq ili kuruhusu nchi hiyo kuandaa vyema hafla hiyo kubwa.
Asubuhi ya leo, Jumatano, ibada ya swala ya maiti kwa ajili ya mwili wa Kiongozi Shahidi wa Umma, Ayatullah Seyyed Ali Hosseini Khamenei, na mashahidi wanafamilia yake, imefanyika katika Haram takatifu ya Imam Ali (AS) huko Najaf Ashraf.
Ingawa taratibu za kuaga mwili wa Kiongozi huyo wa Mapinduzi katika miji ya Najaf na Karbala zimepangwa kuchukua muda mfupi tu, tukio hili linatazamwa kama miongoni mwa matukio makubwa na muhimu zaidi katika historia ya miji hii miwili. Uzito wa tukio hili unaonekana zaidi ikizingatiwa kuwa miji hii miwili, ambayo ni ngome kuu za ulimwengu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, kwa kawaida hupokea umati mkubwa wa waumini wakati wa miezi mitukufu ya Muharram, Safar, Sha’ban, na Ramadhan.
AyatIllah Khamenei na wanafamilia wake wanne waliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa kwa pamoja na Marekani na Israel dhidi ya ofisi na makazi yake mjini Tehran mnamo Februari 28 sawa na 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kabla ya Iraq, kulifanyika hafla za kuwaaga mashahidi hao watukufu katika mji mkuu wa Iran, Tehran, na mji wa Qom. Shahidi Imam Khamenei atazikwa siku ya Alhamisi katika haram takatifu ya Imam Ridha AS, katika mji wake wa asili wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran.