Kupata tuzo mbili za kimataifa ndani ya kipindi kifupi ni ishara kuwa juhudi za Tanzania katika ujenzi na usimamizi wa miundombinu ya barabara zimeanza kutambulika kimataifa.
Hivi karibuni tuzo iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki inaonyesha uwezo wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Mafanikio hayo yanaakisi hatua kubwa iliyofikiwa na Tanzania katika kupanua mtandao wa barabara za lami kwani mwaka 2001 nchi ilikuwa na takribani kilomita 1,306 za barabara za lami na sasa mtandao huo ukifikia zaidi ya kilomita 12,700.
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeibuka mshindi wa jumla wa Tuzo ya Umahiri wa Miundombinu ya Barabara Afrika katika hafla ya Tuzo za Utumishi wa Umma Afrika Mashariki mwaka 2026 iliyofanyika Juni 30, 2026 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
TANROADS imetwaa tuzo hiyo baada ya kuibuka kinara miongoni mwa washiriki katika makundi mbalimbali ya tuzo na kutangazwa kuwa mshindi wa jumla wa mashindano hayo yaliyolenga kutambua taasisi zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za umma na maendeleo ya miundombinu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango mkubwa wa TANROADS katika maendeleo ya miundombinu ya barabara, kuimarisha uunganishaji wa maeneo mbalimbali kwa njia za usafiri (national connectivity), kuongeza ufanisi wa usafiri (transport efficiency), kuendeleza ubora wa uhandisi (engineering excellence) pamoja na kujenga na kusimamia mtandao endelevu wa barabara (sustainable road networks) nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumzia hilo Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta anasema tuzo hizo si heshima kwa taasisi hiyo pekee, bali ni mafanikio ya Serikali na wananchi wote kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya miundombinu.
Anasema ushindi huo unaendelea kuthibitisha nafasi ya TANROADS kama taasisi inayoongoza katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara yenye viwango vya kimataifa, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo, pamoja na kuimarisha mtandao wa usafiri ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.
Besta anasema shukrani ni kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu ya barabara ambapo tuzo hizo zinathibitisha uimara katika utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja.
Barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma, ikiwa ni moja ya mradi ya kimkakati inayotekelezwa na TANROADS.
“TANROADS imeendelea kujenga na kutengeneza barabara licha ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza, ikiwamo athari za mvua na uharibifu wa miundombinu katika maeneo tofauti nchini,”anasema Besta.
Besta anasema miradi mingi inaendelea kutekelezwa na pale ambapo barabara zimeharibika, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati mkubwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora za usafiri.
Mbali na tuzo ya Afrika Mashariki, Besta anasema mwaka 2024, Tanzania pia ilitunukiwa tuzo ya kimataifa na International Road Federation (IRF) katika mkutano uliofanyika Marrakesh, Morocco, kutokana na mafanikio katika usimamizi wa usalama barabarani na ubunifu wa miradi ya barabara.
Anasema tuzo hiyo ni miongoni mwa tuzo zenye hadhi kubwa duniani katika sekta ya barabara, na Tanzania ilikuwa nchi pekee kutoka Afrika kutwaa heshima hiyo.
“Tuzo hii inaonesha kuwa Tanzania imefanya vizuri katika usimamizi wa miradi ya barabara pamoja na kupunguza vihatarishi vya usalama barabarani, hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu,” anasema Besta.
Besta anasema mafanikio hayo yamewezekana kutokana na uwekezaji wa Serikali pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali katika sekta ya miundombinu.
Anawahakikishia Watanzania kuwa TANROADS itaendelea kujenga na kufanya matengenezo ya barabara ili kukidhi matarajio ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kaimu Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanzania), Aisha Malima wa pili kulia akipokea tuzo ya mshindi wa jumla ya Umahiri wa miundombinu ya barabara Afrika, katika hafla ya tuzo za Utumishi wa umma Afrika Mashariki ya mwaka 2026
Anasema Tanzania ndiyo nchi yenye miradi mingi ya barabara inayofadhiliwa na taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, jambo linaloonesha imani ya wadau wa maendeleo kwa uwezo wa nchi katika kusimamia miradi hiyo.
Akizungumzia sababu za taasisi za Serikali kuanza kushinda tuzo za kimataifa, Besta anasema maboresho ya utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa mashirika ya umma chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina yameongeza ufanisi wa taasisi nyingi za Serikali.
Besta anasema TANROADS tayari imeanza kuchukua hatua za kutekeleza miradi mikubwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), akibainisha kuwa maandalizi ya baadhi ya miradi yamefikia hatua za mwisho.
Anasema hivi karibuni Serikali imesaini mikataba ya ushauri na maandalizi ya miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kupitia mfumo huo, ikiwemo mradi wa upanuzi wa barabara ya kilometa 232 pamoja na madaraja yake jambo ambalo Serikali pekee haitaweza.
Pia, anataja Mradi wa Dodoma Integrated Sustainable Transport (DIST) kuwa ni miongoni mwa miradi mikubwa yenye thamani ya mabilioni ya fedha inayotekelezwa kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri katika Jiji la Dodoma.
Kwa mujibu wa Besta, nchi nyingi zilizoendelea, hususan za Kusini Mashariki mwa Asia, zimefanikiwa kujenga miundombinu bora kwa kutumia mfumo huo, na Tanzania inaendelea kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na taasisi za fedha kama NSSF, PSSSF, CRDB, NBC na NMB ili kuongeza uwekezaji katika sekta ya barabara.
“Mustakabali wa ujenzi wa miundombinu unategemea ushirikiano mpana kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za kifedha. Huo ndiyo mwelekeo ambao Tanzania inaendelea kuufuata,” anasema.
Ongezeko la malori
Besta anasema ongezeko kubwa la magari, hususan malori yanayosafirisha mizigo kwenda na kutoka nchi jirani kama Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), limeongeza shinikizo kwenye barabara nyingi za Tanzania.
“Barabara nyingi tulizojenga miaka iliyopita sasa zinabeba mizigo mikubwa kuliko ilivyokuwa imekusudiwa, hivyo kutokana na ukuaji wa uchumi na biashara za kikanda, kuna ulazima wa kuziboresha na kuzijenga kwa viwango vya juu zaidi ili ziweze kuhimili ongezeko hilo la magari na mizigo,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, anasema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha barabara za kulipia (toll roads) katika baadhi ya maeneo ili kupata fedha za kuendeleza matengenezo na ujenzi wa miundombinu mipya.
Anasema mfumo huo unatumika katika nchi nyingi duniani na lengo lake si kuwaongezea wananchi mzigo, bali kuhakikisha kunakuwa na chanzo endelevu cha fedha za kutunza na kuboresha barabara.
“Ni muhimu wananchi wakaelewa kuwa matumizi ya barabara za kulipia ni sehemu ya mfumo wa kugharamia ujenzi na matengenezo ya miundombinu, huu ni utaratibu unaotumika katika mataifa mengi na unasaidia kuhakikisha barabara zinaendelea kuwa katika ubora unaohitajika,” anasema.
Miradi ya kimkakati
Besta anasema TANROADS inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika Jiji la Dodoma inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.
Anasema miradi inayotekelezwa na TANROADS ikiwemo barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato pamoja na mradi wa barabara ya njia sita kutoka katikati ya jiji kuelekea Chamwino, itaongeza fursa za kiuchumi, kupunguza muda wa safari na kuboresha huduma kwa wananchi.
Moja ya lori likipita kwenye daraja ambalo linasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Anasema barabara ya mzunguko wa nje iliyofikia takribani asilimia 95 ya utekelezaji itasaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji, wakati Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kitafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na utalii.
Pia, anasema mradi wa barabara ya njia sita utarahisisha usafiri wa wananchi na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi katika mji mkuu wa nchi.
“Miradi hii inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri na usafirishaji zilizo bora, salama na zenye kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” anasema Besta.
Anawahakikishia wananchi TANROADS itaendelea kutoa elimu kuhusu usalama barabarani, uhifadhi wa barabara, utunzaji wa mazingira na umuhimu wa kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti baada ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Waunga mkono maboresho ya miundombinu
Dereva wa lori linalosafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Rwanda, Jabir Mwakalonge anasema kuongezeka kwa ubora wa barabara kutapunguza gharama za uendeshaji na muda wa safari.
“Tunapitisha mizigo mingi kwenda Rwanda, Burundi na DRC, barabara zikiboreshwa na kupanuliwa, safari zitakuwa fupi, magari hayataharibika mara kwa mara na gharama za usafirishaji zitapungua, hata kama kutakuwa na barabara za kulipia, kikubwa ni kuona huduma tunayoipata inaendana na fedha tutakazolipa,” anasema.
Kwa upande wake, dereva wa basi la abiria linalofanya safari kati ya Dar es Salaam hadi Mwanza , Hamisi Mfaume, anasema wananchi watafaidika zaidi ikiwa fedha zitakazopatikana kupitia mfumo wa PPP zitatumika kujenga barabara zenye ubora na usalama.
“Barabara nzuri zinapunguza ajali, zinahifadhi magari yetu na zinawahi kufikisha abiria wanakokwenda, tunachotamani ni kuona miradi inakamilika kwa wakati na ubora unaokusudiwa,” anasema.
Naye Mhandisi wa Ujenzi wa Barabara, Peter Mbuya anasema mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa duniani kupata fedha za kuharakisha ujenzi wa miundombinu.
“Kutokana na ongezeko la magari na uzito wa mizigo inayopita kwenye barabara kuu za Tanzania, kuna haja ya kujenga barabara zenye uwezo mkubwa zaidi wa kubeba mizigo. Mfumo wa PPP unaweza kusaidia kupata fedha za kutosha bila kutegemea bajeti ya Serikali pekee, mradi utekelezwe kwa uwazi na kuzingatia maslahi ya wananchi,” anasema Mbuya.