DAR ES SALAAM: Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na Umoja wa Wanasheria wa Afrika (PALU), Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), unaendelea kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Kukuza Uzingatiaji wa Katiba yenye lengo la kuimarisha utawala wa sheria, kulinda haki za binadamu na kuboresha upatikanaji wa haki nchini Tanzania.
Kampeni hiyo, inayoshirikisha pia vyama vya wanasheria, mashirika ya kiraia (AZAKi), taasisi za elimu ya juu, wataalamu wa sheria pamoja na vyombo vya habari, imebeba kaulimbiu isemayo, “Kuimarisha Uzingatiaji wa Katiba, Haki za Binadamu na Upatikanaji wa Haki kwa Wote.”
Kwa mujibu wa waandaaji, kampeni hiyo ilizinduliwa mwezi Juni 2026 jijini Dodoma na inatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa na dhamira ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa Katiba, kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala bora, pamoja na kuhimiza kuheshimiwa kwa haki za msingi za binadamu.
Baadhi ya viongozi na wadau wa sekta ya sheria na asasi za kiraia wanasema kampeni hiyo inakuja wakati ambao kuna umuhimu wa kuongeza ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za sheria, mashirika ya kiraia na wananchi katika kulinda misingi ya Katiba na utawala wa sheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa ADLG, James Luhende kutoka jijini Mwanza, anasema mazingira ya utendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini bado yanahitaji kuboreshwa ili yawezeshe taasisi hizo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Mazingira ya utendaji ya NGOs za Tanzania sio mepesi, yamegubikwa na mambo mengi ya kurudisha nyuma, kuanzia mambo ya kisheria mpaka mambo ya kiutendaji ambayo mtu (kiongozi) anakuwa haelewi mambo ya kisekta au ametumwa kuharibu taasisi au mtu.”
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma anasema bado kuna changamoto katika kujieleza na ushiriki wa wananchi katika masuala ya kitaifa, hali inayofanya majukwaa ya majadiliano kuwa muhimu zaidi.
“Sasa hivi kumekuwa na uhuru umeminywa sana japo ukiangalia watu wengi wanasiasa wanasema kila kitu kiko vizuri lakini ukweli ni kwamba kila kitu hakiko vizuri. Watu bado hawana uhuru wa kuzungumza, watu hawana nafasi ya kusema katika mambo mbalimbali, watu ni waoga wanaogopa katika kila kona, kwa hiyo ni muhimu sana kuwa na makongamano ya aina hii ambayo yanaleta wadau mbalimbali ili kuweza kujadili mambo haya.”
Afisa Programu wa Tanganyika Law Society (TLS), Wakili Mercy Kessy, anasema taasisi hiyo imeendelea kushirikiana na Serikali, Bunge na Mahakama katika kutoa mapendekezo ya maboresho ya sheria yanayolenga kuimarisha mfumo wa haki nchini.
“Tunahakikisha kuwa tunaisaidia hii serikali, tunaisaidia mahakama, tunalisaidia bunge katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na hayo maboresho ya sheria. Kwa hiyo tumekuwa tukihusika moja kwa moja. Ikitokea pale ambapo kunahitajika maboresho ya sheria, Bunge, Mahakama hata Serikali wanakuja moja kwa moja Tanganyika Law Society kuhakikisha kwamba sisi kama wanasheria tunatoa maoni yetu ambayo sasa yanaenda kufanyiwa kazi katika zile sheria ambazo zinahitaji kupatiwa maboresho.”
Mjumbe wa Baraza Linaloongoza la Tanganyika Law Society (TLS), Wakili Barnabas Nyalusi, amesema kampeni hiyo itasaidia kujenga uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia Katiba na sheria kwa njia ya maelewano.
“Tunafurahi au tunashukuru kuwa sehemu ya kampeni hii kwa sababu itasaidia hata wanachama wetu kuhimiza utii wa Katiba bila kukosana na kuingia kwenye mtafaruku na wanaosimamia sheria.”
Waandaaji wa kampeni hiyo wameeleza kuwa maeneo matatu makuu yatakayopewa kipaumbele ni kutambua na kulinda watetezi wa haki za binadamu, kukuza uhuru wa vyombo vya habari na kulinda uhuru wa kujieleza, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama na kuhimiza mageuzi ya sheria zinazogusa haki za wananchi.
Katika eneo la mageuzi ya sheria, kampeni hiyo pia itafuatilia utekelezaji wa maamuzi ya mahakama kuhusu sheria mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Usajili wa Kuzaliwa na Vifo (BRADEA), Sheria ya Ndoa pamoja na sheria nyingine zinazohusu ulinzi wa haki za msingi za binadamu.
Waandaaji wanasema kampeni hiyo itakuwa jukwaa la kuimarisha majadiliano shirikishi kati ya Serikali, taasisi za sheria, mashirika ya kiraia, wanahabari na wananchi kwa lengo la kuendeleza utawala wa kidemokrasia, kuheshimu misingi ya Katiba na kuharakisha mageuzi ya sheria yanayochochea upatikanaji wa haki kwa wote.
Aidha, wametoa wito kwa taasisi za Serikali, washirika wa maendeleo, mashirika ya kiraia, jumuiya ya wanasheria, taasisi za elimu, vyombo vya habari na wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni hiyo ili kujenga jamii inayozingatia Katiba, kulinda haki za binadamu na kuimarisha utawala wa sheria nchini.
