Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limesema mwitikio wa wananchi wanaotembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), unaashiria kuongeza uelewa wa jamii kuhusu nafasi ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) katika kuchochea maendeleo na ajira.
Hayo yamebainishwa leo Julai 10, 2026 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dk Mwajuma Lingwanda baada ya kutembelea banda la taasisi hiyo kwenye maonyesho yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba.
Amesema wananchi wanapaswa kutumia maonyesho hayo kupata taarifa sahihi kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta ya elimu ya ufundi pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na baraza hilo.
Dk Lingwanda amesema elimu ya TVET inaendelea kuwa mhimili muhimu wa kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kukuza uchumi wa viwanda.
“Ni muhimu wananchi waendelee kutembelea banda letu ili kupata elimu kuhusu huduma za Nactvet na kufahamu fursa mbalimbali zilizopo katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini,” amesema.
Amesema moja ya vivutio vilivyopo katika banda hilo ni ushiriki wa wanafunzi kutoka shule za sekondari zenye mkondo wa amali, wanaoonyesha kwa vitendo ujuzi na maarifa waliyojifunza darasani.
Kwa mujibu wa Dk Lingwanda, maonyesho hayo yanatoa nafasi kwa wazazi, walezi na wananchi kujionea matokeo ya elimu ya amali, hatua inayochangia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wake katika kuwaandaa vijana kujiajiri na kuajirika.
Mbali na kutembelea banda hilo, Dk Lingwanda alikagua mabanda ya baadhi ya taasisi zinazosimamiwa na baraza hilo, zikiwemo Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi City, Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Aidha, amewataka viongozi wa taasisi hizo kuendelea kubuni programu za mafunzo zinazokwenda sambamba na mahitaji halisi ya soko la ajira, kuimarisha tafiti za ufuatiliaji wa wahitimu na kuhakikisha mafunzo yote yanaendeshwa kwa kuzingatia miongozo na viwango vya ubora vinavyowekwa na Nactvet.
Amesema hatua hizo zitasaidia kuongeza ubora wa wahitimu, kuimarisha ushindani wao katika soko la ajira na kuhakikisha elimu ya ufundi inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Mmoja wa watembeleaji, mkazi wa Mbagala, James Mwakalinga amesema banda la Nactvet limempa uelewa mpana kuhusu fursa zinazopatikana katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
“Nimegundua kuwa elimu ya ufundi si mbadala wa kushindwa masomo mengine, bali ni njia muhimu ya kupata ujuzi unaoweza kumsaidia mtu kujiajiri au kuajiriwa. Ni vizuri wazazi na vijana wengi wakatembelea banda hili ili wapate taarifa sahihi,” amesema.
Naye, Mrema Paul, mkazi wa Kimara, amesema maonesho ya vitendo yaliyofanywa na wanafunzi wa mkondo wa amali yameonyesha kuwa elimu ya ufundi inaweza kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea.
“Nilivutiwa kuona wanafunzi wakionyesha ujuzi wao kwa vitendo. Hii inaonyesha kuwa tukiwekeza elimu ya ufundi, tutazalisha vijana wenye uwezo wa kutatua changamoto za soko la ajira badala ya kusubiri kuajiriwa pekee,” amesema.