SIMBA inatarajia kuingia kambini Julai 18, 2026 kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame itakayopigwa nchini Rwanda kuanzia Julai 24 hadi Agosti 8 mwaka huu.

Wakati Simba ikijiandaa kuingia kambini, tayari imefahamu imeangukia kundi gani katika michuano hiyo baada ya leo Ijumaa kuchezeshwa droo.

Simba imepangwa kundi B likiwa na timu nyingine ya Tanzania Singida Black Stars. Pia zipo Jamus ya Sudan Kusini na Mogadishu City kutoka Somalia.

SIMB 01

Katika droo hiyo iliyochezeshwa na kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Haruna Niyonzima, kundi A linaundwa na APR ya Rwanda, Vipers (Uganda), Gor Mahia (Kenya) na Garde Republicaine (Djibouti), wakati kundi C ni Al Hilal (Sudan), Rayon Sports (Rwanda), Tusker (Kenya) na KVZ (Zanzibar).

“Timu itaingia kambini Julai 18 kwa ajili ya kujinadaa na mashindano ya Kagame ambayo tutayatumia kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao,” amesema bosi mmoja wa Simba.

SIMB 02

Alipotafutwa kocha wa Singida Black Stars, Muhibu Kanu, amesema kikosi chao kitaingia kambini Julai 15 mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo, wanayoyachukulia kama maandalizi ya msimu unaokuja wa 2026-2027.

“Tumepangwa kundi gumu, lakini lina faida kubwa kwani tutajipima mapema ili kujua ubora wetu, kuliko na kupangwa na timu dhaifu halafu mnashinda na inakuwa haina maana yoyote ya kujua ubora wa timu,” amesema Kanu na kuongeza;

“Tukimaliza michuano hiyo itakuwa imetupa picha ya kikosi gani tunacho kwa ajili ya msimu ujao.”

SIMB 03

Kwa mtazamo wa staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Steven Mapunda amesema: “Kutokana na muda ambao ligi itatakiwa kuanza (Agosti 14) timu za Tanzania zinazoshiriki Kagame zitafaidika kutumia kama maandalizi ya msimu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *