Geita. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kufika mahakamani na kueleza sababu za kuendelea kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Geita, Neema Chozaire.

Mbali na hao, wengine ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita.

Mahakama hiyo imetoa wito huo baada ya maombi yamefunguliwa jana Jumatano, Julai 8, 2026 katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita kwa shauri namba 15077 la mwaka 2026, chini ya hati ya dharura baada ya mwenyekiti huyo kushikiliwa kwa zaidi ya siku kumi bila kufikishwa mahakamani wala kupewa dhamana.

Shauri hilo ambalo Chadema ndiyo mleta maombi, limefunguliwa chini ya Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, Jaji Projestus Kahyoza, kupitia wakili wa utetezi na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Beatus Emmanuel.

Aidha, shauri hilo limepangwa kusikilizwa Jumanne Julai 14, 2026, saa 9:30 asubuhi na kabla ya terehe ya usikilizwaji wajibu maombi wanatakiwa kuwasilisha nyaraka za viapo vyao kesho ijumaa Julai 10, 2026.

Akizungumza na Mwananchi, Wakili wa utetezi Beatus Emmanuel, amesema wameamua kufungua shauri hilo baada ya ndugu, viongozi wa chama na wakili wake kunyimwa nafasi ya kuonana na kiongozi huyo.

Pia, ameitaja sababu nyingine kuwa ni kunyimwa dhamana kwa Chozaire licha ya kushikiliwa kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Pia, kumekuwepo na hofu ya Chozaire kunyimwa mahitaji ya kibinadamu ikiwamo chakula kwa kuwa hakuna anayejua alipo kiongozi huyo.

“Hatupewi nafasi hiyo wala ndugu, jamaa na viongozi wenzake hawajui ameshikiliwa wapi, ila inajulikana anashikiliwa na polisi lakini eneo gani hasa ambapo ndugu wanaweza kwenda kumuona ni haipo na hiyo ruksa hata mawakili hawapati,” amesema.

Aidha, Wakili Beatus amesema kukamatwa kwa kiongozi huyo kabla ya kukamilika kwa uchunguzi, imekuwa chanzo cha kiongozi huyo kuendelea kushikiliwa bila sababu akiutaja utaratibu huo kupitwa na wakati.

Julai mosi 2026, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wake Mkoa wa Geita, Safia Jongo, ilithibitisha kumshikilia Chozaire kwa makosa ya kijinai huku ikibainishwa kuwa kada huyo angefikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *